RAMADHANI HASSAN -DODOMA
WAZIRI wa Madini, Doto Biteko, amewasilisha bajeti ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2020/21, huku akisema kuanzishwa kwa masoko ya madini nchini kumewezesha kufanyika biashara ya zaidi ya Sh trilioni moja kwa mwaka.
Akisoma bajeti hiyo bungeni jana ambayo ilipitishwa na wabunge, Biteko alisema masoko hayo yamesaidia kutatua changamoto za muda mrefu ambazo zilikuwa zikiikabili sekta hiyo, hususan wachimbaji wadogo kukosa masoko ya uhakika na bei stahiki.
Alisema katika kipindi cha kuanzia Machi 2019 hadi Februari 2020 kupitia masoko hayo, wachimbaji wadogo wamefanya biashara yenye thamani ya Sh 1,088,693,000,153.19.
Biteko alisema katika fedha hizo, Serikali imepata mrabaha na ada ya ukaguzi wa Sh 78,008,413,233.13.
“Masoko haya yameleta mabadiliko makubwa katika sekta ya madini ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa kasi ya ukuaji wa sekta hii kwa kipindi cha Januari hadi Septemba iliongezeka kutoka asilimia 0.9 mwaka 2018 hadi asilimia 12.6 mwaka 2019 kwa kipindi kama hicho,” alisema Biteko.
Alisema uanzishwaji wa masoko ya madini ni maono ya Rais Dk. John Magufuli kuhakikisha anawapatia wachimbaji wadogo soko la uhakika.
“Masoko hayo yameleta manufaa mengine kwa wananchi, ikiwemo kuzalisha fursa za ajira na kuongezeka kwa kipato cha wachimbaji wadogo tofauti na hapo awali.
“Namuomba Mungu azidi kumjalia maono zaidi na zaidi ili Watanzania wazidi kuneemeka,” alisema Biteko.
Alisema katika kipindi cha Januari hadi Septemba, 2019 kasi ya ukuaji wa sekta ya madini ulifikia asilimia 12.6.
“Ukuaji huu uliifanya sekta ya madini kushika nafasi ya pili ikitanguliwa na sekta ya ujenzi iliyokua kwa asilimia 14.8.
“Ukuaji huu ulitokana na kuongezeka kwa uzalishaji wa madini mbalimbali yakiwamo dhahabu, makaa ya mawe, Tanzanite na almasi,” alisema Biteko.
Alisema hadi Februari, 2020 nasoko ya madini 28, na vituo vya ununuzi wa madini 28 vimeanzishwa na kuwezesha kutatua changamoto zilizokuwa zinaikabili sekta hiyo.
WAVUNJA REKODI
Biteko alisema wizara hiyo ilipangiwa kukusanya Sh 476,380,613,492, kati yake Sh 470,897,011,000 zilipangwa kukusanywa na kuwasilishwa hazina ambapo hadi Machi, 2020 Sh 358,870,785,797 zimekusanywa na kuwasilishwa.
Alisema makusanyo hayo ni asilimia 102 ya lengo la Sh 353,172,758,250 katika kipindi husika.
MACHIMBO YA TANZANITE MIRERANI
Biteko alisema kutokana na uwekezaji uliofanyika kwenye machimbo ya Tanzanite Mirerani, kumekuwa na ongezeko kwa mapato yatokanayo na madini hayo.
Alisema mapato yameongezeka kutoka Sh 166,094,043 kabla ya kujenga ukuta hadi Sh 2,150,000,000 baada ya kujengwa kwa ukuta.
MADINI KUKAMATWA
Biteko alisema pia katika kudhibiti utoroshwaji wa madini nchini, walikamata madini ya Dola za Marekani 3,210,976.35 na Sh 1,556,209,334.61.
Alisema madini hayo yalikamatwa Tunduru, Kyerwa, Mwanza, Mirerani, Holili, Babati, Hai, Dodoma, Nzega na Kahama.
“Nitoe wito kwa wafanyabiashara na wadau wa sekta ya madini kwa ujumla kufanya shughuli zao kwa kuzingatia sheria, kanuni, miongozo na taratibu zinazosimamia sekta ya madini,” alisema Biteko.
STAMIGOLD
Katika hatua nyingine, alisema Kampuni ya Stamigold ambayo ni kampuni tanzu ya Stamico kwa kipindi cha Julai, 2019 hadi Februari, 2020 imeweza kuzalisha na kuuza wakia 9107.45 za madini ya dhahabu na wakia 1,170.21 za madini ya fedha, vyote vikiwa na thamani ya Sh 31,539,991,237.11.
“Mgodi umelipa Sh 2,303,564,360.31 kwa ajili ya malipo ya mrabaha, ada ya ukaguzi na ushuru wa huduma.
“Aidha, mgodi umeanza kuuza dhahabu inayozalisha kwenye masoko ya ndani ya madini.
“Hatua hii imeokoa gharama ya usafirishaji kiasi cha Sh milioni 131.8 kama dhahabu ingeuzwa nje ya nchi,” alisema Biteko.
UTARATIBU MPYA UNUNUZI DHAHABU
Akihitimisha mjadala wa hotuba yake ya bajeti, Biteko alisema kwa sasa wanunuzi wa dhahabu wanaruhusiwa kununua katika maeneo mbalimbali tofauti na utaratibu wa kununua katika kanda husika.
Alisema zamani kulikuwa na utaratibu ukitaka kununua dhahabu ni lazima ununue katika kanda unayotoka.
Biteko alisema anapenda kulitangazia Bunge kwamba utaratibu huo ameuvunja na sasa wanunuzi wa dhahabu wataruhusiwa kununua mahali popote.
“Naomba nitoe tangazo kwa wanunuzi, sasa utaratibu wa kununua kwa kanda tunauvuka na sasa unaweza kununua popote bila kujali mpaka wake,” alisema Biteko.
Alimpongeza Rais Magufuli kwa kuweza kutoa mwongozo wa kusimamia vyema sekta ya madini.
”Msimamizi mkuu wa sekta ya madini ni Rais kwa sababu amekuwa akitoa mwongozo katika sekta hiyo, tunamshukuru sana.
”Niwahakikishieni wabunge, hakuna mchango hata mmoja ambao tutaupuuza. Mimi huwa ninaamini hata saa mbovu huwa kuna muda inasema ukweli,” alisema Biteko.
Kuhusu hoja ya wachimbaji kukosa umeme, alisema jambo hilo alilimaliza kwa kusimamia maeneo 27 ya wachimbaji kupata umeme.
”Tulipeleka maeneo 27 ya maombi ya umeme. Maeneo yote ambayo tuliyaombea yote yamepatiwa na wale ambao wanahitaji kwa sasa walete maombi. Nataka niwahakikishie Serikali inafanya kazi vizuri,” alisema Biteko.
Kuhusu Shirika la Madini (Stamico) kuanza kununua madini, Biteko alisema kazi hiyo wataianza hivi karibuni na wameipa leseni mbili.
”Stamico tayari imeomba leseni mbili za kununua dhahabu, tunataka sasa waingie katika biashara, Stamico walikuwa na tatizo la kimuundo, sasa hivi hatutengenezi hasara, tumezalisha kwa sasa zaidi ya bilioni 30,” alisema Biteko.
Alisema kama mchimbaji mdogo analipa ushuru ni kwanini Stamico washidwe kulipa kodi.
”Nilikuwa najiuliza kama mchangiaji mdogo analipa kodi iweje Stamico yenyewe eti tena ipewe fedha kwa ajili ya kujiendesha. Na leo ninavyozungumza hakuna hasara inayotengenezwa na Stamico. Muundo wa shirika tumeisharekebisha,” alisema Biteko.