Na Mwandishi Wetu
BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imetoa taarifa yake ya kuishia Julai, mwaka huu huku ikionyesha kuwa mfumuko wa bei umekuwa ukipungua kwa kiwango cha wastani tangu Aprili, mwaka huu.
Taarifa hiyo inayopatikana katika tovuti ya BoT inaonyesha kuwa kiwango cha mfumuko wa bei hadi Julai, mwaka huu ulikuwa umepungua hadi kufikia asilimia 5.2 kutoka asilimia 5.4 ya awali.
Taarifa hiyo ilisema kupungua kwa mfumuko wa bei kulisababishwa na upungufu wa bei za vyakula na vinywaji visivyo pombe na inaonyesha kuwa Julai, mwaka huu ilionesha upungufu wa asilimia 0.2 ukilinganisha na Julai, mwaka jana.
Pia taarifa hiyo ilisema kuwa kiwango cha mfumuko wa bei kwa vyakula na vinywaji hadi Julai, mwaka huu kilikuwa asilimia 8.9 ukilinganisha na asilimia 7.6 ya Julai, mwaka jana.
Pia ilisema mfumuko wa bei usiotokana na vyakula ulipungua hadi asilimia 3.1 kutoka asilimia 3.2 ya Julai, mwaka jana huku mfumuko wa bei ya nishati na mafuta ulishuka hadi asilimia 8.8 Julai, mwaka huu toka asilimia 10.3 Juni, mwaka huu.
Pia ilisema mfumuko wa bei kwa bidhaa zote isipokuwa vyakula kwa kipindi cha mwaka mzima umepanda hadi asilimia 2.2 kutoka asilimia 1.9 Juni, mwaka huu lakini ilikuwa chini zaidi kuliko iliyokuwa Juni, mwaka jana yaani asilimia 2.6.
Pia ripoti hiyo ilisema akiba ya chakula katika Wakala wa Taifa Hifadhi ya Chakula (NFRA) ilikuwa tani 68,697 huku bei ya vyakula vya mazao ilishuka Julai, mwaka huu ukilinganisha na Juni, mwaka huu.