MWANDISHI WETU
Benki ya Exim Tanzania imezindua kampeni iitwayo ‘Exim kazini leo kwa ajili ya kesho’ yenye lengo la kutilia mkazo mahusiano yake kwenye soko la kibenki Tanzania.
Kampeni hiyo ya miezi 12 ni mwendelezo wa kauli mbiu ya Benki ya Exim “Innovation is life” inayolenga kuangazia huduma za benki ya Exim zinazokidhi mahitaji ya wateja wa aina mbalimbali.
Akizungumza na waandishi wa habari katika uzinduzi wa kampeni hiyo, Mkuu wa Kitengo cha Masoko na Mawasiliano kutoka Exim, Stanley Kafu alisema benki hiyo kwa kupitia ubunifu kwenye huduma zake inaendelea kuweka dhamira ya kuboresha maisha na lengo kuu ni kujidhatiti kwenye mafanikio, ukuaji na maendeleo ya wateja wa benki hiyo.
“Kwa miaka mingi, Exim imekuwa sehemu ya ubunifu na imekuwa ikijidhatiti katika kuboresha kesho ya wateja wetu na jamii inayotuunga mkono na kutuzunguka kwa kuhakikisha inakuwa bora zaidi na ndiomana tupo kazini leo kwa ajili ya kesho yao.” alisema.
Alisema kampeni hii inadhumuni la kuonesha umuhimu wa kuifikiria kesho yako na kuanza kuifanyia kazi leo kwa kuwa ili mteja aweze kunufaika na yajayo, inatakiwa kujipanga vyema leo.
Alisema benki ya Exim imekuwepo kwa kipindi cha zaidi ya miaka 21 ikitoa huduma zenye ubunifu kwa wateja wake kwa maendeleo ya leo na kesho yao.
“Kampeni hii itakayoendeshwa kwa kipindi chote cha mwaka imetengenzwa kwa ajili ya wateja wote wa benki ya Exim kwenye mikoa yote na tayari imeshaanza kuonesha mafanikio kupitia baadhi ya programu kama vile “Deposit Utokelezee” ambayo imewapa wateja wa benki uwezo wa kupata faida kupitia riba.
“Hadi mwisho wa kampeni hii, tunatumaini kuwa tutakuwa tumetilia mkazo dhamira yetu kwa wateja wetu huku tukizungumzia zaidi nafasi ya benki yetu kwenye soko na kuiweka benki yetu kama moja ya benki mzawa inayohudumia wateja binafsi na mashirika au taasisi mbalimbali,” alisema.
Alisema benki hiyo imesherehekea miaka 21 ya mafanikio, ukuaji na uongozaji kwenye soko la kibenki ndani ya bara la Afrika huku ikipanua soko lake kwa kufungua matawi zaidi kwenye nchi za Comoro (2007), Djibout (2011) na Uganda (2016).