26.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 23, 2024

Contact us: [email protected]

Bil. 17.9 kusambaza umeme vitongoji 166 Morogoro

Na Mwandishi Wetu, Morogoro

Jumla ya vitongoji 166 mkoani Morogoro vinatarajiwa kupata umeme baada ya Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kumtambulisha Mkandarasi aliyeshinda zabuni ya kupeleka umeme katika vitongoji hivyo ili aanze kazi.

Mradi huo wenye gharama ya shilingi bilioni 17.9 unatarajiwa kutekelezwa katika kipindi cha miezi 24 na utakapokamilika utanufaisha zaidi ya Kaya 5,478.

Akizungumza wakati wa hafla fupi ya kumtambulisha Mkandarasi huyo ambaye ni kampuni ya SINOTEC CO. LTD, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha hizo pamoja na kuwapongeza REA kwa kusimamia vyema maono ya Rais kuhakikisha wananchi vijijini nao wanapata maendeleo kupitia upatikanaji wa nishati ya umeme.

“Mkoa wa Morogoro ni mkoa wa kimkakati, Mkoa wa uzalishaji na tumejipanga kuwa Mkoa namba moja katika kilimo nchini. Na kuwepo kwa umeme maeneo ya vijijini kutasaidia kuongeza thamani ya mazao ya kilimo. Umeme ndio nguzo namba moja katika kuongeza thamani mazao ya kilimo. Tuendelee kumpongeza na kumshkuru Mhe. Rais kwa kutoa fedha zinazoenda kuwezesha zaidi ya Vitongoji 166 vinapata umeme,” amesema Malima.

Amewasisitiza wananchi kutunza miundombinu ya umeme na kumtaka pia mkandarasi huyo kuhakikisha anatekeleza mradi huo ndani ya muda uliopangwa na kwa viwango vya ubora.

Awali akitoa taarifa ya upelekaji wa umeme Vijijini, Mhandisi Msimamizi wa Miradi ya REA Kanda ya Kati, Aneth Malingumu amesema kuwa kati ya vijiji 669 katika Mkoa wa Morogoro, vijiji 652 ambavyo ni sawa na asilimia 97.5 vimefikiwa na nishati ya umeme na kuongeza kuwa vijiji 17 vilivyobaki viko kwenye hatua za mwisho za ukamilishaji na kabla ya Oktoba 20 vitakuwa vimepata umeme.

Kwa upande wa vitongoji, Mhandisi Malingumu amesema kuwa Mkoa wa Morogoro unajumla ya vitongoji 3,369 na katika hivyo, vitongoji 1,655 sawa na asilimia 49 tayari vimepatiwa umeme.

“Katika kipindi cha miaka miwili tunategemea vitongoji 455 vya Mkoa wa Morogoro vitapatiwa umeme. Ndani ya hivyo, 289 mkandarasi tayari yuko site na anaendelea na kazi kupitia mradi wa ujazilizi yaani Densification IIB. Aidha, vitongoji 166 vitapatiwa umeme kupitia mradi huu tunaotambulisha mkandarasi wake leo kwa gharama ya shilingi Bilioni 17.9.” Amefafanua Mhandisi Malingumu.

Mhandisi Malingumu pia amemuhakikishia Mkuu huyo wa Mkoa kuwa REA imejipanga vyema kuhakikisha umeme unafika kwenye vijiji vyote na safari ya kupeleka umeme katika vitongoji inaendelea kulingana na upatikanaji wa fedha.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Kampuni SINOTEC CO. LTD, Zhang Jianguang ameahidi kutekeleza mradi huo kwa wakati na kwa ubora na kwamba tayari ameanza maandalizi yote muhimu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles