27.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, May 21, 2024

Contact us: [email protected]

‘Bundi si uchuro, ni fursa kiuchumi’

Na Faraja Masinde, Muheza

Jamii imetakiwa kumtazama ndege aina ya bundi kama fursa na kubadili dhana iliyojengeka kuwa ni uchuro anapotua kwenye makazi.

Hayo yamebainishwa juzi wilayani Muheza mkoani Tanga na baadhi ya wananchi wa vijiji vinavyozunguka Hifadhi ya Taifa ya Mazingira ya Misitu ya Amani walipotembelewa na waandishi wa habari wa Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET).

Walisema Watanzania wanapaswa kumuona ndege huyo kama fursa kwani ana faida mbalimbali, ikiwamo kukuza uchumi na kudhibiti panya waharibifu wa mazao.

Mmoja wa wananchi hao, Abdallah Mfaume, kutoka kijiji cha Magoda, alisema bundi ni ndege anayewaletea kipato na Serikali kwa ujumla kupitia shughuli za utalii.

“Bundi ni ndege ambaye anatuletea kipato ndani ya kijiji na Taifa kwa sababu amekuwa kivutio kikubwa cha utalii na pindi watalii wanapokuja kutembelea katika shoroba yetu inatupa mapato yanayoingia serikalini na hapo kuna asilimia 5 inayorudi kijijini.

“Ni kweli kwamba zamani wakati tunakua sisi tuliaminishwa kuwa bundi ni ndege ambaye ana uchoro na anapotokea amelia jirani na nyumba basi kuna changamoto. Lakini baada ya kupata elimu, kwa sasa bundi tunamuona kama ndege rafiki na fursa pia,” amesema Mfaume.

Baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Sekondari Shebomeza wilayani Muheza wakiangalia ndege wanaopatikana katika hifadhi hiyo kwa kutumia kifaa maalum.

Veronica Shunda anayesoma kidato cha kwanza ni kati ya wanafunzi walioko katika Klabu ya kutunza mazingira katika Shule ya Sekondari Shebomeza iliyoko kijiji cha Amani, amesema watu hawatakiwi kumuogopa bundi kwa sauti yake kwani hiyo huwa ni kiashiria cha usalama.

“Bundi anapokuwa analia huwa ni sababu mbili. Kwanza, anataka kuwajulisha wengine kwamba yupo hapo. Pili, huwa ni kutaka kujihami, hivyo watu hawatakiwi kuogopa kabisa ndege huyu,” amesema.

Edigar Apolinary ni Afisa Mfuatiliaji kutoka Shirika la Nature Tanzania katika Hifadhi ya Misitu Asilia ya Amani, ambapo amesema kuwa bundi anayepatikana katika hifadhi hiyo ni ‘Usambara Eagle Owl’ ambaye huwezi kumpata sehemu nyingine duniani mbali na Tanzania na kwamba ana faida lukuki tofauti na watu wanavyodhani.

Akitaja moja ya faida ya bundi, Apolinary amesema ni kuondoa wadudu waharibifu kama panya ambao wanaharibu mazao. “Bundi anaweza kula panya wengi sana na na hivyo kusaidia changamoto ya uharibifu wa mazao na mazingira inayosababishwa na panya kupungua.

“Kitu kingine, bundi anasaidia katika nyanja ya utalii kwa sababu watu wengi wanakuja kumuangalia bundi. Anapatikana tu hapa katika milima hii ya Usambara Mashariki, sasa ile dhana ya watu kwamba bundi anasababisha uchuro siyo kweli.

“Watu wengi wanadhani kwamba kwa kutoa sauti kubwa ya kuogopesha na kupatikana kwake tu usiku ikiwamo macho yake ya kuogopesha kwamba anasababisha uchuro. Hapana, siyo kweli kabisa. Ndiyo maana tunafanya kazi kubwa ya kuelimisha watu,” amesema Apolinary.

Ameongeza kuwa muda mwingi ili kumuona bundi huyo watalii hulazimika kumfuata usiku na tochi kwani ndiyo huonekana kirahisi. “Muda mwingine huwa tunafuata sauti kwani akilia sauti yake huwa ni kubwa sana popote ulipo utamsikia tu kwa hiyo inakuwa ni rahisi kwetu,” amesema.

Akizungumzia utalii wa ndege katika hifadhi ya mazingira asilia ya Amani, ambayo ndiyo ya kwanza kuanzishwa nchini na ya 25 kidunia kwa kuhifadhiwa vizuri, Kaimu Mhifadhi katika Hifadhi hiyo, Alphonce Nyululu, amesema kuna aina ya ndege zaidi ya 340, ikiwamo bundi.

“Watalii wanaokuja, hasa wanakuja katika sehemu tatu. Kwanza, utalii wa ndege ambapo wanakuja kumuangalia bundi huyu wa Usambara Eagle Owl, ambaye amekuwa kivutio cha watu wengi na kutuongezea mapato.

“Mfano, kutoka mwaka wa fedha 2007-8 hadi 2022-3, Hifadhi ilipokea watalii 14,096 na tulipokea Sh milioni 538,093,400 hadi kufikia Juni, mwaka huu,” amesema Nyululu.

Mkurugenzi Mtendaji wa JET, John Chikomo(kulia) akiangalia moja ya ndege wanaopatikana katika hifadhi hiyo.

Akizungumzia ziara hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa JET, John Chikomo, amesema imekuwa ni fursa nzuri kwa wanahabari kutembelea misitu ya Amani Nilo kwani wamejifunza mambo mengi, ikiwamo umuhimu wa kutunza na kulinda ndege ambao wako hatarini kutoweka.

“Tulikuja kwenye Hifadhi ya Misitu Asilia ya Amani Nilo na tumejionea vivutio mbalimbali ambavyo vinawavutia watalii na havipatikani kokote duniani. Tumeona baadhi ya ndege ambao wameainishwa katika dawati la IUCN kuwa wako hatarini kutoweka, lakini hapa wanapatikana.

“Hivyo kuna umuhimu kwa waandishi wa habari kutembelea eneo hili ili kuhabarisha umma wa Watanzania kuhusu vivutio hivi. Pia, kazi kubwa inayofanywa na wadau mbalimbali wakiwamo USAID kupitia mradi wa Tuhifadhi Maliasili, kuhakikisha eneo hili linabaki katika uhalisia wake,” amesema Chikomo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles