Na Ramadhan Hassan, Dodoma
Bodi ya Korosho Tanzania (CBT), imesema itaendelea kutatua changamoto zote zinazolikabili zao la korosho ikiwemo kutafuta masoko ya uhakika.
Hayo yameelezwa leo Jumamosi Oktoba 8,2022 na Kaimu Mkurugenzi wa CBT, Francis Alfred alipokuwa akielezea utekelezaji wa shughuli za bodi hiyo na mwelekeo wa utekezaji kwa mwaka 2022/2023.
Amesema viwanda vya ubanguaji wa korosho viko 52 lakini vinavyofanya shughuli ya ubanguaji kwasababu ya uwepo wa mitambo ni 30.
Amesema viwanda hivyo vinauwezo wa kubangua tani 64, 500 lakini mwaka jana viliweza kubangua korosho tani 8,959.
Amesema viwanda vyote vilivyopo nchini vikiwekewa mitambo ya ubanguaji vinaweza kubangua korosho zaidi ya tani 185,000 kwa mwaka.
Alfred amesema viwanda hivyo vimeshindwa kubangua korosho kutokana na uwezo wake kwasababu mbalimbali ikiwemo upatikanaji wa malighafi zinazosheleza mwaka mzima.
“Changamoto nyingine ni upatikanaji wa mitaji ya bei nafuu na nyingine kukidhi ubora wa chakula ili kuweza kuuza vizuri kwenye masoko makubwa duniani wakiwemo Marekani na bara la Ulaya ikiwemo Ujerumani,”amesema.