Na JANETH MUSHI
-ARUSHA
SERIKALI inatarajia kutumia zaidi ya Sh bilioni 87 kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya kiwango cha lami katika Wilaya ya Ngorongoro.
Kauli hiyo ilitolewa mwishoni mwa wiki na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo, wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake kuhusu masuala mbalimbali ya maendeleo katika mkoa huo.
Alisema Ngorongoro ni wilaya pekee mkoani hapa ambayo haina barabara ya lami.
Mkuu huyo alisema kuwa barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 49, itaanzia eneo la Waso hadi Sale.
Gambo alisema ujenzi huo unatarajiwa kuanza mwaka huu ambapo mkandarasi ameshapatikana na anakamilisha hatua za mwisho ili aanze ujenzi huo, ambao unagharamiwa na Serikali kuu.
“Tangu tumepata uhuru, Ngorongoro haijawahi kuwa hata na kilomita moja ya lami, hili ni jambo la kihistoria katika wilaya hiyo tunamshukuru Rais, Dk.John Magufuli na serikali yake kwa ujumla kwa kuwezesha ujenzi wa barabara hiyo,”alisema.
Akizungumzia msongamano wa magari, alisema Serikali ina mpango wa kuboresha barabara za ndani zitakazosaidia kupunguza foleni katikati ya jiji ikiwamo barabara ya Unga Limited kuelekea dampo ambayo ina urefu wa kilomita 5.9 inayojengwa kwa kiwango cha lami ambayo itagharimu zaidi ya Sh bilioni 17.9.
Kuhusu changamoto ya maji, kiongozi huyo alisema Serikali imetenga zaidi ya Sh bilioni 476 kwa ajili ya kukabiliana na tatizo la maji katika jiji la Arusha na maeneo ya jirani, ambapo fedha hizo zitatekeleza miradi ya maji safi pamoja na maji taka.
Alisema mradi huo ukianza mwaka huu baada ya miaka miwili tatizo la maji katika jiji hilo litaisha.