Na RAPHAEL OKELLO – BUNDA
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha Akiba na Mikopo cha Bunda Saccos, Abas Kakwaya amewataka wanachama 122 wa chama hicho kurejesha haraka Sh milioni 300 wanazodaiwa ili kukinusuru chama hicho kufilisika.
Alisema miongoni mwa wadaiwa wakubwa ni waliowahi kushika nadhifa ya uenyekiti na watumishi wa Saccos hiyo akiwamo meneja.
Kwa mujibu wa Abas, Saccos hiyo ilikuwa na watumishi sita kufikia mwanzoni mwa mwaka huu lakini kutokana na kukopa na kushindwa kulipa wametoroka na kubakia mtumishi mmoja tu kwa sasa. Alisema taarifa zao zote zimekwisha kupelekwa polisi.
Akizungumza katika mkutano wa dharura wa Saccos hiyo juzi, alisema wenyeviti hao na watumishi wasiofika watu 10 wanadaiwa takriban Sh milioni 100 kati ya wanachama 122 wenye madeni.
Hata hivyo, alisema Saccos hiyo inadaiwa na wanachama wake akiba ya Sh milioni 230. Mkutano huo uliwataka wanachama hao wawe na subira wakati madeni yanaangaliwa jinsi ya kurejeshwa.
Abas alisema wanaoidai Saccos hiyo watarejeshewa fedha zao kidogo kidogo kadri zitakavyokusanywa.
Makamu mwenyekiti huyo alisisitiza a kwamba Bunda Saccos haijafilisika ingawa imesimamisha huduma ya kutoa mikopo ingawa huduma nyingine zinaendelea.
“Ieleweke kwamba tumesimamisha tu huduma ya kutoa mikopo, tutaendelea na huduma yetu ya uwakala wa M pesa na huduma nyingine.
“Mtumishi wetu na bodi ya Saccos anaendelea na kazi kama kawaida kwa hiyo wanachama Msihofu,” alisisitiza Abas.
Katika mkutano huo, Abas alisema bodi inaingia mkataba wa kukusanya madeni hayo na Kampuni ya Makama Investiment.
Alisema lengo la kufanya hivyo ni kuinusuru Saccos hiyo kubwa wilayani Bunda kutowekwa chini ya Mfilisi.
Aliwataka wenyeviti na watumishi hao kuwa mfano kwa wanachama wengine kurejesha mikopo yao kwa haraka.
Mmmoja wa wajumbe, Siri Makanaki alisema wenyeviti na watumishi wa Saccos wamechangia kwa kiwango
kikubwa kuifikisha Saccos hiyo katika hali mbaya.