BENJAMIN MASESE-MWANZA
SERIKALI imesema sera iliyopo ya sekta ya kilimo inayotumika sasa, ndiyo cha chanzo cha wakulima kuwa masikini kutokana na kuwatumikisha wananchi kuilisha nchi na matajiri, huku wakiwa wanakabiliwa na changamoto kubwa.
Kutokana na hali hiyo, imesema sera imepitwa na wakati ambapo wizara imelazimika kuanza kuipitia upya na kuondoa changamoto na vikwazo kwa wakulima.
Kauli hiyo imetolewa jana na Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe wakati akifungua sherehe za wakulima na maonyesho ya kilimo (Nanenane) katika viwanja vya Nyamhongolo mkoani Mwanza.
Aliwapiga marufuku wakuu wa wilaya na mikoa kuwazuia wakulima kuuza chakula chao kwa kuhofia uwepo wa njaa.
Alisema kila mkulima, anajua namna anavyotunza na kuilisha familia yake hivyo kama kuna kiongozi anahofia uwepo wa njaa ni vema akanunua mazao hayo kwa bei anayotaka mkulima na kuyatunza ili yaweze kusubiria dhana aliyoiweka kichwani kwake, kwamba kutakuwapo na uhaba wa chakula.
“Hatuwezi kujenga viwanda wakati wakulima ni masikini wa kutupwa, lazima tuwawezeshe kwa kutengeneza mazingira ya watu kunufaika na kilimo chao sambamba na kuwa na soko la uhakika, ndio maana leo hii kama wizara tumeanza kupitia sera ya kilimo na kuondoa changamoto na vikwazo vilivyokwekwa .
“Sera iliyopo imepitwa na wakati kabisa, inawaumiza wakulima na kuwafanya kubaki kila mwaka kuilisha nchi na matajiri huku wao wakibaki na umasikini wao huku kukiwapo na utitiri wa taasisi nyingi ambazo ukichunguza zimeanzishwa kwa lengo la kuwakandamiza, hii haiwezekani kama wizara tumeanza kuangalia ni taasisi gani zinatakiwa kufutwa na kubaki chache.
“Fedha ambazo zilikuwa zikielekezwa kwenye utitiri wa taasisi hizo, zitaelekezwa katika mfuko maalum ambo wizara tunatarajia kuanzisha na kazi ya mfuko huo ni kufidia mkulima pale inapotokea mtikisiko wa bei katika soko la dunia, kama serikali hatuna uwezo wa kuthibiti bei ya soko la dunia, mfuko huo ndio utakaokuwa na kazi ya kutafuta fedha kwa ajili ya kuwafikia wakulima,”alisema.
Alisema Serikali ilikuwa ikipokea fedha nyingi kutoka mataifa ya nje ili kuendeleza kilimo, lakini zilikuwa zikishia katika semina mafunzo kwa watendaji, huku asilimia 50 ya fedha zilizokuwa zikipokelewa ndizo zinafika kwa wakulima.
Alisema alitoa mfano, mtikisiko uliotokea katika pamba na korosho mwaka huu, kama Serikali isingechukua hatua ya kuzungumza na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kutoa fedha za kununulia pamba, basi wangeuza kilo moja kati ya Sh 500- 700 kulingana na bei ya soko la dunia.
Alisema tayari vikao kati ya Serikali na BoT vya kutoa fedha za pamba vimekamilisha juzi na kuanzia leo Jumatatu fedha zitaanza kutolewa katika benki zingine kwa ajili ya kulipa wakulima wa pamba ambapo tayari bei elekezi ni Sh 1,200 kwa kilo moja.
“Ichukulieni hali hali ya usafirishaji wa pamba kutoka mikononi mwa wakulima kama dharula maana mvua ikianza kunyesha zao hilo likiwa bado lipo majumbamni ni hasara, niwaambie baada ya kupitisha sera mpya na kuunda mfuko wa fidia kwa wakulima, hakika suala kama lililojitokeza katika korosho na pamba litakuwa historian a halitajitokeza maana Serikali tumejipanga kuchukua hatua.
“Mbali ya mfuko wa fidia, kama wizara tumebaini kuwapo na kasoro kadhaa katika bodi ya pamba hivyo kama Serikali tunaigiza bodi ya pamba kuanza mchakato wa kuainisha mahitaji yote ya wakulima kisha tutakuja na mfuko fulani wa uagizaji pembajeo kwa pamoja, lengo ni kupunguza hasara kwa mkulima,”alisema.
Wakati huo huo, Bashe aliwaagiza wakuu wa wilaya, mikoa na watendaji wengine wanaohusika na sekta ya kilimo kuhakikisha mwaka huu wakulima hawapandi pamba kwa kumwaga mbegu, ispokuwa kwa kutumia kamba ikiwa lengo ni kulima kisasa na kupata mavuno mengi.