NA RAMADHAN HASSAN, DODOMA
BARAZA la Vijana la Chadema (Bavicha), limesema litatoa tamko kuhusu kauli ya Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, aliyewataka wasije mjini hapa kuzuia mkutano Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Juzi Mbowe akiwa mkoani Arusha katika mkutano wa mameya na wenyeviti wa halmashauri 18 zinazoongozwa na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), aliwataka vijana hao wasiende kuzuia mkutano huo hadi watakapopewa taarifa nyingine.
Akizungumza mjini hapa jana, Makamu Mwenyekiti wa Bavicha, Patrick ole Sosopi, alisema watatoa tamko baada ya viongozi wao wanaoshikiliwa na Jeshi la Polisi kuachiwa.
Kwa mujibu wa Sosopi, viongozi wenzao watakapoachiwa, wataitisha kikao cha dharura cha Kamati ya Utendaji ya Bavicha kujadili kauli ya Mbowe.
“Ili tuonyeshe msimamo juu ya uamuzi wa mwenyekiti wetu wa ama kukubaliana naye au kutokukubaliana naye, tutazungumza baada ya viongozi wetu kutoka ndani.
“Bavicha ni taasisi kubwa na kiongozi wetu ni Mbowe, tunaheshimu tamko lake, lakini tunasubiri kwanza viongozi wetu watoke ndani ndipo tujadili kauli ya kiongozi wetu.
“Kuna vijana wameshatekeleza agizo la kuanza kwenda Dodoma, lakini sasa nawataka vijana wote nchini watulie hadi hapo tutakapopata majibu ya kikao cha Baraza la Utendaji,” alisema Sosopi.
Wakati huo huo, viongozi wa Baraza hilo wanaoshikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani hapa, hawakufikishwa mahakamani kama ilivyoelezwa juzi na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Lazaro Mambosasa.
Kutokana na hali hiyo, wakili anayewatetea watuhumiwa hao, Fred Kalonga, alisema hajui sababu za wateja wake kutofikishwa kizimbani.
“Nashangaa hakuna mteja wangu hata mmoja aliyeletwa, ingawa nilijua wataletwa hapa. Lakini tunaendelea kufuatilia ili kesho (leo) wafikishwe mahakamani,” alisema Kalonga.
Viongozi wa Bavicha wanaoshikiliwa na jeshi hilo ni Mwenyekiti wa Taifa, Patrobas Katambi, Katibu Julius Mwita, Mwenyekiti Mkoa wa Mbeya, George Tito na Mratibu wa Uenezi na Uhamasishaji, Edward Simbeye.
Hongera Patrick Ole Sosopey