25.5 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 18, 2024

Contact us: [email protected]

BARCELONA WATAWEZA KUISHANGAZA DUNIA WIKI HII?

BADI MCHOMOLO NA MITANDAO


WIKI nyingine tena kwenye ulimwengu wa soka kushuhudia miamba barani Ulaya ikishuka dimbani na kuoneshana ubabe na maajabu katika michuano ya klabu bingwa hatua ya 16 bora kwa michezo ya marudiano.

Wiki mbili zilizopita tulishuhudia wababe wakioneshana uwezo katika soka Ulaya huku mabingwa watetezi, Real Madrid wakiwa kwenye uwanja wa nyumbani wa Santiago Bernabeu na kuwachezesha kichapo wapinzani wao Napoli mabao 3-1, wakati huo Bayern Munich wakitakata kwenye uwanja wa nyumbani kwa mabao 5-1 dhidi ya Arsenal.

Mchezo mwingine ambao uliteka hisia za watu wengi ni ule wa miamba ya nchini Ufaransa, PSG walipowashushia kichapo mabingwa wa Ligi Kuu nchini Hispania, Barcelona kwa mabao 4-0.

Kichapo hicho cha Barcelona kilizungumziwa sana kwenye vyombo mbalimbali vya habari kuwa ni kitakatifu na kitawapa wakati mgumu kurudisha.

Wiki hii ni michezo ya kisasi, inawezekana tukayaona makubwa zaidi ya michezo ile ya awali au mambo yakawa vile vile waliotangulia wakafika moja kwa moja hatua inayofuata.

Ili Barcelona iweze kushinda mchezo huo, wanatakiwa kupata mabao mawili ya haraka ndani ya dakika 15 za mwanzo, inawezekana kutokana na safu bora ya ushambuliaji ambayo inaongozwa na Lionel Messi, Luis Suarez na Neymar.

Barcelona vs PSG

Huu ni mchezo ambao unatarajiwa kuangaliwa na idadi kubwa ya wapenzi wa soka duniani kote ukipigwa kwenye Uwanja wa Nou Camp ambao unachukua jumla ya watazamaji 99,354.

Wapo ambao wanaamini kuwa Barcelona wanaweza kushinda mchezo huo lakini wasifuzu kuingia hatua ya robo fainali kwa kuwa walifungwa mabao mengi kwenye mchezo wao wa awali.

Wapo pia ambao wanaamini kuwa Barcelona ni miongoni mwa klabu ambayo inaweza kuishangaza dunia kwa kufuzu hatua inayofuata huku ikihitaji ushindi wa mabao 5-0 ili iweze kufuzu moja kwa moja au 4-0 ili waende kwenye matuta, jambo ambalo linaonekana kuwa gumu sana.

Kwenye soka yote yanawezekana na baadhi ya wachezaji wa Barcelona wanaamini hilo linaweza kutokea wiki hii.

Kiungo wa klabu hiyo, Andres Iniesta na Luis Suarez, wamedai kuwa wana nafasi kubwa ya kuonesha maajabu kwenye mchezo huo na kufuzu, wakati huo mchezaji wa zamani wa klabu hiyo, Dani Alves ambaye kwa sasa anakipiga katika klabu ya Juventus, amesema Barcelona ni klabu pekee ambayo inaweza kushangaza ulimwengu, hivyo ana imani na mchezo huo inaweza kusonga mbele. Mchezo huo unatarajiwa kupigwa Jumatano.

Arsenal vs Bayern Munich

Kwenye uwanja wa Emirates wenyeji Arsenal watakuwa na kibarua kigumu dhidi ya miamba ya nchini Ujerumani, Bayern Munich ambao kwenye mchezo wa awali uliopigwa kwenye uwanja wa Allianz Arena, Arsenal walichezea kichapo cha mabao 5-1.

Mara kwa mara Arsenal wamekuwa wakitolewa na miamba hiyo katika hatua ya 16 bora kwa misimu miwili mfululizo, hivyo wengi wanaamini hata mchezo huu ambao utapigwa kesho itakuwa ni safari ya mwisho kwa Arsenal.

Wapo mashabiki wa Arsenal ambao wanaamini chochote kinaweza kutokea na kuwafurahisha japokuwa ni wachache wenye imani hiyo, huku wengine wakiamini kuwa wanaweza kushinda lakini wasisonge hatua inayofuata.

Arsenal wanahitaji mabao 4-0 ambapo yatawafanya kuwa sawa 5-5, lakini litakuwa limewabeba bao la ugenini lakini wanatakiwa wasiwaruhusu wapinzani wao kupata bao.

Ni kweli inaweza kuwa ni safari ya mwisho kwa Arsenal kusonga mbele kutokana na deni kubwa la mabao walilonalo.

Napoli vs Real Madrid

Kwenye uwanja wa Stadio San Paolo, Real Madrid hawana kazi kubwa sana ya kuhakikisha wanasonga mbele, wanahitaji ushindi wa aina yoyote au sare ya aina yoyote lakini wasifungwe mabao zaidi ya 2-0 ambayo yatawafanya Napoli wasonge mbele hatua inayofuata.

Napoli pia wanaweza kuonesha maajabu na kusonga mbele endapo watahakikisha wanashinda mabao zaidi ya mawili na kuwazuia mabingwa watetezi wasipate bao.

Jambo hilo linawezekana kwa kuwa baadhi ya michezo ya Real Madrid wiki mbili zilizopita wamecheza chini ya kiwango na kupata ushindi mwembamba katika Ligi Kuu, hivyo Napoli kazi ni kwao kutumia uwanja wa nyumbani.

Dortmund vs Benfica

Katika mchezo wa awali, Benfica walikuwa kwenye uwanja wa nyumbani na kuwafurahisha mashabiki wake kwa ushindi mwembamba wa bao 1-0.

Kazi yao kubwa katika mchezo wa kesho kutwa ni kuhakikisha wanawazuia wapinzani wao wasipate bao, hivyo watahakikisha wizara ya ulinzi imekamilika kuwazuia wapinzani wao.

Haitakuwa rahisi kwa Borussia Dortmund kukubali kupoteza mchezo huo kama ilivyo ule wa awali, hivyo watahakikisha wanapata ushindi mbele ya mashabiki wake ambao wana imani na timu yao na watajitokeza kwa wingi kuipa nguvu timu hiyo.

Mshambuliaji wa Dortmund, Pierre Aubameyang, ambaye ni kinara wa ufungaji wa mabao katika msimamo wa ligi nchini Ujerumani akiwa na jumla ya mabao 19 sawa na mshambuliaji wa Bayern Munich, Robert Lewandowski, hakuwa fiti sana kwenye mchezo wa awali alidaiwa kuchoka mara baada ya kutoka kwenye michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon).

Lakini kwenye mchezo huo ujao, mshambuliaji huyo anataka kuisaidia klabu yake na kuwapa furaha mashabiki ambao watajitokeza kwenye uwanja huo.

Wengi wanawapa nafasi Dortmund kuweza kusonga mbele, japokuwa mchezo huo unaonekana utakuwa mgumu na ushindani wa hali ya juu, ila chochote kinaweza kutokea, hivyo wiki hii itakuwa ya vita ya kisasi na ushindani wa soka.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles