Faraja Masinde
JUNI 20, kila mwaka, huwa ni siku ya wakimbizi duniani, maadhimisho haya yalianza mwaka 2000.
Kwa mujibu wa tafsri isiyo rasmi, mkimbizi ni mtu aliyeondoka nyumbani kwake mahali anapoishi kwa sababu ya kulazimishwa, kufukuzwa au kwa hofu ya kuteswa.
Aidha, kuna mapatano ya kimataifa yanayoratibu hali hii, chini ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa (UN), kuhusu Hadhi ya Wakimbizi kutoka mwaka 1951, mkimbizi ni mtu ambaye kutokana na hofu ya kweli ya kuteswa kwa sababu ya rangi, dini, utaifa, uanachama wa kikundi fulani cha kijamii, au maoni ya kisiasa, yumo nje ya nchi yake, na ameshindwa au, kutokana na hofu hiyo, hana nia ya kutegemea ulinzi wa nchi hiyo.
Maisha hayo ndiyo aliyopitia Barthelemy Berthelemy, ambaye ni mkimbizi wa Burundi na mfanyikazi wa Médecins Sans Frontières kwa maana ya Madaktari Wasio na Mipaka (MSF) katika kambi ya Nduta, Kaskazini Magharibi mwa Tanzania, ambapo MSF ndiye mtoaji wa huduma ya afya kwa wakimbizi 75,000.
Barthelemy anasema kuwa alianza safari ya kushangaza ya kuusaka usalama wa maisha yake akiwa na familia yake mwaka 2015.
Katika mwelekeo wake huo mpya, anasema kuwa alihisi na kuamiani kuwa Tanzania ndiyo ilikuwa sehemu bora na salama kwake kuishi kama anavyosimulia.
“Ninapofikiria mji wangu, ninakumbuka siku za joto, zilipanda baiskeli kwenye ziwa la dhahabu Ziwa Tanganyika, ambapo viboko hutoka kwenye uso na watoto hucheza majini wakati wa jua. Nakumbuka mavazi ya rangi safi ya marafiki waliokusanyika na kanisa la bluu na nyeupe na sauti ya mchungaji kutoka kwenye mimbari ya jua.
“Nakumbuka siku niliyohitimu kutoka chuo kikuu: uso wenye furaha na rafiki yangu wa kike na nakumbuka nilikuwa na furaha.
“Lakini Uchungu nilianza kuupata mwakak 2015, nakumbuka siku hiyo milio ya bunduki ilivuma kila mahala na kumbukumbu hizo za kusikitisha hazitoiacha akili yangu. Ni kipindi ambacho niliona vitu vikibadilika kwenye akili yangu.
“Nakumbuka jioni moja, watu wawili wenye bunduki waliingia nyumbani kwangu na kunilazimisha kulalia tumbo huku wakinitishia kunipiga risasi wakati wanaiba mali zangu. Baada ya hapo, nilipata uchungu mkubwa ikiwamo maumivu yaliyotokana na kukandamizwa chini kwa muda mrefu na kitako cha bunduki, huo ulikuwa ni mwanzo wa kuanza kuzuka kwa vurugu nyumbani kwangu pamoja na maeneo mengine,” anasema Barthelemy.
Anasema hiyo ndiyo ilikuwa ishara ya yeye kufikiria safari ya kuondoka kabisa mbali na eneo hilo ili kuinusuru nafsi yake na ndoto zake.
“Nilijua ni lazima niondoke, ingawa sikutaka kuacha kazi, familia yangu, kanisa langu na nyumba yangu. Nilimbusu mpenzi wangu nikamwambia kwaheri, siyo siri kwamba nilijisikia vibaya, nasema sijui ninakoenda lakini nikifika nitawafahamisha,” anasema Barthelemy katika ahadi aliyoitoa kwa mpenzi wake.
Anafafanua kuwa alianza safari kwa kuendesha baiskeli akiwa amebeba mkoba na nguo kadhaa ikiwamo pia bibilia yake, simu ya mkononi na kiasi cha fedha Dola 80 mfukoni.
“Niliendesha baiskeli kwa muda mrefu, huku nikijicha nyuma ya majengo na miti wakati nilipokuwa nikisikia milio ya bunduki. Nilitembea kupitia miji yenye watu wengi wakati mapigano yalipokuwa yakiendelea kurindima mithiri ya kengele za kanisa saa ile.
“Baada ya siku tano za baiskeli na kulala katika vijiji vya mitaa, nilivuka hadi wa Tanzania, nguo zangu zilikuwa za maji na uso wangu ulikuwa umechoka na uchovu, hapa ndipo maisha yangu kama mkimbizi yakaanza,” anasema Barthelemy.
Anasema mwanzoni alikaa na wanaume karibu 20 katika ukumbi katika kituo cha wakimbizi wa usafiri karibu na mpaka wa Tanzania ambapo walilala kwenye mikeka, sakafu ngumu ya matope na kula mahindi yaliyochanyanywa na maji.
“Niliimba kwa watu, na kwa pamoja tuliomba kwamba tutapata makazi, maji na usalama. Baada ya wiki moja, nilihamishwa na Umoja wa Mataifa(UN) kwenda kambi ya Nyarugusu, nyumbani kwa wakimbizi wapatao 150,000 kutoka Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
“Nilipofika kambini mvua ilinyesha kwa ghafla na niliweza kuona ilikuwa bahari ya matope yaliyotawanyika na karatasi nyeupe za plastiki zilizowekwa na miti yenye kutu.
“Nilishiriki hema yangu na wanaume wengine sita, kulala kitandani kwenye sakafu ngumu, nimevaa nguo huku nikitetemeka kutoka kwenye uchafu hatua ambayo ilisababisha kuzungukwa na chawa kila mahali,” anasema Barthelemy.
Anasema mwanzoni alikuwa akijihisi kuwa yuko mwenyewe lakini baadaye aliona watu wengine wengi wakiwa wamemzunguka hatua iliyomwezesha kupata nguvu.
“Tulikusanya kuni kwa ajili ya moto na tulikaa karibu na moto usiku huku tukipika uji na kusimuliana hadithi juu ya nyumba zetu na familia. Niligundua kuwa siko peke yangu na kwamba ndugu zangu wengi hapa waliteseka zaidi kuliko mimi. Tulikuwa wamoja na tulishikamana na kuondoa dhana ya ukimbizi, lakini kama wanadamu,” anasema Barthelemy.
Anasema miezi miwili na nusu baadaye alihamishwa kambi na kupelekwa Nduta Kaskazini Magharibi mwa Tanzania.
“Nilitoka kulala chini kwenye plastiki hadi kulala ndani ya hema hata hivyo, baadaye niliweza kujenga nyumba yangu mwenyewe ya miti niliyoijenga kwa kuni kavu na matope, na kisha tulijenga kanisa jipya la kambi hiyo,” anasema.
Anasema baada ya kukaa kwa muda mrefu hatimaye alipata kazi katika Shirika la Mdaktari Wasio na Mipaka (MSF).
“Katika MSF, mimi nafanya kazi na madaktari, wauguzi na wahandisi kutoka ulimwenguni kote, pamoja na Watanzania, na ninahisi hisia kubwa za kuwa wamhimu.
“Kwani sisi ndiyo watoa huduma pekee ya kiafya katika kambi hiyo na tunatoa matibabu ya kuokoa maisha kwa ugonjwa wa malaria, kisukari na shida zingine za kutishia maisha ambazo watu wanakabiliwa nazo kambini.
“Juni 2016 rafiki yangu wa kike aliondoka Burundi kuanza safari ileile hatimaye tuliunganishwa tena katika Kambi ya Wakimbizi ya Nduta. Baada ya mwaka wa kujitenga, tukiwa na hofu kwa maisha ya kila mmoja, tulifunga ndoa kanisani, leo hii tuna mtoto wa kiume anayeitwa GoodLuck,” anasema Barthelemy.
“Nimeishi nikiwa mkimbizi kwa miaka mitano nchini Tanzania na ninachoomba ni: “Tafadhali, usituhukumu kwa sababu sisi ni wakimbizi. Sisi sio waovu wala wabaya, sisi ni wanadamu kama wewe, tunaishi na tunahisi, na hofu na ndoto, kama mwanadamu yeyote. Kilichotokea kwetu kinaweza kutokea kwa mtu yeyote duniani. Hakuna mtu anachagua kuwa mkimbizi.
“Natumai kwamba siku moja nitaweza kurudi nchi ya mama yangu, mahali salama, kwenye kanisa langu, ninakosa familia yangu. Siku moja, nitaijenga nyumba yangu mwenyewe kwenye ardhi ninayomiliki,” anasema Barthelemy.
Takwimu za Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuwahudumia Wakimbizi, UNHCR, zinaonesha kwamba, kuna watu takribani milioni 80 kutoka sehemu mbalimbali duniani ambao wamelazimika kuishi kama wakimbizi, wahamiaji, watu wasiokuwa na makazi maalum pamoja na watu wanaotafuta hifadhi ya kisiasa.
Huku kukiwa na watoto milioni 13 ambao wamelazimika kuishi kama wakimbizi na wahamiaji. Umoja wa Mataifa (UN) umetenga ulitenga Juni 20 ya kila mwaka kama siku ya wakimbizi duniani ambapo kwa mwaka huu unaadhimisha kumbukumbu ya miaka 20 tangu Siku ya Wakimbizi Duniani ilipoanzishwa mwaka 2000, kama kumbukumbu ya Mkataba wa Wakimbizi Duniani uliotiwa saini na Jumuiya ya Kimataifa mwaka 1951.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, katika maadhimisho ya Siku ya Wakimbizi Duniani, alisema Umoja wa Mataifa hauna budi kujifunga kibwebwe ili kukomesha vita, kinzani na migogoro ya kijamii inayoendelea kusababisha mamilioni ya watu kuyakimbia makazi na nchi zao ili kutafuta hifadhi, usalama na maisha bora zaidi.