RATIFA BARANYIKWA Na MASHIRIKA YA KIMATAIFA
KAMA ilivyo kwa Tanzania ambayo inajiandaa na Uchaguzi Mkuu utakaofanyika baadae mwaka huu, Marekani nayo ipo kwenye mchakato huo huo.
Tambwe za wanasiasa kama Tundu Lissu, Benard Membe na wengine dhidi ya Rais Magufuli anayewania kipindi cha pili cha urais, zipo pia Marekani ambako nako wanasiasa kila kukicha wanazidi kutafuta mbinu na mikakati ya kuraruana majukwaani ili kushinda mioyo ya wapiga kura.
Wiki hii imemalizika kwa tukio kubwa la mgombea urais wa chama cha Democrat, ambaye ni makamu wa Rais wa zamani wa Marekani, Joe Biden kumteua Seneta wa California, Kamala Harris kuwa mgombea mwenza wake.
Suala si tu Biden kumteua mgombea mwenza, bali kumteua mtu mwenye asili ya weusi na mwanamama mwenye misimamo na mpiganaji ambaye alipata kumpinga wakati fulani hata yeye mwenyewe waziwazi.
Wapo wanaona uteuzi huo wa Biden kwa seneta huyo mweusi umebeba sura ya harakati za watu weusi hasa kupitia ule msemo; ‘Black lives matters’ ambazo zilitikisa taifa hilo kwa maandamano makubwa hivi karibuni baada ya kifo cha Mmarekani mweusi, Floyd George aliyeuawa kwa kukandamizwa shingoni na polisi wa kizungu wa nchi hiyo.
Vyombo vya habari vya Marekani, vikiripoti uteuzi huo siku ya Jumanne wiki hii viliandika; Biden ameandika historia kwa kumteua Seneta Harris akiwa mweusi wa kwanza aliyechanganyika na mu-Asia kwenye nafasi hiyo.
Biden amemtangaza mgombea mwenza wake huku wiki ijayo ukitarajiwa kuitishwa mkutano mkuu wa chama cha Democrat.
Uamuzi huo ambao ulikuwa ukisubiriwa kwa muda mrefu, Biden aliutangaza kupitia mtandao wa Twitter akimtaja Harris kama; “ Mpiganaji asiyeogopa, kijana na mmoja wa watumishi bora wa umma wa nchi hiyo.
Timu ya kampeni ya Biden, inasema wawili hao watahutubia kwa pamoja Jumatano huko Wilmington, Del., na baada ya hapo watahudhuria harambee.
Ujumbe wake wa Twitter ulisomeka hivi;
Ninayo heshima kubwa kutangaza kwamba nimemchagua @KamalaHarris – mpiganaji asiyeogopa, kijana mdogo na mmoja wa wafanyakazi wa umma wa serikali – kama mgombea mwenza wangu.
Biden anamtaja Harris kama kijana, na taarifa zinaonyesha ana miaka 55, na yeye ana miaka 77 wakati mpinzani wake wa Republican, ambaye anawania kipindi cha pili cha urais wa Marekani, Donald Trump akiwa na miaka 74 na makamu wake wa rais, Mike Pence miaka 61.
Harris naye alitumia ukurasa huo huo wa twitter kuelezea jinsi alivyopokea kwa heshima uteuzi huo wa Biden, akisema kuwa ni mtu ambaye anaweza kuwaunganisha Wamarekani pamoja kwa sababu ametumia maisha yake kuwapigania.
“Na kama rais, ataiwezesha Marekani kutimiza malengo yetu”
Harris ambaye alipata kuwa Mwanasheria Mkuu wa California na mwanamke pekee mweusi kwenye baraza la Seneti la Marekani, amepata kupambana na Biden katika kinyanganyiro cha urais ndani ya chama hicho mwaka jana.
Lakini sasa amepasua na kuingia kwenye orodha ya makamu wa rais na kusisitiza umuhimu wa uzoefu.
Ni wanawake wawili tu ambao wamepata kuteuliwa kuwa wagombea mwenza nchini Marekani, Geraldine Ferraro wa chama cha Democrat mwaka 1984 na Sarah Palin wa chama cha Republican mwaka 2008, na hakuna aliyepata kushinda.
“Kiti hicho kilihitaji mwanamke mweusi, Biden alihitaji mpambanaji,” alisema LaTosha Brown, ambaye ni mmoja wa waanzilishi wa vuguvugu la ‘Black Voters Matter’
Wiki kadhaa kabla ya Biden hajatangaza chaguo lake, Harris alibeba vichwa vya habari mbaya ikiwamo ripoti zilizochapishwa na CNBC zilizosema; baadhi ya washirika wa Biden walikuwa wameiambia kamati yake ya kumtafuta mgombea mwenza “alikuwa “too ambitious.”
Wanawake wakiwamo wale walioko ndani ya timu ya kampeni ya Biden walikusanya taarifa hizo kama ushahidi wa ubaguzi wa kijinsia kwenye siasa.
“Kauli yangu katika hili: Namshukuru Mungu alikuwa ambitious,” alisema Brown
Harris amewashinda wengi katia listi aliyokuwa nayo Biden ya wagombea mwenza, wakiwamo Seneta Elizabeth Warren, mmoja wa maofisa katika utawala wa Rais Barrack Obama, Susan Rice, Mwakilishi wa California, Karen Bass,na Gavana wa Michigan Gretchen Whitmer.
Biden, ambaye anajua kazi hiyo akiwa amewahi kuwa makamu wa Rais wa Barack Obama, alisisitiza kwamba anataka mgombea mwenza anayehisi ana endana naye na mtu ambaye alikuwa tayari kuchukua urais ikiwa ni lazima.
Mtoto wa wahamiaji wa Kihindi na Jamaica, Harris anavunja kizuizi wakati wapiga kura wengi wanataka mabadiliko na usawa kwa watu weusi hasa katika wakati huu ambao kuna maandamano mengi ya haki za raia kote nchini Marekani. Anaweza kuwa mwanamke wa kwanza, mweusi, au mu-asia kuwa makamu wa rais iwapo atachaguliwa.
Inasemekana chaguo lake lina msukumo wa wanaharakati wa Democratic likichagizwa pia na rekodi zake za uaminifu ndani ya chama.
Rekodi yake katika utekelezaji wa sheria – iliyoundwa wakati wa nyakati ngumu za uhalifu miaka ya 1990 – inaweza kuwa dhima kwake na miongoni mwa Wanademocrat ambao wanashinikiza mageuzi ya haki ya jinai hasa baada ya mauaji ya George Floyd.
Harris mwenyewe alikuwa ni miongoni mwa walioandamana Washington iliko Ikulu ya Trump kupinga ukatili uliofanywa dhidi ya Floyd.
Wanademocrat wa mlengo wote wameshangilia uteuzi wake, wanamsifu Harris kwa utaalam wake na kujitolea kwa jamii ya watu weusi na kuuita uamuzi wa Biden kuwa chaguo la ujasiri na la kihistoria ambalo limefikia wakati sahihi kisiasa.
Harris ni mmoja wa watu walionyesha haraka kupingana na sera za Rais Trump dhidi ya wahamiaji.
“Kama binti wa wahamiaji, hadithi ya Seneta Harris inakua kama ukumbusho wenye nguvu kwamba kupitia michango yao, wahamiaji wanaifanya Marekani kuwa na nguvu,” Marielena Hincapié, ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa National Immigration Law Center Immigrant Justice Fund, alisema kupitia taarifa yake mara tu baada ya uteuzi wa Harris.
Rashad Robinson, ambaye ni rais wa Color Of Change PAC, aliwaambia waandishi wa habari kwamba taasisi yake ipo tayari kushirikiana na Harris, ambaye amemuelezea kama mtu aliyekuwa tayari kuzungumza na wanaharakati, hata wakati walipokuwa wanakabiliwa na mrejesho mbaya.
Lakini alionya kuwa alama ya wawili hao Biden na Harris haitoshi pekee kuwashawishi wapigakura weusi, kwamba wasitarajie msaada usiokuwa na usawa.
Alisema Harris atatakiwa kuzungumzia juu ya rekodi yake juu ya haki ya jinai, changamoto ambazo amekuwa nazo na azungumze kuhusu mahali alipo sasa.
Adrianne Shropshire, ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa BlackPAC, amesema wakati huo wa kihistoria wa wanawake weusi umewadia kabla ya kumbukizi ya Sheria ya Haki za Kupiga Kura, ambayo ilizuia ubaguzi wa rangi katika uchaguzi, na Marekebisho ya 19, ambayo yatoa nafasi kwa wanawake haki ya kupiga kura.
Alimtaja Harris kama “bingwa wa haki asiyeogopa.”
“Anaelewa mazingira haraka na atafanya kazi ili kurejesha uwezo, uongozi na maadili kwa Marekani,” Shropshire anasema..
Tangu alipojiunga na Seneti mwaka 2017, Harris alijipa jina yeye mwenyewe la kushoto akiwagalagaza maofisa wa serikali ya Trump kwenye kamati na sasa kwenye kinyang’anyiro cha urais.
Si tu utawala wa Trump, huko nyuma alipata kumshushia lawama kali Biden akimshambulia kwa msimamo wake kuhusu usafiri wa wanafunzi mashuleni.
Baada pia ya michakato ya kisiasa, Harris alirejesha uhusiano wake na Biden, na hata kumuunga mkono kwenye kinyang’anyiro cha kuwania urais.
Watu wanaofuatilia siasa za Marekani wanahusisha uteuzi wa Harris na uhusiano binafsi kutokana na kwamba alipata kuwa rafiki wa mtoto wa kiume wa Biden, marehemu Beau, amaye alikuwa Mwanasheria Mkuu wa Delaware wakati yeye akishikilia nafasi kama hiyo California.
Chaguo lake unaweza kuwa mwanzo mwingine wa kuzidi kustawi au kupanda wa Harris ndani ya chama cha Democrat katika mika ijayo.
Biden ambaye ana miaka 77 atakuwa Rais mwenye umri mkubwa zaidi katika historia ya Marekani na iwapo atachaguliwa na kuna shaka kama ataweza kuhudumu hata kipindi cha pili jambo ambalo wachambuzi wanaona kuwa linamfanya Harris huko mbele apande na hata kuwania urais iwapo watashinda katika uchaguzi wa mwaka huu.
Kitendo cha Biden kumteua Harris mara moja walionekana kuongoza kwenye kura za maoni dhidi ya Trump, ambaye ameonekana kupigwa mfululizo kwenye kura hizo za maoni kutokana na jinsi alivyoshughulikia suala la virusi vya corona na mahusiano ya.
Siku Biden alivyomtangaza Harris, Trump aliwaambia waandishi wa habari kwamba ameshangazwa na uteuzi huo, hata kama amekuwa akionekana kusimama mstari wa mbele, lakini amefurahia chaguo kwa sababu anamuona mwepesi kwenye mashambulizi.
Alimshutumu Harris kw akutaka kuongeza kodi, kufyeka fedha za wanajeshi, na mtu aliyeonyesha ubaya kwa Biden wakati wa chaguzi za ndani ya chama chao.
Trump ametaka kuchochea wasiwasi miongoni mwa wapiga kura weupe kuhusu maandamano ya hivi karibuni ya haki ya kibaguzi na maandamano – akimtaja Biden kuwa mtu mwenye misimamo mikali ambaye anataka kurudisha nchi nyuma.
Lakini wakati huo huo, timu ya kampeni ya Trump imeendesha matangazo yanayolenga wapiga kura Weusi kuwakumbusha jukumu alilotekeleza Biden katika kupitisha muswada wa uhalifu mwaka 1994 ambao ulichangia kuongezeka kwa idadi ya wafungwa.
Wachambuzi pia wanasema timu ya kampeni ya Trump au washirika wake wanaweza kukusanya rekodi za nyuma za Harris akiwa kama Mwanasheria Mkuu zikiwa na nia ya kusambaratisha kura za watu weusi.
Pamoja na hayo Harris bado hajulikani kwa wapiga kura wengi kama ilivyo kwa Biden au Trump, huku kura ya maoni iliyoendeshwa ikionyesha kuwa asilimia 20 ya wapigakura hawajawahi kumsikia.
Kati ya wagombea mwenza ambao Biden alikuwa akiwafikiria hata hivyo Harris alikuwa ni wa pili kujulikana baada ya Warren.
Wanaharakati na wanamikakati wa kisiasa wa Democratic wanasema walikuwa tayari wamejiandaa kupambana na mashambulizi yeyote dhidi ya Harris au juhudi zozote za kusambaratisha kura za watu weusi.
Mike Madrid, mwanamikakati wa muda mrefu wa Republican na mmoja wa waanzilishi wa mradi wa ‘The Lincoln’, kamati ya kisisa inayopambana dhidi ya Trump, amemtaja Harris kama chaguo sahihi kwa tiketi ya Democrat na mtu ambaye amefanikiwa kufanya mashambulizi kwenye ngazi ya taifa kwa zaidi ya mwaka mmoja.