28.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

BoT kutoa Muongozo mpya Kudhibiti Huduma ndogo za Kifedha

Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital

Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ipo mbioni kutoa miongozo na kanuni mpya kwa ajili ya kuratibu watoa huduma ndogo za kifedha daraja la pili ili kukabiliana na changamoto zilizopo, ikiwemo uvinjifu wa utu, sheria, na maadili katika utoaji wa mikopo.

Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba, alieleza hayo Juni 10, 2024, wakati akifungua mafunzo kwa watoa huduma ndogo za kifedha daraja la pili. Amesema lengo ni kuwajengea uwezo watoa huduma hao kwa kuwapa ujuzi, uwezo, na nafasi ya kubadilishana uzoefu.

“Tumepokea malalamiko mengi kuhusu vitendo vya ukiukwaji wa maadili na utu vinavyofanywa na baadhi ya watoa huduma ndogo za kifedha, hali inayoharibu biashara ya sekta ya fedha,” alisema Tutuba na kuongeza kuwa:

“Tunafahamu ipo mikopo ambayo imekuwa ikiumiza sana wakopaji, aidha kwa kutokueleweka au kwa ukosefu wa uelewa. Ili kumlinda mkopaji na mkopeshaji, tumejipanga kuja na miongozo itakayosaidia kulinda utu na maadili,”.

Gavana Tutuba aliongeza kuwa benki kuu imeamua kuja na miongozo na kanuni zitakazosaidia kurekebisha sekta ya fedha, hasa katika utoaji wa mikopo. Kanuni hizi zinatarajiwa kutoka Julai, 2024, na zitaainisha miongozo na taratibu za kufuatwa katika uendelezaji wa utoaji wa huduma ndogo za kifedha.

Tutuba alisema waendesha mikopo watatakiwa kuwasilisha kiwango cha riba kwa BoT kufuatilia na kuweka wazi mikataba yao kisheria, na kuhakikisha wanapata leseni. Wale ambao hawatakuwa na leseni watachukuliwa hatua za kisheria.

“Ili kuweza kufanikisha hili, Chuo cha Benki Kuu kimekuwa kikishirikiana na kurugenzi ya usimamizi wa sekta ya fedha kutoa mafunzo ya muda mfupi kwa watoa huduma ndogo za kifedha daraja la pili katika matawi yetu yote,” aliongeza Gavana Tutuba.

Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha Benki Kuu, Dk. Nicas Yabu, alisema licha ya mafunzo hayo, tayari wameshatoa elimu kwa watoa huduma zaidi ya 1,120 mwaka huu. Alisema mafunzo mafupi kwa watoa huduma ndogo za kifedha yanalenga kupunguza au kuondoa kabisa changamoto zilizopo.

Baadhi ya watoa huduma ndogo za kifedha walisema ni kweli kwamba baadhi yao wamekuwa wakikiuka sheria na taratibu, hivyo ni muhimu kupatiwa mafunzo hayo. Pia waliwataka wananchi kuheshimu na kupata elimu ya mikopo ili kuondoa lawama.

Walisema changamoto kubwa wanayokutana nayo ni uelewa mdogo kuhusu mikopo kwa wakopaji wao, hali inayosababisha kuchelewa kurudisha mikopo au kushindwa kulipa kabisa. Gabriel Omende, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mikopo ya Uwezo, alisema.

“Hii ni fursa kubwa kwetu kujifunza na kukumbushwa wajibu wetu katika kutoa huduma. Changamoto kubwa tunayokabiliana nayo ni riba, lakini BoT wameahidi kushughulikia suala hilo, pamoja na baadhi ya wateja ambao sio waaminifu,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles