30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

ZITTO: TAKWIMU ZA UCHUMI ZIMEPIKWA

 

Na AGATHA CHARLES-Dar es Salaam

KIONGOZI wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, amesema kuna taarifa za kupikwa kwa takwimu za Pato la Taifa kwa robo ya pili ya mwaka huu, ili kuonyesha kuwa hali ya uchumi ni nzuri.

 

Kauli hiyo aliitoa katika mkutano wa kutoa maazimio ya Kamati ya Uongozi kwa waandishi wa haabri uliofanyika Makao Makuu ya chama hicho, Kijitonyama, Dar es Salaam jana.

 

“Kamati ya uongozi ilitaarifiwa pia kuwa takwimu za hivi karibuni za pato la taifa zilizotolewa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) zina shaka, ikiwamo kupikwa kwa takwimu ili kuonyesha kuwa hali ni nzuri wakati sivyo,” alisema.

 

Zitto alisema hali ya uchumi ni mbaya, thamani ya shilingi imepoteza uwezo wake, mfumuko wa bei umepanda kwa kasi, hasa vyakula na mahitaji muhimu.

 

Alitaja maeneo mengine yanayoporomoka kuwa ni uzalishaji katika kilimo, mikopo kwa sekta binafsi, uzalishaji katika sekta ya viwanda ambao umeshuka zaidi ya nusu, huku mapato ya Serikali yakididimia.

 

Zitto alisema taarifa ya Serikali iliyotolewa katika kipindi cha Juni hadi Julai, mwaka huu kuhusu mikopo katika sekta binafsi inaonyesha ukuaji wa mikopo imeporomoka kutoka asilimia 24 hadi sifuri.

Alisema madhara ya kuporomoka kwa mikopo yataathiri viwanda katika uzalishaji wake.

 

“Yote hayo yanatokea katika wakati ambao haki za kiraia na uhuru wa kidemokrasia vinazidi kubanwa na tumeshuhudia magazeti yakifungiwa, uwapo wa mswada mbaya wa sheria mpya ya vyama vya siasa, mauaji holela ya raia pamoja na kushambuliwa kwa wote wanaoonekana kuihoji Serikali,” alisema.

 

Pia alisema ripoti hiyo ya robo ya pili ya mwaka yaani Juni, Mei na Aprili, mwaka huu wameshaifanyia utafiti tayari kwa kuwa ni suala la kisera na litawakilishwa katika Kamati Kuu ya chama hicho.

 

“Tumegundua kasi ya ukuaji wa uchumi wa asilimia 5.7 kiuhalisia ni mbaya zaidi si nne, tatu, mbili wala si moja. Uchambuzi umekamilika na tumewasiliana na wachumi mbalimbali kwa ajili ya kutazama jambo hilo kabla ya kulisema. Tutakapoliwakilisha Kamati Kuu mtaweza kulipata na liko katika lugha nyepesi hata mtu wa kawaida atalielewa kwanini tunasema takwimu zimepikwa. Hakuna ukuaji kati ya Aprili hadi Juni, mwaka huu,” alisema.

 

Pia alisema moja ya suala la uchumi atakaloliwasilisha katika Kamati Kuu ya chama hicho ni taarifa za kuchotwa kwa fedha za mashirika ya umma na kutumiwa na Serikali bila kufuata sheria.

 

“Kuna mashirika matano hadi sasa hayana fedha za kujiendesha, tumekubaliana hilo nitaliwasilisha katika Kamati Kuu ya chama na litajadiliwa kisha nikaliwakilishe bungeni,” alisema.

 

Pia alisema suala hilo linahitaji muda kujadiliwa na kwa kuwa ni jambo linalovunja misingi ya sheria za fedha na linatokana na kuwa na Bunge dhaifu.

 

“Kamati ya Bunge ya Bajeti ina uwezo wa kudhibiti hilo iwapo Bunge ni imara,” alisema.

 

Katika hatua nyingine, alisema wataendelea kuikosoa Serikali ya Rais Dk. John Magufuli kwa kuainisha upungufu wake na kutoa sera mbadala kama upinzani unavyopaswa kufanya.

 

Zitto alisema kazi hiyo imefanyika vyema katika kipindi cha mwaka huu na kuwa mwiba kwa chama tawala na Serikali, kutokana na namna ambavyo wamekuwa wakizisema sekta zote, ikiwamo binafsi.

 

Alisema chama hicho kimekuwa kikishughulikia masuala mbalimbali, ikiwamo kilimo na kimekuwa kikiwakanya watawala ambao ndio wanaoshughulikia sera na kuzitekeleza.

“Huwezi kushughulikia masuala ya kilimo bila kumgusa waziri wa kilimo, huwezi kushughulikia suala la uchumi unavyodidimia bila kumgusa mkuu wa nchi, kwa hiyo inawezekana misingi tunayoikiuka ni kuwasema watawala, hatuwezi kukwepa kukosoa au kusema viongozi wanaotawala, sisi ni chama cha upinzani. Wanaoona utawala wa sasa mzuri wasiwakwaze wanachama wanaoona haufai kwa sababu unaua uchumi na kuminya haki za watu.

 

“Tunawaasa wote wanaodhani kuwa chama hiki kitakuwa jukwaa la kusifia chama tawala na Serikali kuwa si jukwaa sahihi kwao, wajitathmini ama kuendelea na uanachama au wajivue kama wenzao wanavyofanya,” alisema.

 

Akizungumzia mwenendo wao na malalamiko, yakiwamo ya baadhi ya viongozi wake kukiuka misingi ya kuanzishwa kwake yaliyotolewa na Samson Mwigamba, aliyekuwa mmoja wa viongozi wa chama hicho, ambaye na wenzake tisa walikihama wiki hii na kujiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM), Zitto alisema baada ya tathmini wamegundua kipo sahihi kwa asilimia 100.

 

Zitto alisema baada ya tuhuma hizo, chama hicho kiliitisha Kamati ya Uongozi ili kujitathmini na kugundua kuwa kinaendelea kusimamia misingi 10 iliyoko katika katiba ya chama hicho, ikiwamo uzalendo, usawa wa kiuchumi kwa raia, kupinga ubaguzi wowote, ikiwamo wa dini, mrengo wa kisiasa au kipato.

Alitaja misingi mingine kuwa ni kupigania haki za kidemokrasia, uhuru wa mawazo na matendo, kupigania uwazi serikalini pamoja na kusimika uadilifu kisheria inayoongozwa na utu na kuleta umoja kwa Watanzania.

 

Pia alisema hilo linaongozwa na ahadi tano za mwanachama, ikiwamo kupambana na dhuluma, kujenga taifa la kujitegemea, kujenga umoja wa Afrika na demokrasia ndani na nje ya chama.

Alisema wanaoondoka ndani ya chama hicho wanapaswa kuacha kuwashawishi wanachama wengine kuondoka au kutoa tuhuma za uongo.

“Mwanachama ambaye safari imemshinda ashuke mwenyewe badala ya kujaribu kulichoma gari moto ili na sisi tunaoamini kwenye safari tushindwe kuendelea na safari,” alisema.

 

Kuhusu uchaguzi wa madiwani, alisema chama hicho kitashiriki katika kampeni za uchaguzi wa marudio katika kata 43 za mikoa mbalimbali nchini.

Alisema chama hicho kitazindua kampeni hizo Oktoba 29, mwaka huu, eneo la Kijichi, Dar es Salaam na kitapigania kuelimisha namna ya kuukataa utawala wa kiimla aliodai unanyemelea nchi.

 

Naye Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Zanzibar, Hamad Yussuf, alisema Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira, ambaye pia ni mwanachama wao, anapaswa kujitathmini iwapo anazo sifa za kuendelea kuwa mmoja wao.

Kauli hiyo aliitoa wakati akijibu swali la mwandishi wa habari hizi aliyehoji kama Mghwira bado anaendelea na masuala ya chama hicho au alishaamua kujiondoa kama alivyofanya Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Profesa Kitila Mkumbo, ili kutekeleza vyema utendaji wake serikalini.

“Mghwira na Profesa Kitila wote tunawaheshimu, Kitila aliandika barua na kurudisha kadi yetu. Mghwira ajitathmini, akiona anaweza aendelee, akishindwa basi tunamtakia heri,” alisema Yussuf.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles