26.4 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

Bashe aeleza mkakati wa Serikali kulinda kilimo

Mwandishi wetu -Dar es salaam

NAIBU Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, amesema Serikali imejipanga kulinda sekta ya kilimo kwa kuhakikisha inatafuta masoko ya uhakika ili kukuza uchumi wa nchi.

Pamoja na hilo amesema uamuzi wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) na NMB kutoa Sh bilioni 9.5 kwa wakulima wa korosho ili waweze kununua pembejeo, ni sehemu ya mkakati wa kuhakikisha mkulima anainuliwa.

Amesema kupitia mkopo huo, wakulima 2,997 watanufaika moja kwa moja na fedha hizo hazitapita vyama vya msingi (Amcos).

Hayo aliyasema jana Dar es Salaam, wakati wa makubaliano ya utolewaji fedha hizo.

Bashe alisema sekta ya kilimo imebeba Watanzania asilimia 60 hadi 70, hivyo inapaswa kuwekewa mazingira rafiki wakati wote, ikiwamo kumnufaisha mkulima wa chini.

“Kama mnavyofahamu uchumi wetu, zaidi ya Watanzania asilimia 60 hadi 70 wapo katika sekta ya kilimo na sekta hii imekuwa ikikumbwa na matatizo mengi sana kwa sababu ya namna ilivyo.

“Moja ya tatizo kubwa ni uhakika wa soko, na upande mwingine ni suala la fedha kwa maana namna gani mkulima anaweza kukopesheka na kupata fedha, hivyo kama Serikali tumefanya mpango maalumu kupitia Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania.

“TADB ndiyo benki ambayo itamkopesha mkulima, lakini haina uwezo wa kufika kule kijijini, hivyo anakuwa Vehicle, ana-guarantee benki za biashara kwa sababu kuna benki za maendeleo na benki za biashara,” alisema Bashe.

Alisema ili benki za biashara ziweze kumkopesha mkulima, zinahitaji mtu atakayebeba baadhi ya mahitaji ya msingi ya mtu ambaye anapewa dhamana ya kukopeshwa.

“Nitumie nafasi hii kuipongeza Benki ya NMB na benki nyingine kwa kuwa katika huu mpango, ambapo wameza kuwakopesha wakulima wa korosho.

“Mnafahamu kilichotokea katika korosho, hasa baada ya uamuzi wa Serikali kuamua kununua korosho yote kwa bei ambayo itamlinda mkulima.

“Kabla korosho haijauzwa kuna ambao walikuwa hawajapata fedha kwa ajili ya kununua pembejeo za kilimo.

“Ni zao ambalo tunatarajia kuanza kulipata kuanzia mwezi ujao (wa 10), kutokana na hali hiyo TADB imeamua ku-gurantee mkopo huu kwa asilimia 50 ili NMB aweze kuwakopesha wakulima.

“Kwa hiyo kama mkulima akikopeshwa Sh 100 basi Sh 50 imebebwa na Serikali kupitia Benki ya Kilimo Tanzania,” alisema.

Bashe alisema linafanyika hilo ili kumlinda mkulima wa korosho na jambo kama hilo tayari limefanywa na kwenye zao la kahawa.

“Na safari hii tumekuwa na mtikisiko kwenye zao la pamba na tumejadiliana pia na TADB pamoja na NMB, tunatengeneza utaratibu ambao benki hizi za kibiashara zitakuja pamoja kumkopesha mkulima pale linapotokea tatizo kwenye soko.

“Kwa hiyo mimi niwashukuru kwa hili suala, NMB peke yake wameweka Sh bilioni 95.5 ambazo asilimia 50 zimebebwa na TADB, na vizuri tunapozungumzia kwamba asilimia 70 ya Watanzania kuwapo kwenye sekta ya kilimo.

“Ili uchumi wetu uweze kukua ni lazima sekta hii iwe na ‘stability’ (utulivu), inatokana na mambo matatu ambazo ni gharama za uzalishaji, upataji wa fedha na uhakika wa masoko,” alisema,

Bashe alisema mambo hayo yanatakiwa kupewa kipaumbele ili kuweza kufikia kupata matokeo chanya.

“Ukiangalia kwa sasa mwenendo wa uchumi wetu kwa ujumla, ‘total portifolio’ ya mikopo katika uchumi wetu ni karibu trilioni 16. Kati ya hizo ni asilimia 8 tu ndio inakwenda kwenye sekta ya kilimo wakati sekta hii inachangia asilimia 20 ya pato la taifa, karibu dola bilioni 56.

“Sasa kama hatutoongeza uwezekano wa uwekezaji kwenye ngazi ya msingi na kati, maana yake wakulima wetu bado watabaki kwenye dimbwi la umaskini.

“Kwa hiyo Serikali tumekuwa tukifanya juhudi mbalimbali kwa kuwekeza TADB kama taasisi ambayo inaweza kuwapunguzia hatari benki za biashara katika kupeleka katika sekta ya kilimo.

“Ninawashukuru sana mkurugenzi wa NMB na TADB na ninaziomba na taasisi zingine za fedha zitambue kwamba skimu ya ‘gurantee’ katika sekta ya kilimo vehicle tunayoitumia sisi kama Serikali ni Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania,” alisema.

Aliwaomba wakurugenzi wa TADB na NMB kama wameweza kupunguza riba kutoka asilimia 18 hadi 17, ni vema mwakani ifike asilimia 15 hadi 10 kwa sababu hatari zinaendelea kupungua.

MTIKISIKO SEKTA YA PAMBA

Akizungumzia mtikisiko katika sekta ya pamba, Bashe alisema kuwa zao hilo lilipata mtikisiko na hata baadhi ya watu kufikia kutumia mitandao ya kijamii kuilaumu Serikali kwa kutonunua pamba.

“Wanaonunua pamba za wakulima ni wafanyabiashara, mpaka sasa benki zetu kama NMB zimeendelea kusapoti sekta binafsi katika kununua pamba.

“Taasisi za fedha zije na ‘product’ (bidhaa) kwa ajili ya kununua pamba zaidi, kwa sasa uzalishaji umeongezeka zaidi ya tani 100,000 na tunatarajia mwakani kufika tani 350,000 hadi 400,000 ni karibu mara mbili,” alisema.

Alisema hadi sasa pamba iliyopo kwenye vyama vya msingi (Amcos) ni karibu tani 70,000 ukiachia zile zilizopo majumbani, ambapo kwa msimu huu Watanzania wamezalisha pamba nyingi kuliko uwezo wa kampuni zinazonunua.

Bashe alisema mzozo wa nchi za Marekani na China umechangia kwa kiasi kikubwa kukwama kwa zao hilo kwenye soko la dunia.

Awali Kaimu Mkurugenzi wa NMB, Filbert Mponzi, alisema wamechukua uamuzi huo ili kulinda mnyororo wa thamani ya mazao kutoka kwa mkulima.

Mkurugenzi wa TADB, Japhet Justine, alisema kwa sasa Serikali kupitia benki hiyo imedhamiria kumlinda mkulima ili aweze kunufaika na kilimo kama injini kwa uchumi wa nchi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles