Na Mwandishi wetu
Aplikesheni ya Boomplay inayotoa huduma ya kusikiliza na kupakua muziki, imesaini makubaliano ya kushirikiana kibiashara na Warner Music kwa lengo la kuongeza wigo wa upatikanaji wa kazi za muziki wa kampuni hiyo maeneo mengi zaidi duniani.
Katika makubaliano hayo Boomplay sasa itapata fursa ya kusambaza kazi za muziki zaidi ya 1,000,000 kutoka Warner Music kwenda kwa watumiaji wake nchini Tanzania na mataifa mengine tisa ya barani Afrika ikiwamo Cameroon, Ivory Coast, Ghana, Kenya, Nigeria, Rwanda, Senegal, Uganda na Zambia.
Mkurugenzi Mtendaji wa Boomplay, Joe He, amesema, makubaliano haya na makampuni makubwa ya muziki ya kimataifa kama Warner Music, yanatawawezesha kuyakaribia mafanikio ya malengo waliyojiwekea ya kujenga jukwaa kubwa la muziki linaloaminika na wengi barani Afrika.
“Tunataka kila mpenda muziki awe na uwezo wa kupata nyimbo na video, wakati wowote na mahali popote. Tunatarajia uwepo wa mafanikio bora kupitia ushirikiano huu na muendelezo mzuri wa kibiashara tukiwa na Warner Music hasa katika kipindi hiki kizuri kwenye fani ya muziki Afrika,” amesema.
Aidha, amesema ushirikiano huo pia utawawezesha wasanii wa Warner Music kujitangaza zaidi na kwa haraka mbele ya mamilioni ya watumiaji wa Boomplay na kuiwezesha app hiyo kuifikia dhamira yake ya kukusanya kazi za muziki kutoka sehemu mbalimbali za dunia na kuzileta barani Afrika.
Naye Meneja wa Boomplay Tanzania, Natasha Stambuli amesema; “tunatarajia mafanikio makubwa na fursa mbalimbali yakiwa ni matokeo ya makubaliano kama haya katika tasnia ya muziki nchini Tanzania. Huu ni mwanzo wa mambo makubwa zaidi hapo mbeleni kwa Boomplay pamoja na Warner Music.”