|Susan Uhinga, Tanga
Serikali imeahidi kulipatia jiji la Tanga Sh bilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya kwa ili kusogeza huduma zaidi kwa wananchi na kupunguza msongamano wa wagonjwa wanaopelekwa katika hospitali ya Rufaa ya Bombo.
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Joseph Kakunda amesema hayo leo Jumanne Agosti 14, wakati alipotembelea vituo hivyo ili kujionea ujenzi unavyoendelea wa hospitali hiyo unavyoendelea.
Amesema serikali baada ya kutenga fedha kwa vituo vya afya 108 nchini kote sasa inatoa fedha katika kujenga hospitali za wilaya katika mikoa ambayo haina hospitali za wilaya.
“Katika mwaka wa fedha ulioishia Juni mwaka jana Jiji la Tanga ilipata kiasi cha Sh bilioni 1.4 kwa ajili ya kupanua na kuvijengea uwezo Vituo vya Afya vya Ngamiani na Makorora ambapo vilipewa Sh milioni 500 kila kituo na kituo cha Mikanjuni nacho kilipewa Sh milioni 400.
“Katika vituo hivyo tayari vituo 85 tayari vimekamilika hapa nchini huku vituo 23 bado havijakamilika na kwamba serikali itatoa fedha kwa ajili ya kujenga hospitali za majiji zipatazo 67 nchini ikiwamo jiji la Tanga,” amesema.
Aidha, alilitaka jiji la Tanga litakapopewa fedha hizo kuhakikisha wanajenga hospitali ya kisasa zaidi itakayoendana na hadhi ya Jiji hilo.
Kwa upande wake Meya wa Jiji la Tanga, Mhina Mustafa aliishukuru serikali kwa kuwapatia fedha za kupanua vituo hivyo na kuahidi hadi ifikapo Septemba 30 mwaka huu vituo hivyo vitakuwa vimekamilika.