25.8 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 16, 2024

Contact us: [email protected]

Ukatili dhidi ya wanawake kwenye matibabu ukomeshwe

Benjamin Masese -Mwanza

HIVI karibuni kumeibuka vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake ambao kwa namna moja au nyingine wamekuwa wakijikuta katika wakati mgumu, pale wanapowafuata wataalamu wa afya maeneo yao ya kazi ili kupata huduma.

Vitendo hivyo vikiwamo kuchomwa sindano ya dawa za usingizi na kubakwa, vinafanywa na wataalamu wa afya ambao wameaminiwa na Serikali, lakini tunashuhudia wakikiuka maadili ya kazi zao na kuingiwa na tamaa ya ngono.

Matukio ya namna hii yamekuwa yakifanywa na madaktari na wale waganga wa kienyeji ambapo hivi karibuni tulishuhudia jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza likimshikilia Hemed Jumanne (40) mkazi wa Sengerema ambaye ni mganga wa kienyeji akidaiwa kumbaka mwanamke mmoja (miaka 32) jina linahifadhiwa, aliyefika kwake ili kupata tiba.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Jumanne Muliro, mganga huyo anadaiwa kutenda kosa hilo Januari 4, 2020 katika Mtaa wa Jiwe Kata ya Igogo, Wilaya ya Sengerema ambapo alifafanua kwamba baada ya mwanamke huyo kufika kwa mganga kwa lengo la kupata tiba, ndipo aliingiwa na tamaa za kimapenzi na kumpa dawa za kumpumbaza na kisha kumbaka.

Cha kusikitisha ni pale mganga huyo kudaiwa kujipaka dawa kwenye sehemu zake za siri na baadaye kumwingilia mwanamke huyo huku akidai anampatia matibabu. Hakika kitendo  hicho ni cha kikatili, kinyama na ni kosa la jinai.

Unaweza kujiuliza maswali mengi sana kwa kitendo hicho alichofanyiwa mwanamke huyo, kwanza haijulikani kama mganga huyo au mwanamke ni mwathirika wa magonjwa ya zinaa ikiwemo Ukimwi au la, na iwapo baada ya kitendo hicho inawezekana akapata mimba ambayo inaweza kusababisha ndoa yake kuvunjika.

Wakati wananchi wanafikiria tukio hilo la mganga wa kienyeji na mgonjwa wake, hivi karibuni tumeona tukio jingine la mganga katika Kituo cha Afya cha Serikali mkoani Tabora, akidaiwa kumbaka mjamzito baada ya kumchoma sindano ya usingizi.

Licha ya mjamzito huyo kusindikizwa na mtu wa jinsia ya kike kutoka nyumbani kwenda hospitalini kwa ajili ya vipimo vya mimba, lakini cha kushangaza daktari anadaiwa aliingiwa na tamaa ya ngono na kumlaghai kwamba ujauzito huo upo hatarini kuharibika hivyo alihitaji matibabu.

Katika matibabu hayo anadaiwa alimchoma sindano ya usingizi huku akiamuru yule msindikizaji kutoka nje amuache mgonjwa apumzike kumbe ambapo alitumia fursa hiyo kumbaka mjamzito huyo wa miezi minne lakini alipozinduka alijigundua tayari amefanyiwa ukatili wa kingono.

Si kwamba vitendo hivi ni vigeni lakini vinaonekana kuongezeka, hivyo kuna haja ya Serikali kuweka mkakati wa kuthibiti ukatili huu, inawezekana mtu anayediriki kufanya kitendo hicho katika eneo lake la kazi basi ana uwezo wa kuvifanya nje ya hapo.

Ni wakati mwafaka waziri mwenye dhamana ya sekta ya afya, akawa mkali na kuwachukulia hatua za kisheria wahusika, pia wale waganga wa kienyeji nao wanapaswa kufutiwa usajili wao na kuchukuliwa hatua za kisheria.

Hivi sasa, wanawake wengi wanaogopa kutibiwa na wanaume katika hospitali na vituo vya waganga wa kienyeji kwa hofu ya kuchomwa au kunyweshwa dawa la usingizi na kufanyiwa ukatili, sasa kama suala hili halitachukuliwa kwa uzito wake itafikia hatua wanawake wakahitaji kutibiwa na wanawake wenzao.

Binafsi nawasihi wananchi kujiepusha kupenda kutibiwa na waganga wa kienyeji hasa wale ambao wanajivisha mwamvuli wa waganga wa jadi kumbe lengo lao ni kutapeli watu na kufanya vitendo vingine vya jinai, lakini pia mamlaka zishughulikie kwa uwazi kudhibiti matendo haya katika sehemu zote za tiba.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles