Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken anakutana leo na viongozi wa Ukraine, kuonyesha mshikamano wa nchi yake baada ya hatua ya Urusi kuyarundisha majeshi yake karibu na mpaka baina yake na Ukraine.
Katika ziara hiyo ya siku moja, Blinken pia anatarajiwa kuwahimiza viongozi wa Ukraine kufanya juhudi zaidi kupambana na ufisadi.
Mwezi uliopita, Urusi iliwapeleka wanajesha wapatao 100,000 katika mpaka wake na Ukraine, hiyo ikiwa hatua kubwa zaidi ya kijeshi kuchukuliwa na Urusi tangu ilipoitwaa kimabavu rasi ya Crimea kutoka Ukraine mwaka 2014.
Katika mkutano wa mataifa saba ya kidemokrasia yanayoongoza kiuchumi, maarufu kama G7 ambao umemalizika mjini London, wajumbe wake walirejelea miito ya kutaka uhuru wa Ukraine uheshimiwe, katika eneo lote ndani ya mipaka yake ya nchi kavu na baharini inayotambuliwa kimataifa.