Joseph Hiza na Mashirika ya Habari,
WATOTO wachanga wanajulikana kwa kulala saa nyingi ambazo hupungua kwa kadiri umri wao unavyoongezeka.
Hata hivyo, hakuna mfumo rasmi ya kulala kwa ajili ya watoto wachanga kwa sababu saa zao mwilini huwa hazijakamilka.
Wao kwa ujumla huwa wanalala kwa saa 16 hadi 20 kwa siku, hii ni kati ya usiku na mchana, hali ambayo hutoweka wanapokua.
Lakini mwanamke mmoja nchini Uingereza anaugua maradhi yanayomfanya aamke baada ya kulala saa hadi 22 kati ya zile 24 za siku.
Mwanamke huyo, Beth Goodier (20), anaugua maradhi ya kulala sana isivyo kawaida, ambayo hujulikana kwa kitaalamu kama ‘Kleine-Levin Syndrome (KLS),’ yakiwa yametawala maisha yake.
Hali hiyo ya kinyorojia, ambayo ilianza wakati alipokuwa na umri wa miaka 16, inamaanisha kuwa mwanamke huyo analala wastani wa saa 18 kwa siku.
Wakati hali hiyo inapomkumba, mara nyingi kila baada ya wiki tano, anaweza kulala kati ya wiki moja na tatu na huhitaji uangalizi wa saa 24.
Hata wakati anapoamka anaweza kuwa na hali kama ya mtoto mchanga, akiwa katika mkanganyiko na kutoweza kueleza tofauti baina ya uhalisia na ndoto.
Inaaminika kuwa kuna watu 40 tu nchini Uingereza na 1,000 duniani wanaougua maradhi hayo, asilimia 70 kati yao wakiwa wavulana.
Haijaweza kujulikana kisababishi cha hali hiyo wala dalili zake, huku ikiwa haina tiba.
Beth mkazi wa Stockport, Greater Manchester, nchini humo alionekana hivi karibuni wakati wa kipindi cha Breakfast cha Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC).
Akijadili jinsi alivyokata tamaa kwa hali hiyo inayomkabili alisema; “Natumia nusu ya maisha yangu kitandani, yamekuja katika wakati nyeti wa maisha yangu.
“Hakika yamekuja kipindi ambacho mtu unaelekea utu uzima, unapaswa kuwa chuo kikuu, kupata ajira na kujitambua katika jamii.
“Maradhi haya yamechukua yote hayo kutoka kwangu katika wakati muhimu wa kujiandalia msingi wa maisha ya baadaye. Hivyo maisha yangu yanashikiliwa mateka na maradhi haya,” anasema.