26.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

Bonnah anavyowajibika jimboni kutatua kero za wananchi

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Mbunge wa Jimbo la Segerea, Bonnah Kamoli ameendelea na ziara katika maeneo mbalimbali ya jimbo hilo ili kuzipatia ufumbuzi kero za wapigakura wake.

Amekuwa akifanya ziara katika mitaa na kata na kuzungumza na wananchi katika mikutano ya hadhara kwa lengo la kutatua kero zao.

Amesema pamoja na jitihada mbalimbali za kutekeleza miradi ya maendeleo kwenye jimbo hilo lakini bado linakabiliwa na changamoto za miundombinu ya barabara, maji na huduma nyingine za kijamii.

Mbunge wa Jimbo la Segerea, Bonnah Kamoli, akizungumza na wanafunzi wa Shule ya Msingi Magoza wakati alipokuwa akikagua miradi ya maendeleo. Kulia ni Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Simon Kawa.

“Kote ninakopita nimepokea kero nyingi lakini niwaahidi zote tunazifanyia kazi kwa kushirikiana na madiwani na wenyeviti, na ziara zangu zitakuwa endelevu mpaka tuhakikishe kero zote zinatatuliwa,” amesema Bonnah wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kata ya Kisukuru.

Juzi akiwa katika kata hiyo alitembelea Shule ya Msingi Magoza na kuahidi kuwa atashirikiana na Diwani wa kata hiyo, Lucy Lugome, kuhakikisha wanatatua changamoto zinazoikabili.

Baadhi ya madarasa ya shule hiyo ni chakavu huku pia ikiwa na upungufu wa matundu ya vyoo kwani yaliyopo ni 10 wakati mahitaji ni matundu 46.

Aidha mbunge huyo ameelezwa na Mtendaji wa Kata hiyo kuwa ujenzi wa kituo cha polisi kinachogharimu Sh milioni 70 umefikia asilimia 75 na kwamba tayari wamepokea Sh milioni 40 kutoka Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam.

Amesema pia barabara ya Maji chumvi – Segerea – Migombani – Mkuwa zitajengwa kwa kiwango cha lami kupitia mradi wa DMDP na wakati wanasubiri mradi huo atashirikiana na diwani kuweka vifusi katika barabara hizo na zingine katika mitaa yote ziweze kupitika.

Mbunge wa Jimbo la Segerea, Bonnah Kamoli, akitoka kukagua Kituo cha Polisi kinachojengwa katika Kata ya Kisukuru. (Wapili Kulia) ni Diwani wa Kata hiyo, Lucy Lugome.

Kuhusu ujenzi wa zahanati amesema fedha zilishatengwa lakini kiwanja kilichotengwa kwa ajili ya ujenzi huo kiliuzwa. Hata hivyo ameahidi kushirikiana na diwani kuhakikisha eneo linapatikana zahanati iweze kujengwa.

Kwa upande wake Diwani Lucy amemshukuru mbunge huyo kwa jitihada anazofanya kusikiliza na kutatua kero za wananchi pamoja na kuwapatia Sh milioni 10 kupitia mfuko wa jimbo ambazo zitatumika kutengeneza kivuko cha Efatha.

Nao baadhi ya wananchi wa jimbo hilo wamesema Bonnah ni kiongozi mwenye utashi na uwezo wa kusimamia ilani na kwamba ana dhamira ya dhati ya kutatua changamoto zao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles