Na PATRICIA KIMELEMETA
MAHAKAMA ya Rufaa imetupilia mbali rufani iliyowasilishwa na wapiga kura wanne katika kesi ya kupinga matokeo ya Jimbo la Bunda katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba, mwaka juzi.
Katika kesi hiyo, wapiga kura hao, ambao ni Magambo Masato, Matwiga Matwiga, Janes Ezekiel na Escietik Malagila, wakiwakilishwa na Wakili wao, Constantine Mutalemwa, waliwasilisha hoja 10, ikiwamo ya kuiomba mahakama hiyo kutengua matokeo yaliyompa ushindi Mbunge wa Jimbo hilo kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Ester Bulaya.
Maombi hayo yaliwasilishwa mbele ya jopo la majaji watatu ambao ni Mbarouk Mbarouk, Rehema Mkuye na Augustino Mwarija.
Akisoma hukumu hiyo kwa zaidi ya dakika 45 jana, Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufaa, Elizabeth Mkwizu, alisema hoja 10 zilizowasilishwa na upande wa walalamikaji hazina mashiko na zimetupiliwa mbali.
Alisema kutokana na hali hiyo, walalamikaji hao wanatakiwa kulipa gharama zote za uendeshaji wa kesi hiyo.
“Baada ya jopo la majaji kukaa na kupitia hoja zote zilizowasilishwa mahakamani hapa za upande wa walalamikaji na utetezi, wameona kuwa hoja 10 zilizowasilishwa na wapiga kura hazina mashiko, zimetupiliwa mbali.
“Kutokana na hali hiyo, wanapaswa kulipa gharama zote za uendeshaji wa kesi hii,” alisema Mkwizu.
Katika kesi hiyo, wapiga kura hao wanaomuunga mkono aliyekuwa mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Stephen Wassira, kupitia kwa Wakili wao, Mtalemwa, waliiomba mahakama hiyo pia kufuta uamuzi wa kukataa kesi ya uchaguzi uliotolewa na Mahakama Kuu Kanda Mwanza na kuelekeza kuwa matokeo ya uchaguzi yafutwe na uchaguzi kurudiwa kwa gharama.
Wakili Mutalemwa alidai kuwa, katika uchaguzi huo kulikuwa na kasoro kubwa ambapo fomu ya mwisho ya matokeo ya ubunge yalionyesha idadi ya wapiga kura isiyo sahihi ya 164,794, badala ya ile iliyotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ya wapiga kura 69,369.
Alidai kasoro hiyo imeweza kuathiri matokeo ya uchaguzi wa jimbo zima kwa sababu idadi halisi ya wapiga kura iliyotolewa na NEC ndiyo msingi mzima wa utaratibu wa matokeo kabla ya kutangazwa.
Alidai jaji wa mahakama ya chini hakuzingatia kifungu cha 115 cha Sheria ya Ushahidi kwa kuwa kulikuwa na malalamiko ya matokeo ya uchaguzi yafutwe na kwamba Bulaya hakuzingatia matakwa ya sheria ya uchaguzi kwa kushindwa kueleza bajeti yake ya uchaguzi.
Alidai kutokana na hali hiyo, wateja wake hawakubaliani na maelezo yaliyotolewa na jaji wa mahakama ya chini.
Alidai Bulaya alikuwa na jukumu la kuthibitisha kama ametimiza masharti hayo, tofauti na jaji alivyohitimisha kwamba halikuwa jukumu lake bali la walalamikaji.
Alidai mgombea Wassira hakualikwa katika mchakato wa kujumlisha kura, suala lililoathiri matokeo ya uchaguzi kwa kushindwa kumtambua mgombea wala chama chake.
Alidai kuwa jaji alitafsiri vibaya kwa kukataa kutumia mamlaka yake kuamuru idadi ya kura kuletwa mahakamani ili kupata idadi ya kura zilizoharibika.
Hata hivyo, upande wa utetezi, ukiongozwa na Wakili Tundu Lissu, ulikiri kuwapo kwa makosa ya idadi ya wapiga kura katika fomu namba 24 B, hata hivyo, alidai makosa hayo hayajitoshelezi kutengua matokeo ya uchaguzi.
“Mahakama hii imeeleza mara nyingi katika kesi mbalimbali kuwa kanuni kuu ya kutengua matokeo ya uchaguzi ni kwamba si kila kosa linalofanywa katika Sheria ya Uchaguzi linahalalisha matokeo kufutwa,” alidai.
Lissu alidai si kila dhambi chini ya sheria ya uchaguzi, mshahara wake mauti ya uchaguzi, hivyo basi kukosea kujaza fomu ya matokeo ya watu waliojiandikisha kupiga kura, kweli ilithibitishwa kulikuwa na makosa hayo, lakini si sababu ya kufutwa matokeo.
Pia alidai walalamikaji walikuwa na wajibu wa kuthibitisha iwapo mjibu rufani wa kwanza (Bulaya) ametimiza masharti ya sheria ya uchaguzi kwa kuwa taarifa zake zipo kwa msajili wa vyama vya siasa nchini ambaye ana taarifa za wagombea wote na katibu tawala wa wilaya.
Lissu alidai mgombea wa CCM alipewa taarifa ya mahali ambapo kura zitahesabiwa kwa kuwa ilipelekwa ofisi ya chama hicho.
Wakili huyo aliiomba mahakama hiyo kutupilia mbali rufani hiyo, kutokana na sababu alizozieleza kuwa gharama na mteja wake apatiwe gharama zake za mahakama ya chini.
Katika kesi hiyo, upande wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) uliwakilishwa na Mawakili Obadia Kamea na Angela Msagala.