25.5 C
Dar es Salaam
Saturday, May 18, 2024

Contact us: [email protected]

Bodi ya Mfuko wa Barabara yatakiwa kufanyia kazi malalamiko ya watumiaji

Na Sheila Katikula, Mwanza

Bodi ya Mfuko wa Barabara imetakiwa kufanyia kazi malalamiko ya watumiaji wa barabara kwa wakati nakwamba kufanya hivyo kutapunguza ajali za mara kwa mara.

Hayo yamebainishwa Julai 25, 2022 jijini Mwanza na Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya kwenye warsha ya kujadili namna ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kwenye miundo mbinu ya barabara na uzinduzi wa mfumo wa kieletroniki na ufatiliaji wa hali ya barabara nchini.

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya.

Amesema hatua stahiki zitachukuliwa kwa wahusika ambao hawatazifanyia kazi kwa wakati taarifa hizo.

“Ni muhimu sasa kuhakikisha tunatenga fedha kila mwaka ili kugharamia shughuli za utafiti ambao utajikita zaidi katika kuleta teknolojia ya ujenzi, matengenezo ya barabara ambayo itahimili athari za mabadiliko ya tabianchi, utafiti huo pia ulenge katika kuongeza matumizi ya malighafi inayopatikana hapa nchini, hususan kwenye maeneo ya mradi kama vile mawe na vifusi na changarawe,” amesema Mhandusi Kasekenya.

Ameongeza kuwa Serikali itaendelea kuongeza vyanzo vya mapato ya mfuko wa bodi ya barabara pamoja na Halmashauri zimetakiwa kutenga fedha kila mwaka kwa ajili ya kugharamia matengenezo ya barabara kwenye maeneo yao.

“Serikali imewekeza fedha nyingi kwenye miundombinu ya barabara inakabiliwa na hatari kubwa ya kuharibika kutokana na madhara ya mabadiliko ya tabianchi ambapo takribani Sh bilioni 209.7 zilitumika kufanya matengenezo ya dharura kati ya mwaka 2015 na 2020.

“Kwa kutambua athari za mabadiliko ya tabianchi, serikali iliandaa Mkakati wa Kitaifa wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kuanzia 2021 hadi 2026 ambao malengo yake ni pamoja na kujumuisha masuala ya mabadiliko ya tabianchi kwenye mipango na bajeti za kisekta na kuwezesha upatikanaji endelevu wa fedha na teknolojia ili kukabiliana na madhara hayo,” amesema Mhandisi Kasekenya.

Aidha, amewataka Wakala wa Barabara kufanya ukaguzi wa mara kwa mara kwenye madaraja na makaravati ili kuepuka kutokea kwa majanga.

Kwa upande wake Meneja wa Mfuko wa Barabara, Eliud Nyauhenga amesema pamoja na ufuatiliaji wa kila siku, mwaka bodi hufanya tathmini ya utendaji wa Wakala wa barabara kupitia wataalam elekezi kwa kutumia mfumo wa kutathmini kazi za barabara kwa kuzingatia thamani ya fedha.

Pia ameongeza kuwa vigezo vinavyotumika kufanya tathmini ya utendaji ni umakini katika maandalizi ya mradi, usanifu wa mradi, taratibu za manunuzi, ujenzi, matengenezo ya mradi na kufunga mradi.

Aidha, amesema kuwa mikoa na wilaya ambazo zimekuwa na utendaji usioridhisha zitatambulishwa kwa lengo la kuwahimiza kufanya kazi kwa ushirikiano, weledi na kufuata sheria na taratibu za nchi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles