Na PATRICIA KIMELEMETA – DAR ES SALAAM
LICHA ya wadaiwa sugu wa Benki ya Twiga Bancorp kuanza kurudisha fedha walizokopa kwenye benki hiyo baada ya kufilisika, mpaka sasa uongozi wa benki umeshindwa kuwataja wadaiwa hao.
Akizungumza na gazeti hili jijini Dar es Salaam jana, Meneja Msimamizi wa Benki Kuu (BoT), Nkanwa Magina, alisema kuwa, hali ya kifedha ndani ya benki hiyo imeanza kurejea tangu walipoanza kazi Novemba 8, mwaka huu, baada ya kufungiwa kwa muda kutokana na kufilisika hadi kufikia asilimia 10 hadi 12.
Alisema, hali hiyo imebadilika baada ya wadaiwa sugu kuanza kulipa madeni yao, jambo ambalo limechangia kupunguza ukubwa wa tatizo.
“Siwezi kuwataja wadaiwa sugu wa benki kwa sababu sheria za kibenki zinatubana, lakini ninachoshukuru hadi sasa ni kwamba wameanza kujitokeza kulipa madeni yao, jambo ambalo limechangia kuongezeka kwa mtaji,” alisema Magina.
Aliongeza, katika kipindi hiki ambacho benki hiyo ipo kwenye mchakato wa kumtafuta mwekezaji ili aweze kuwekeza, tayari imeanza kufanya vizuri sokoni kutokana na kuongezeka kwa wateja wapya na wale wa zamani kuanza kuweka fedha zao, jambo ambalo limechangia mzunguko wa fedha kuwa vizuri.
Alisema, kabla ya kufungiwa, benki hiyo ilipitia katika wakati mgumu, baada ya wadaiwa hao kushindwa kurudisha fedha hizo, jambo ambalo lilichangia kuyumba kwa mtaji.
Alisema, mkakati uliopo ni kuhakikisha kuwa, wanaendelea kukusanya madeni ili waweze kuongeza mtaji, ambao utawasaidia wawekezaji kuvutiwa kuwekeza kwenye benki hiyo.