Mwandishi Wetu -Dar es Salaam
WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa amekutana na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Usajili wa Biashara na Leseni (Brela), Godfrey Nyaisa kwa mara ya kwanza tangu alipomteua kuchukua nafasi hiyo.
Bashungwa na Nyaisa walikutana jana katika ofisi ndogo ya wizara iliyopo Waterfront, Dar es Salaam ili kujadili dira mpya ya Brela.
Katika mazungumzo yake, Bashungwa alimtaka Nyaisa kuhakikisha analipa uzito wa kipekee suala la uboreshaji wa mfumo wa usajili kwa njia ya mtandao (ORS) pamoja na huduma kwa mteja ili kupunguza usumbufu kwa wadau.
“Ninakutaka ufanyie kazi mapungufu yote yaliyopo Brela, hasa upande wa mifumo na huduma kwa wateja ili kwenda na kasi ya Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli ya kuwa na Tanzania ya viwanda,” alisema Bashungwa.
Aidha Bashungwa alibainisha kuwa Brela ni mlango wa wawekezaji na wafanyabiashara, hivyo huduma inapokuwa nzuri wateja wataongezeka, pia mapato ya nchi yataongezeka.
Kwa upande wake, Nyaisa alitoa shukrani zake kwa uteuzi aliopata na kuahidi kufanya maboresho makubwa.
“Nakuahidi kujenga Brela mpya itakayojibu mahitaji ya wadau wake wote kwa haraka.
“Nitumie fursa hii pia kuwajulisha wadau wote kuwa tunaandaa mkutano nao kwa nia ya kufahamiana, kupata maoni na ushauri wao katika kuijenga Brela mpya,” alisema Nyaisa.
Nyaisa aliteuliwa Januari 19, mwaka huu akichukua nafasi ya Loy Muhando aliyekuwa akikaimu nafasi hiyo.