26.9 C
Dar es Salaam
Friday, January 3, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Benki ya Azania yazindua tawi jipya Dodoma

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

BENKI ya Azania imezidi kujitanua baada ya kuzindua tawi lake jipya jijini Dodoma, ikiwa ni mkakati wake wa kukuza mtandao wa matawi yake na kuunga mkono jitihada za Rais Dk. John Magufuli kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa tawi hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Charles Itembe, alisema kwa sasa benki hiyo ina matawi 19 ikiwamo hilo jipya lililopewa jina la Sokoine-Dodoma ikiwa ni ishara ya benki hiyo kutambua mchango wa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Sokoine, katika ustawi wa taifa kwa ujumla.

“Malengo yetu ya kimkakati kwa sasa ni kukuza mtandao wa matawi ya benki yetu, angalau matawi matatu kwa mwaka na pia kukuza nafasi yetu ya umiliki wa soko (market share) angalau kwa asilimia tatu ndani ya miaka mitatu,” alisema Itembe.

Alisema nia ya benki hiyo ni kuwa katika hadhi ya benki kubwa daraja la kwanza katika kipindi cha ndani ya miaka hii mitano ya kimkakati wa kibiashara.

Kuhusu uamuzi wa kufungua tawi hilo jijini humo, Itembe, alisema: “Dodoma ni katikati ya nchi, pili ni makao makuu ya shughuli za kiserikali na pia ni mkoa unaokuwa kwa kasi kibiashara.”

Alisema kupandishwa hadhi kwa Manispaa ya Dodoma na kuwa jiji kumeiweka benki hiyo katika nafasi nzuri kwa kuwa ukuaji wa jiji hilo unaendana sambamba na mahitaji ya kifedha.

“Katika kuunga mkono sera ya Rais John Magufuli ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda, ni lazima kuwa na mbinu ya kuweza kukuza kipato kupitia kufanya biashara na benki zenye msingi imara. Tupo tayari kushirikiana na wananchi na Serikali katika kufanikisha hilo,” alisema.

Akizungumza kabla hajazindua rasmi tawi hilo, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Ashatu Kijaji, mbali na kuipongeza menejimenti ya benki hiyo, alitoa changamoto kwa taasisi za fedha hapa nchini ikiwamo benki hiyo kuhakikisha zinajipanga kikamilifu kukabiliana na suala la mikopo chechefu na kupunguza gharama za uendeshaji ili ziweze kuwahudumia wateja wake ikilinganishwa na hali ilivyo sasa.

“Chanzo cha mikopo chefu ni watumishi wasio waadilifu kwenye taasisi hizi na ndiyo maana naomba bodi na menejimenti ziwachukulie hatua sambamba na kupunguza gharama za uendeshaji kwa sababu sisi kama Serikali hatutavumilia uzembe wa aina yoyote katika utekelezaji wa hili,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles