25.7 C
Dar es Salaam
Thursday, November 28, 2024

Contact us: [email protected]

Bashe amrarua Kinana

*Asema analenga kuigawa CCM, kumdhofisha Rais
*Amuunga mkono JPM 2020, Msekwa naye ajibu waraka wao kwa hoja tatu

MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM

MBUNGE wa Nzega Mjini (CCM), Hussein Bashe, amesema waraka ulioandikwa na makatibu wakuu wastaafu wa chama hicho, Yusuf Makamba na Abdulrahman Kinana, una malengo ya kugawa chama hicho na kumdhoofisha Rais Dk. John Magufuli.


Wiki iliyopita Kinana na Makamba waliandika barua kwa Baraza la Wazee wa CCM, wakitaka lichukue hatua dhidi ya tuhuma zilizoelekezwa kwao kwa madai kuwa zimewachafua na viongozi wa chama hicho hawachukui hatua.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Bashe alisema “Moja Kinana na wenzie walichokifanya ni kukigawa chama na kutaka kumuondolea Rais Magufuli uhalali.

“Kinana ni mnafiki anafahamu alichokifanya ni kinyume kabisa na Katiba, Baraza la Wazee kikatiba halishughuliki nayo. Kinana anafahamu alichokifanya kina malengo makubwa mawili moja ni kugawa na pili kumdhohofisha Mwenyekiti wa CCM (Rais John Magufuli).

“Jambo hili halikubaliki yeye hana Moral authority, anachokifanya Kinana na waraka wake ni kuigawa nchi na na kumdhoofisha mgombea wetu, ambaye kwa mwaka ni Magufuli pekee, tutamuunga mkono kwa nguvu zote.”


Bashe alisema hawawezi kuruhusu Magufuli ni ambaye ni mwenyekiti wao na mgombea uraia wa chama hicho 2020 achafuliwe.
“Lije jua ije mvua, hatuwezi kuruhusu hatua ambayo inadhoofisha uhai wa chama,” alisema Bashe.


Alisema anashangazwa na hoja ya Kinana kulalamikia kuchafuliwa na Musiba huku akisahau na yeye ndiye alikuwa kiongozi wa kuchafua wenzake katika zaidi ya miaka 40 aliyokuwa na pia akiwa Mjumbe wa Kamati Kuu.


“Ni ajabu sana kwa mtu kama Kinana (Abdulrahman) eti sasa analalamika kuwa anachafulia na Musiba (Syprian), na anachokifanya Musiba ndicho na yeye Kinana alishiriki kwenye mitandao ya kuchafua watu kwa masilahi wanayojua wao. Sasa anatoka hadharani kulalamika huku akijua kwamba naye alimiza watu kwa mtindo kama huu

“Aache kulalamika sasa anajua utaratibu wa chama unaeleleza nini na namna ya kuwasilisha malalamiko… huu ninauita ni unafiki wenye lengo la kutaka kukigawa chama na kumkwamisha Rais Magufuli, jambo ambalo katu hawezi kufanikiwa kwani CCM tupo pamoja na Mwenyekiti wetu ambaye pia ndiye mgombea wetu mwaka 2020,” alisema Bashe

Msekwa awajibu kwa hoja tatu

Katibu wa Baraza la Wazee wa CCM, Pius Msekwa, naje alijibu waraka wa kina Kinana kwa hoja tatu kupitia barua yake ya Julai 15, iliyokuwa na kichwa cha habari cha ‘barua ya majibu ya awali’.

Barua hiyo ambayo Msekwa alipotafutwa na MTANZANIA alikiri kwamba ni yake, ilijibu mambo makuu mawili yaliyokuwa kwenye barua ya Makamba na Kinana kwa kujikita kwenye hoja tatu.

Sehemu ya barua hiyo Msekwa ilisema “Nakiri kupokea barua yenu ambayo mliisaini wote wawili na ikawasilishwa kwangu kwa mkono na Mheshimiwa Nape Nnauye.”

Katika barua yake hiyo, Msekwa alitoa muhtasari wa alichokielewa kwenye barua ya Kinana na Makamba, akisema “baada ya kuisoma kwa makini, nimetambua kwamba malengo makuu ya barua hiyo, yalikuwa ni mawili.

“Kuwasilisha kwa pamoja malalamiko yenu dhidi ya mtu
ambaye “amekuwa akitoa maelezo yenye kuwatuhumu na kuwazushia uwongo ninyi, na viongozi wengine wastaafu wa CCM na wa Serikali waliostaafu na walioko madarakani, kwamba eti mnamhujumu Rais kutekeleza majukumu yake” (ukurasa wa kwanza, para ya pili).”

“Kuomba Baraza la Viongozi Wakuu Wastaafu wa CCM ‘walishughulikie jambo hili, kwa namna ambayo wazee wenyewe wataona kuwa inafaa,’ (ukurasa wa pili,
para ya mwisho.”

“Zaidi ya hayo, nimezingatia maelezo yenu ya kuwa tuliamini kwamba, kama utaratibu wa CCM ulivyo, kazi ya kulinda heshima ya CCM ni pamoja na kukemea vikali, pale viongozi wake wakuu wa sasa na waliostaafu
wanapochafuliwa.

“Kwa hiyo basi, tulitegemea wahusika ndani ya chama watazikemea kauli zake anayewachafua, na kumuasa asitumie jina la Mwenyekiti wa CCM kuchafua na kudhalilisha watu au kumchukulia hatua nyingine muafaka. “Kwa bahati mbaya, hili halikufanyika”. (ukurasa wa kwanza, para ya tatu).”

“Kwa maelezo hayo, barua yenu inachukua sura ya “rufaa kwa wazee” hawa, kutokana na kuona kwamba chama “kimeshindwa kukemea vikali jambo hili,” barua hiyo ilimaliza kutoa muhtasari wa ile ya kina Makamba.

Akianza kutoa majibu yake ya awali kwa wastaafu hao, Msekwa kwenye barua yake hiyo alisema “Kama mnavyofahamu, baraza hili hufanya kazi kwa njia ya vikao rasmi, katibu peke yake hana mamlaka ya kutoa maamuzi yoyote. Kwa hiyo nitawasilisha barua yenu kwa wajumbe wa baraza, ili kupata maelekezo yao juu ya nini kifanyike.

“Lakini wakati tunasubiri, naweza kutoa majibu ya awali, yakiwa ni ya kukumbushana mambo ya msingi ambayo yanapaswa kuzingatiwa, ambayo mimi na ninyi tulisimamia utekelezaji wake, wakati tulipokuwa madarakani kama viongozi wakuu wa chama,” alisema Msekwa.

HOJA ZA MSINGI

Msekwa alisema CCM imekipangia kila kikao cha chama kazi za kufanya na kazi za baraza hilo zimetajwa na kuainishwa katika Ibara ya 127 (3) ya Katiba ya CCM, toleo la 2012, kuwa ni kutoa ushauri kwa chama na kwa Serikali zinazoongozwa na chama hicho.

“Lakini kazi zile za kuangalia mwenendo wa wanachama na viongozi wake na kuchukua hatua stahiki pale inapobidi, zimepangiwa vikao vingine vya chama ambavyo ni vya utendaji kama ilivyoainishwa katika ibara zinazohusu vikao hivyo.

“Maana yake ni kwamba kikatiba, baraza halikupewa mamlaka au ‘jurisdiction’ ya kutenda kazi hizo, ambazo ni za ki-uendeshaji. Badala yake, jukumu hilo limetolewa kwa vikao vingine ambavyo ni vya viongozi walioko madarakani,” alisema.

Hoja nyingine kwa mujibu wa Msekwa inahusu umuhimu wa kuzingatia miiko ya utoaji ushauri ambayo ndiyo kazi mahsusi ya baraza hilo.

“Ushauri huombwa kamwe hauwezi kushinikizwa kwa mshauriwa au kutolewa kwake kama amri, ndiyo kusema kwamba ushauri hauwezi kutolewa pale ambapo hauhitajiki. Na mwenye kuamua kuwapo kwa hitaji hilo ni yule anayehitaji kupata ushauri, siyo yule anayetaka kutoa ushauri,” alisema.

Hata hivyo alisema pale ushauri unapotolewa unaweza ama kukubaliwa au kukataliwa na unapokubaliwa thamani yake inakuwa ni kubwa kwa maana ya kuondoa tatizo lililokuwapo.

Alisema pale ushauri unapokataliwa thamani yake inakuwa ni sifuri kwa maana ya kutatua tatizo lililopo.

Katika hoja yake ya tatu, Msekwa alisema jukumu la mtu yeyote aliyetuhumiwa la kusafisha jina lake ni la mtuhumiwa mwenyewe na kiutaratibu si sahihi kujaribu kukwepa jukumu hilo na kujaribu kulihamishia kwa watu wengine.

“Barua yenu imeeleza kwamba “mlitafakari suala la kujitokeza hadharani ili kutoa yaliyo moyoni mwenu katika kujibu uwongo wake, kusafisha majina yetu,
heshima yenu, na rekodi nzuri ya utumishi wenu, lakini mkaona kuwa ni vyema kwanza mkawasilisha malalamiko yenu kwenye Baraza la Ushauri la Viongozi Wakuu Wastaafu wa CCM, ili jambo hili lishughulikiwe”.

“Sasa ki-utaratibu, siyo sahihi kujaribu kukwepa jukumu hilo la watuhumiwa wenyewe kujisafisha kwa kukanusha tuhuma zinazowahusu na kujaribu kulihamishia jukumu hilo kwa watu wengine.

“Hii ni kwa sababu watuhumiwa wenyewe ndio wanaojua ukweli kuhusu tuhuma hizo, na kama kweli hazina msingi, ni wajibu wao kufichua ukweli wanaoujua.

“Umuhimu wa jambo hili unatokana na kuwapo kwa dhana inayosema kwamba “silence means consent”; ambayo maana yake ni kwamba ‘ukinyamaza kimya
bila kukanusha tuhuma zilizoelekezwa kwako, ukimya wako huo unachukuliwa kwamba umekiri ukweli wa tuhuma hizo’.

“Nafurahi na kuwapongeza, kwamba tayari mmetekeleza wajibu huo kupitia vyombo vya habari. Msiruhusu machungu ya tuhuma hizo yakawasahaulisha misingi hii, mkashawisika ‘kutafuta njia za mkato’ za kuyashughulikia, ambazo kumbe zinakiuka katiba ya chama chetu.

“Naomba ieleweke kwamba madhumuni ya kukumbushana juu ya mambo haya ya msingi, ni kuonesha tu ugumu uliopo wa kikatiba, kwa Baraza la Ushauri la Viongozi Wakuu Wastaafu wa CCM kushughulikia malalamiko yenu, kama mlivyoomba.

“Ugumu huo unatokana na kuzingatia kuwa katiba ya chama haikutoa jukumu la kufanya kazi za kiuendeshaji kama hii ya kusikiliza malalamiko yenu. Lakini baraza letu pia halikupewa mamlaka ya kusikiliza rufani zinazotolewa dhidi ya chama kama hii ya kwenu.

“Ni muhimu vile vile, kuzingatia kwamba Baraza la Viongozi Wakuu Wastaafu wa CCM, ni chombo maalum cha chama hicho, kilichoundwa na kupewa kazi
maalum, iliyotajwa katika Katiba ya chama.

“Baraza hili siyo kundi lolote tu la “wazee wa Chama” kama yalivyo yale “mabaraza ya wazee” mengine, yaliyotajwa katika ibara ya 128 ya katiba ya chama, ambayo wajumbe wake wanatajwa kuwa ni wazee wote wana CCM, wenye umri kuanzia miaka 60, ambao kwa kuwa hawakupangiwa jukumu lolote maalum, wanadhaniwa kuwa wanaweza kushiriki tu katika utekelezaji wa shughuli zozote za chama kwa kutumia busara za uzee wao, kama watakavyoona wao kuwa inafaa.

“Nahitimisha kwa kurudia kusema, kwamba haya ni majibu ya wali tu. Nawajibika kusubiri maelekezo ya wajumbe wa Baraza.”

MAKAMB

Alipoulizwa na MTANZANIA kama wamepata majibu ya baraza hilo Makamba alisema hawajapata.

“Tumekwishatoa maelezo yetu kama kuna barua ya Msekwa sisi hatujaipata, tukiandikiwa sisi tukiipata kama tuna cha kusema tutawaambia,” alisema Makamba.

MTANZANIA ilivyomweleza Msekwa kwamba wastaafu hao wanasema hawajapata barua hiyo, alisema “Tuachie tuwasiliane wenyewe, hayo ni mawasiliano.”

Awali Kinana na Makamba waliwasilisha maombi kwenye baraza hilo wakitaka wajumbe watumie busara zao kushughulikia jambo hilo ambalo linaelekea kuhatarisha umoja, mshikamano na utulivu ndani ya chama.

Walisema shutuma zinazotolewa dhidi yao hazina ukweli na kwamba zimeandaliwa kwa lengo la kuwadhalilisha, kuwavunjia heshima, kuwajengea chuki na kuwachafulia majina ndani na nje ya chama.

Viongozi hao walisema waliamini anapojitokeza mtu kuwadhalilisha viongozi waandamizi wastaafu hatua zitachukuliwa na taarifa kutolewa kwa umma lakini hakuna hatua zozote zilizochukuliwa kuhusu jambo hilo.

“Mara kadhaa ametutuhumu sisi wawili, makatibu wakuu wastaafu wa CCM kwa mambo ya uzushi na uongo. Mara ya kwanza alisema tunamkwamisha rais kutekeleza majukumu yake.

“Tuliyapuuza maneno haya kwa imani kwamba viongozi wetu watayaona kwa namna yalivyo kuwa haiwezekani tushiriki kuihujumu serikali ya chama tulichokitumikia maisha yetu yote. Haiingii akilini wastaafu wawili walio majumbani kwao eti wana uwezo wa kumzuia rais kutekeleza majukumu yake.

“Tumeamua kutokwenda mahakamani kwa sababu unapochafuliwa unachokwenda kudai mahakamani ni fidia, kwetu sisi heshima yetu haiwezi kuthaminishwa na fidia,” walisema katika barua yao waliyomuandikia Msekwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles