24.9 C
Dar es Salaam
Wednesday, May 22, 2024

Contact us: [email protected]

Brigedia Jenerali Mbita afariki dunia

mbitaJonas Mushi na Patricia Kimelemeta, Dar es Salaam

MMOJA wa Watanzania waliofanikisha ukombozi wa nchi za Kusini mwa Afrika,Brigedia Jenerali Hashim Mbita (82), alifariki dunia jana katika Hospitali Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Lugalo ambako alikuwa amelazwa kwa muda mrefu.

Akizungumza na MTANZANIA nyumbani kwa marehemu Chang’ombe Madukani Dar es Salaam jana, mtoto wa marehemu Iddi Mbita alisema baba yake alifariki dunia saa 3:30 asubuhi baada ya kusumbuliwa kwa muda mrefu na shinikizo la damu.

“Mzee amekuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa presha kwa miezi minane sasa…tulikuwa tukimpeleka nje ya nchi kutibiwa lakini hali ilikuwa inabadilika kila mara,”alisema Mbita.
Alisema siku tatu kabla ya baba yake kufariki dunia hali yake ilikuwa mbaya hadi kushindwa kula chakula huku akilazimika kulishwa kwa mipira.

Akizungumzia utaratibu wa maziko, alisema kesho baada ya ibada itakayofanyika katika msikiti wa Kwamtoro, mwili wa marehemu Mbita utapelekwa kuzikwa katika makaburi ya Kisutu.

RAIS AMLILIA

Wakati huohuo, taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu, ilisema Rais Jakaya Kikwete ameagiza Serikali na JWTZ kushirikiana na familia kusimamia msiba huo.

Katika taarifa hiyo, Rais Kikwete amesema marehemu Mbita alikuwa mtumishi wa miaka mingi wa Serikali,jeshi,Chama cha TANU na Kamati ya Ukombozi ya Umoja wa Afrika.

Katika Chama cha TANU aliwahi kuwa Katibu Mtendaji wake.
Pia alijiunga na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ambamo alipitia nafasi mbalimbali hadi kufikia cheo cha Brigedia Jenerali.
Taarifa hiyo ilisema marehemu Mbita alikuwa mtu wa kwanza kwenda kupigania uhuru katika nchi zilizokuwa zikipigania uhuru zikiwamo Msumbiji, Zimbabwe, Angola na Afrika Kusini.

Rais Kikwete pia ameitumia salamu za rambirambi familia ya marehemu Mbita akieleza kuwa ni miongoni mwa watu wachache watakaokumbukwa kwa uongozi uliotukuka.

“Ni wachache katika nchi yetu wanaoweza kulinganishwa na mzee Mbita kwa kiwango cha utumishi uliotukuka wa miaka mingi na usiokuwa na kasoro. Katika utumishi wa Serikali alipata kuwa Mwandishi wa Habari Mkuu wa Idara ya Habari, Mwandishi wa Habari wa Rais na baadaye Balozi wa Tanzania nchini Zimbabwe. Kazi zote alizifanya kwa ufanisi mkubwa sana,”ilisema taarifa ya Ikulu.

Marehemu Mbita ameacha watoto sita na mjane mmoja.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles