Na ASHA BANI-DAR ES SALAAM
Ubalozi wa Ghana kupitia balozi wake wa heshima hapa nchini, umepokea shairi kutoka kwa binti wa Kitanzania, Aisha Kingu, likimuenzi Katibu Mkuu mstaafu wa Umoja wa Mataifa (UN) marehemu Koffi Annan.
Shairi hilo lilipokelewa jana jijini Dar es Salaam na Msaidizi wa Balozi wa heshima wa Ghana, Bakari Jumanne, kwa niaba ya balozi wa nchi hiyo hapa nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Aisha, alisema ameamua kuandika shairi hilo likielezea wasifu wa aliyekua katibu mkuu mstaafu marehemu Koffi Annan, kama njia moja ya kumuenzi kwa kazi kubwa aliyoifanya katika kuutumikia umoja wa taifa na dunia kwa ujumla na kwa heshima aliyoipa Afrika kuwa Katibu mkuu wa kwanza mweusi Afrika.
“Nilipokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kifo cha katibu huyo mstaafu ambaye nilikua nikimfuatilia utendaji wake wa kazi, ikanipelekea kama mwana mashairi kumwandikia shairi hilo,” alisema Kingu.
Binti huyo mwenye Shahada ya Sheria na mmoja wa wanachama wa CPTM (Common Wealth Partnership for Technology), alisema ana thamini mchango wa marehemu Koffi Annan wakati wa uhai wake hasa katika kusaidia matatizo yanayoikabili nchi za Afrika likiwemo tatizo la elimu kama alivyoandika katika shairi lake akisema:
“Mwanadiplomasia wa Afrika, Kiongozi uliyetukuka, Msimamizi wa amani, Mwanaharakati wa demokrasia, Afrika itatukuza matendo yako, kwa kuwa ulipiga hatua kwa ujasiri, utulivu na uwazi,” alisema.
Binti huyo mwenye ndoto ya kuja kuwa mmoja wa watumishi Umoja wa Mataifa, ameongeza kwa kusema marehemu Koffi Annan ni mfano wa kuigwa na yeye kama kijana amewaasa vijana wenzake kuyaishi yale mema aliyofanya Koffi Annan pamoja na kuenzi kazi alizozifanya.
Akizungumza mara baada ya kupokea shairi hilo, Msaidizi wa balozi wa heshima, alisema atahakikisha shairi hilo linafika ubalozi wa Ghana uliopo Kenya kwa ajili ya kusafirishwa kuelekea Ghana.
“Kwa niaba ya balozi wa heshima wa Ghana nchini Tanzania Mheshimiwa Ken Kwaku, napokea shairi hili kutoka kwa Aisha Kingu na ningependa kutoa shukrani za dhati kwako kwa kumuenzi marehemu Koffi Annan kwa shairi hili zuri, Mungu akubariki uweze kufanikiwa katika harakati za kutimiza malengo na ndoto ulizonazo. Endelea kukuza kipaji chako wewe tayari ni nyota inayong’aa ikiwakilisha taifa la Tanzania,” alisema.