Na LEONARD MANG’OHA – DAR ES SALAAM
BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imetoa ufafanuzi kuhusu kushuka kwa thamani ya shilingi dhidi ya dola ya Marekani na kwamba hali hiyo ni ya kawaida.
Taarifa ya benki hiyo iliyotolewa jana, ilidai kuwa kushuka kwa thamani ya sarafu ya Tanzania dhidi ya Dola ya Marekani kunatokana na kupungua kwa utalii na mauzo ya nje ya mazao katika msimu huu.
“Hivi karibuni thamani ya shilingi dhidi ya fedha za kigeni, hususan Dola ya Marekani imekuwa ikipungua na kusababisha mijadala katika magazeti na mitandao ya kijamii. Mijadala hiyo inaonesha kwamba ama shilingi iko kwenye hali mbaya, ama kuna upungufu wa akiba ya fedha za kigeni nchini.
“Benki Kuu ya Tanzania inapenda kuutarifu umma kwamba mwenendo wa thamani ya shilingi dhidi ya Dola ya Marekani kunatokana na msimu huu ambapo mapato ya fedha za kigeni yanayotokana na utalii na mauzo ya nje ya mazao hupungua.
“Hali hii ni ya kawaida na hubadilika kuanzia sehemu ya pili ya kila mwaka, mapato ya fedha za kigeni yatokanayo na utalii na mauzo nje huongezeka,” ilieleza taarifa hiyo.
Taarifa hiyo iliongeza kuwa kwa siku za karibuni Dola ya Merakani imekuwa ikiimarika thamani na kufanya fedha za nchi nyingine kupungua thamani.
Hata hivyo taarifa hiyo iliongeza kuwa Tanzania ina akiba ya kutosha ya fedha za kigeni, ambayo inaweza kugharamia ununuzi wa bidhaa na huduma kutoka nje kwa kipindi cha miezi 4.9.
“Kiwango hiki ni juu zaidi ya kiwango kinachotakiwa kwa nchi yetu cha uwezo wa kununua bidhaa na huduma kutoka nje kwa muda wa miezi minne na kile cha Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) cha miezi 4.5.
“Ieleweke pia kwamba kiwango cha kubadilisha fedha huamuriwa na nguvu za soko zinazotokana na mahitaji na kiwango cha fedha za kigeni kilichoko sokoni. Benki Kuu ya Tanzania hushiriki mara kwa mara katika soko kwa ajili ya kuhakikisha kuna utulivu katika kiwango cha kubadilisha fedha kuendana na vigezo vya kiuchumi,” iliongeza taarifa hiyo.
BoT ilieleza kuwa itaendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa thamani ya shilingi dhidi ya fedha za kigeni katika soko na kuhakikisha washiriki katika soko hilo wanazingatia kanuni na maadili ya uendeshaji wa soko la fedha za kigeni.