28.1 C
Dar es Salaam
Thursday, December 2, 2021

Shule za Serikali zazidi kuporomoka

Na ANDREW MSECHU – Dar es Salaam

HALI ya shule za Serikali inazidi kuwa mbaya kila mwaka. Katika mtihani wa taifa wa kidato cha nne uliofanyika Novemba mwaka jana, zilizopenya kwenye kundi la 200 bora ni saba pekee.

Shule hizo ni zile zilizo kwenye kundi la shule zenye watahiniwa zaidi ya 40, ambazo kwa mwaka jana zilikuwa 3,488.

Kwa mujibu wa matokeo ya mtihani wa kidato cha nne wa kuanzia mwaka 2016, unaonyesha shule za Serikali inazoingia kwenye mia 100 hazizidi sita huku nyingi zikiwa ni kongwe.

Hata hivyo shule hizo zimeendeela kushuka kila mwaka, licha ya Serikali kufanya juhudi za kuziboresha.

Kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa na Katibu Mtendaji wa Baraza na Mitihani la Taifa (Necta) Januari 25, mwaka huu, Sekondari ya Ilboru ndiyo shule ya kwanza ya Serikali ikishika nafasi ya 36 katika 200 bora.

Shule nyingine na nafasi zake kwenye mabano ni Kibaha (45), Mzumbe (48), Tabora Boys (67), Kilakala (76), Tabora Girls (90) na Msalato (102) ambayo ndiyo ya mwisho kwenye kundi la shule zilizo kwenye 200 bora.

Katika mtihani wa mwaka juzi, shule ya kwanza ya Serikali ilikuwa Mzumbe (21), Kibaha (31), Ilboru (39), Kilakala (40), Tabora Boys (60) na Tabora Girls (66) ikifunga fungu la shule zilizopenya 100 bora kwa zile zenye watahiniwa zaidi ya 40.

Mwaka 2016 ambao shule hizo kidogo zilifanya vizuri kidogo ikilinganishwa na sasa, shule ya kwanza ilikuwa Kibaha iliyoshika nafasi ya 16, Mzumbe (27), Kilakala (28) Kibosho Girls (36), Tabora Boys (41) na Ilboru (42).

WADAU WAZUNGUMZA

Mhadhiri wa Chuo Kikuu Katoliki cha Ruaha, Profesa Gaidence Mpangala, alisema historia ya elimu ya nchi hii inayumba kwa sasa kwa sababu katika miaka ya 1970 hadi 1980 ambayo hata yeye alikuwa akishiriki kusahihisha mitihani ya wanafunzi wa shule za sekondari, wanafunzi wa shule za Serikali ndio waliokuwa wakifanya vizuri zaidi.

Alisema ni kweli kwamba walikuwa wakiingia kusahihisha mitihani walikuwa wakianza na ya wanafunzi wa shule za Serikali kwa sababu kwanza ilikuwa haiwaumizi kichwa ndipo wanapokuja katika mitihani ya wanafunzi wa shule binafsi, lakini inaonekana sasa mambo yamebadilika sana.

Mhadhiri huyo alisema pamoja na mkakati wa kutoa elimu bure kwa wanafunzi wa shule za Serikali, kwa sasa inaonekana upande wa shule hizo umekumbwa na matatizo mengi, la kwanza likiwa ni kutokuwepo kwa motisha kwa walimu, hatua inayowafanya wengi kutofundisha kwa moyo na kutumia muda mwingi kwenye miradi yao ya kuwaongezea kipato.

“Kwa mtindo huo, mimi mwenyewe nimewahi kumuhamisha mtoto wangu kutoka shule ya Serikali kwenda shule binafsi, kwa sababu mtoto analalamika kuna walimu wa baadhi ya masomo ya muhimu wanaingia darasani hadi mara mbili kwa mwezi, sasa katika hali kama hiyo wanatarajia mwanafunzi afanye juhudi zake binafsi ili afaulu, suala ambalo si rahisi. Ni wanafunzi wachache wanaoweza kufanya hivyo,” alisema.

Alisema ni wazi kwamba nidhamu ya walimu imeshuka sana kutokana na Serikali kutojali mazingira yao ya kazi na kutowapa motisha, hivyo isitarajie muujiza katika hilo, bali inatakiwa kutoa motisha na kuhakikisha shule zinapatiwa walimu wa kutosha wa fani zote pamoja na vifaa vinavyotakiwa kufundishia wanafunzi.

Akitoa ufafanuzi, Profesa Mpangala alisema kumekuwa na ongezeko kubwa la shule za Serikali katika utaratibu wa shule za kata, lakini bado hazina walimu wa kutosha wa masomo yote, pia hazina vifaa vya kufundishia na maabara, suala ambalo lisipotafutiwa ufumbuzi shule za Serikali zitaendelea kushika mkia na zile za binafsi zitaendelea kuongoza.

Alisema inaonekana kuna tatizo kwenye sera ya elimu kuhusu walimu kwa sababu walimu wengi waliomaliza vyuo bado wanarandaranda mitaani na hawaajiriwi wakati kukiwa na upungufu mkubwa wa walimu katika shule nyingi za Serikali, huku waliopo kwenye ajira wakiwa hawafurahii ajira zao kutokana na kutokuwepo mazingira mazuri ya utendaji kazi na kukosa motisha.

KAULI YA WIZARA

Kutokana na hali hiyo, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk. Avemaria Semakafu, jana aliliambia gazeti hili kuwa shule za Serikali haziwezi kulinganishwa na shule binafsi kwa sababu za Serikali hubeba wanafunzi wote kwa wingi wake bila kufanya mchujo wowote.

Alisema shule hizo zimekuwa zikipika wanafunzi vizuri kwa pamoja bila kuwachuja na kuwapa wote uwezo wa kufanya vizuri, tofauti na shule za binafsi ambazo zimekuwa zikifanya mchujo kila mara na kuwaacha wanafunzi wengine, hivyo kubaki na wale wanaowahitaji wao.

“Hizi shule za Serikali ndizo zinazojua kupika kwa sababu zinapika bila kuchekecha, ndizo zinazochukua wanafunzi hata wale wenye uwezo mdogo na kuwapika na bado utaona kuna daraja la kwanza wa kutosha, la pili wa kutosha na hata la tatu. Wapishi hawa wanaopika bila kuchekecha ndio wapishi wazuri wanaostahili kusifiwa,” alisema.

Dk. Semakafu alisema dhana ya kusema kuwa shule binafsi ndizo shule bora kwa sababu zinaonekana kushika nafasi za juu si sahihi kwa sababu si kwamba zina wafundishaji wazuri, bali kazi yao ni kuchuja tu wanafunzi na kuacha wale wanaodhani kuwa wanafaa.

Alisema zingeweza kuwa shule bora iwapo tu zingeweza kuchukua wanafunzi na kuwapekela mbele hadi kumaliza kidato cha nne bila mchujo na kuhakikisha kwamba wote wanafanya vizuri.

“Kwa sasa hivi Serikali inafuatilia waraka wake wa Januari 2018 ulioagiza shule hizi kuacha kuchuja wanafunzi hadi wazazi watakaporidhia wenyewe,” alisema na kuongeza kuwa wamebaini bado zipo baadhi ya shule ambazo zinafanya ‘uhuni’ huo, ambazo ushahidi ukikamilika zitachukuliwa hatua za kisheria. Alisema wanaendelea kufanya maboresho ya mazingira ya elimu kwa shule za Serikali ambayo kwa siku zijazo yatatoa mwanya kwa wanafunzi kufanya vizuri zaidi.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,663FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles