NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
BARAZA la Michezo la Taifa (BMT), limeviagiza vyama na mashirikisho ya michezo ambayo hayajafanya uchaguzi kufanya hivyo ili kupata viongozi kulingana na katiba zao na waziagize klabu zao kufanya uchaguzi ili waongoze kwa demokrasia na kwa kufuata katiba.
Kwa mujibu wa taarifa ya Kaimu Katibu Mkuu wa BMT, Mohamed Kiganja, iliyotolewa Dar es Salaam jana, baraza hilo limetoa siku kumi na nne (14) kuanzia jana ili kila chama, shirikisho na klabu kutekeleza maelekezo hayo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, utekelezaji unapaswa uwasilishwe BMT haraka iwezekanavyo.
Agizo hilo ni kwa mujibu wa sheria ya Baraza la Michezo la Taifa (BMT) Na. 12 ya 1967 na marekebisho yake ya 1971 iliyotoa jukumu kwa BMT kusimamia chaguzi za vyama/mashirikisho nchini.