Na Mwandishi Wetu, Mbarali
BENKI ya NMB imezindua huduma mpya ya mkopo wenye riba nafuu kwa ajili ya kuwasaidia wananchi wenye kipato cha chini kutekeleza takwa la kisheria la kurasmisha makazi yao ijulikanayo kwa jina la ‘NMB Plot Loan.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Ndani wa NMB, Benedicto Baragomwa aliyasema hayo wilayani Mbarali katika Mkoa wa Mbeya wakati wa Uzinduzi rasmi wa Programu ya Kitaifa ya Urasimishaji wa Makazi ambayo inatekelezwa kwa ushirikiano kati ya Benki hiyo na Wizara ya Ardhi, Nyumba na maendeleo ya makazi.
Alisema Benki ya NMB itawasaidia wananchi kulipia gharama zote za urasimishaji wa makazi kuanzia upimaji wa viwanja mpaka uandaaji wa Hatimiliki na kwamba mwananchi atalipa kidogo kidogo ndani ya miaka miwili.
Alisema riba ya mkopo huo ni asilimia 10 na kwamba mwananchi atapatiwa hatimiliki baada ya kukamilisha urejeshaji wa mkopo wake katika benki hiyo.
“Tumeanzisha huduma hii kwa sababu kuna wananchi wamekuwa wakishindwa kurasmisha makazi yao kutokana na kukosa fedha za kulipia gharama za urasmishaji, wananchi wakisharasimisha makazi yao na kupatiwa hatimiliki watakuwa na sifa za kukopesheka na benki yoyote,” alisema Baragomo.
Alisema Mwananchi yeyote ambaye atakopeshwa mkopo huo atafunguliwa akaunti ya NMB bila gharama yoyote kwa maelezo kuwa fedha hizo zinapitia benki na hata marejesho yatapitia benki.
Akizindua Programu hiyo ya Urasmishaji wa makazi kitaifa, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi aliipongeza Benki ya NMB kwa kuanzisha huduma hiyo akidai kuwa itasaidia wananchi kupandisha hadhi makazi yao.
Alisema asilimia kubwa ya wananchi wanaishi kwenye makazi holela ambayo yamejengwa bila kufuata sheria na hivyo Serikali badala ya kuyabomoa imeamua kuyarasimisha ikishirikiana na Benki ya NMB ushirikiano ambao alisema haujawahi kutokea.
Lukuvi alisema kwa mujibu wa sheria kila mwananchi anatakiwa kujenga nyumba kwenye kiwanja kilichopimwa, chenye hatimiliki na lazima apate Kibali cha Ujenzi kitu ambacho alidai watanzania wengi hawatekelezi na hivyo kuwa na idadi kubwa ya makazi holela.
“Tulianza kutekeleza urasmishaji huu wa makazi mwaka 2013 lakini mpaka sasa tumefikia asilimia tano pekee nchi nzima, hii ilikuwa inasababishwa na wananchi wengi kukosa fedha za kugharimia, sasa hii huduma ya NMB Plot Loan itatusaidi kurasimisha makazi mengi zaidi,” alisema Lukuvi.
Hata hivyo alisema awali gharama za urasimishaji wa makazi ilikuwa Sh. 150,000 lakini sasa hivi Serikali imepunguza kiwango hicho na kufikia Sh. 130,000 na kwamba kwa sasa gharama hizo zitabebwa na Benki ya NMB na wananchi watalipa kidogo kidogo.
Alisisitiza kwamba kwa sasa mtu yeyote ambaye amejenga mjini ni lazima arasimishe makazi yake tofauti na wale wanaoishi maeneo ya vijijini ambao utaratibu utaendelea kuboreshwa.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera alisema zoezi hilo la urasmishaji wa makazi utasaidia kupunguza migogoro ya ardhi katika maeneo mbalimbali ya Mkoa huo yakiwemo yanayopakana na Hidahi.
Aliwataka wananchi kuchangamkia fursa ya mkopo huo ambao una riba ndogo na kujitokeza kwa wingi kujiandikisha kurasmisha makazi yao huku akimhakikishia Waziri Lukuvi kuwa watashirikiana kukamilisha zoezi hilo.