Anna Potinus
Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amesema Wizara yake inapitia mfumo mzima wa usambazaji wa pembejeo za mazao ili kuondoa ucheleweshwaji na wizi unaoendelea katika usambazaji wa pembejeo.
Bashe ametoa kauli hiyo bungeni leo, alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Cecilia Pareso (Chadema) aliyetaka kujua nini mkakati wa serikali katika kuhakikisha usambazaji wa mbolea unafanyika kwa wakati ili ardhi ambazo zimekosa rutuba ziweze kupata rutuba.
Akijibu swali hilo Bashe amesema Wizara ya Kilimo inachukua hatua ya kufanya mabadiliko katika Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC), ili matatizo hayo yasijirudie.
“Ninakiri kwamba kuna mapungufu katika baadhi ya maeneo kwenye usambazaji wa mbolea na wizara sasa inachukua hatua ya kufanya mabadiliko katika taasisi yetu ya TFC ili matatizo hayo yasiweze kujirudia.
“Kama Wizara tunapitia mfumo mzima wa usambazaji wa pembejeo za mazao ili kuondoa ucheleweshwaji na wizi unaoendelea katika usambazaji wa pembejeo ambao siku ya mwisho anaenda kubeba mkulima kwa hiyo mchakato huu unaendelea na tunaamini msimu huu wa kilimo mambo mengi yatabadilika katika usambazaji wa pembejeo,” amesema Bashe.