Na, HUSSEIN JUMA, SHINYANGA
WATANZANIA tumeshudia Baraza jipya la Mawaziri lililotangazwa mwishoni mwa juma lililopita. Jumatatu ya oKTOBA 9, 2017, tumeona Mawaziri na Manaibu Waziri wakiapishwa kwa mujibu wa sheria.
Vile vile tumeona wizara mbili kuongezeka na hivyo kufanya ongezeko la Manaibu Waziri wapya wapatao watano. Sanjari na hilo, tumeona pia tanguo la baadhi ya Mawaziri, kuhamishwa kwa baadhi ya Mawaziri kutoka wizara moja hadi nyingine na hata kupandishwa baadhi ya Manaibu Waziri na kuwa Mawaziri kamili.
Kwa kawaida, matangazo ya Baraza la Mawaziri na kufanya Baraza jipya, kwa namna moja ama nyingine mtakubaliana na mimi, ni matokeo ya kikao cha Kamati Kuu ya CCM kilichoanza Septemba 27, 2017 kwenye kumbi za Ikulu jijini Dar es Salaam. Sasa wachambuzi wengi wamezungumza mengi; Baraza jipya litakuja na mapya hasa katika kipindi hiki cha Vita ya Uchumi hasa katika kulinda rasilimali za Taifa, kubana matumizi, kupambana na ufisadi, kuwatumikia wananchi hasa wanyonge na kuinua uchumi wa Taifa.
Binafsi najaribu kujiuliza, Baraza jipya la Mawaziri, Moto wa wimbombo na ulindi? Je, ni moto ambao kweli utasaidia jamii hasa katika maendeleo anuai ya kiuchumi na kijamii? Au ni moto utokanao na wimbo wimbo na ulindi ambao kwa sasa umebaki kwa waganga wa kienyeji, ukiachilia mbali makumbusho, kama namna ya kuwahadaa wenye shida na matatizo; moto ambao mganga kwa sasa huutumia kuhadaa wateja akiongezea na maneno (abracadabra) ayajuayo peke yake?
Historia iturudishe nyuma kidogo. Februari 7 hadi 12, 1990, Kamati Kuu ya CCM ilikaa Mjini Dodoma chini ya uenyekiti wa Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Kikao hicho kilitokana na baada ya kudaiwa kuwapo harufu ya rushwa kuenea kwenye uongozi wa Mzee Ali Hassan Mwinyi; rushwa ambayo ilionekana kukwamisha maendeleo na demokrasia kwa kipindi kile.
Kwenye kikao kile, inasemekana alisimama mjumbe mmoja na kusema kuwa, mawaziri, wakuu wa mikoa na wilaya pamoja na wajumbe wa Sekretarieti wajiuzulu ili kuwapa fursa Rais (Mzee Mwinyi) na Mwenyekiti wa chama (Mwalimu. Nyerere) wateue wengine.
Machi 12, 1990, Rais Mwinyi aliwaita kwa pamoja Waziri wa Mambo ya Ndani, Meja Jenerali Kimario, Waziri wa Afya, Aron Chiduo na Waziri wa Sheria, Damian Lubuva; Wizara ambazo zilikuwa zimeathirika vibaya na rushwa, ili kufika kwenye Kamati Kuu waelezi hali hiyo na vipi walikuwa wamejipanga kupambana na hali hiyo. Kwa kuwa walikuwa wamemzoea Mzee Mwinyi kama ‘Mzee wa ruksa’ asiye na makuu, walifika Kamati Kuu ki ruksa. Siku hiyo, Rais Mwinyi hata hakuwa na hotuba ndefu na pengine tayari walikuwa wameshajadili na Mwenyekiti wa chama.
Baada ya siku tatu, Baraza jipya liltangazwa mnamo Machi 15, 1990. Baraza hilo liliwatema mawaziri wanne; aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini Al-Noor Kassum, aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Mawasiliano na Utalii, Arcado Ntagazwa, aliyekuwa Waziri wa Maji, Christina Kisangi na aliyekuwa Waziri asiye na Wizara Maalumu, Getrude Mongella. Badala yake, Baraza hilo lilikuja na sura mpya tatu ndani yake; Nalaila Kiula kama Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kabeho kama Waziri wa Afya na Marcel Komanya kama Waziri wa Ardhi.
Baraza hilo lilileta matarajio mapya kabisa ya kiutendaji hasa katika kuziba mianya iliyokuwa imetengenezwa na mawaziri wachache wasiokuwa waaminifu. Kama vile Dk. Magufuli alivyofanya baraza jipya, Mzee Mwinyi pia alihamisha mawaziri kadhaa katika wizara zao na kuwapeleka wizara zingine kama Cleopa Msuya aliyetolewa kwenye Wizara ya Fedha na kupelekwa Wizara ya Biashara na Viwanda. Baadhi ya matatizo ambayo yalitarajiwa kuondoshwa ilikuwa ni pamoja na matatizo ya kiuchumi, uwajibikaji duni na rushwa.
Kimsingi hakuna kipya kilichotokea kwenye baraza lile ambalo liliwapa matumaini makubwa Rais na Mwenyekiti wa chama na badala yake matatizo yaliyotarajiwa kuondoshwa, yalizidi kushamiri na hatimaye kumkatisha tamaa kabisa Baba wa Taifa, na siku chache baadaye akanukuliwa akisema;
‘…chama kinapotelekeza madhumuni ya kuwepo kwake, hicho si chama tena, bali ni gofu la kufichia wevi wachache dhidi ya wengi na kuwa kero kubwa kwa jamii; na inakuwa hivyo, mimi si mwenzenu tena; wala chama si mama yangu, mama yangu yupo kule Butiama…’
Kauli hii ilimuonesha Baba wa Taifa kuchukizwa sana na washukuriwe sana washauri wake Joan Wickens na baadaye , Joseph Butiku kwa kuwa walimshauri kwa weledi mkubwa sana.
Sasa tukiangalia kwa kawaida Baraza jipya lililotangazwa na tayari limeshaapishwa, lina mambo mengi sana ya kuyatazama aidha kwa jicho la kisiasa ama jicho la kiuchumi.
Kwa jicho la kiuchumi, wengi wameshaanza kutoa maoni yao mbalimbali wengine wakijiuliza sasa inakuwaje kuongeza idadi ya Mawazri na Manaibu Waziri kutoka 32 baraza la awali hadi kufikia 41 baraza hili jipya wakati tupo katika kipindi kigumu cha kubana matumizi. Mawaziri na Manaibu Waziri wapatao tisa walioongezeka watahitaji mishahara, majumba, magari, ofisi zenye wasaidizi nakadhalika.
Kufuatia Baraza hili kutangazwa, baada ya siku chache za kikao cha Kamati Kuu, wengine wameenda mbali zaidi na kuliangalia baraza hili kisiasa kwa kuangalia hasa baadhi ya mawaziri kuenguliwa kama Prof. Maghembe na hata baadhi ya mawaziri kuhamishiwa wizara zingine kama, Angella Kairuki kuhamishiwa Wizara mpya ya Madini. Lakini si hivyo tu, bali hata sura mpya zilizojitokeza kwenye baraza jipya zimezua hisia anuai kwenye mijadala. Wengine wanaangalia utendaji wao kuonekana kumkuna si tu Rais, bali pia umma wa Watanzania. Wengine wanalijadli suala hili kama mwendelezo wa chuki dhidi ya makundi yaliyojionesha kipindi cha kampeni…kimsingi kila mtu analiangalia Baraza jipya kwa kadri anavyojaaliwa kufikiria.
Binafsi, kando na masuala mengine, naliangalia zaidi baraza jipya katika nadharia ya kiutendaji. Kiutendaji kwa kuzingatia hasa uongozi ni nini na kiongozi anatakiwa kuwa na sifa zipi.
Kwa tafsiri nyepesi kabisa, Uongozi ni mamlaka au karama ya kuonesha njia kwa vitendo. Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali, sifa kuu anazotakiwa kuwa nazo kiongozi ni pamoja na (i) awe na ufahamu (ii) awe mwaminifu (iii) mwenye maadili mema (iv) amche Mungu (v) mwenye kukubalika na watu anaowaongoza na; (vi) mwenye kuongoza watu katika misingi bora ya uongozi bila kujali jinsia, rangi, udini wala ukabila.
Prof. Issa Shivji anaeleza sifa za kiongozi bora ni yule ambaye (i) hushawishi kuliko kuwashambulia wananchi wake (ii) huwaeleza kuliko kuwabeza wananchi wake (iii) huvumilia kuliko kuwavurumisha wananchi wake na (iv) huamsha nia na kuonesha njia wananchi wake.
Mwalimu Nyerere, kwa kutambua sifa zote hizi za uongozi, alihakikisha kila Waziri au Naibu Waziri anakisoma vyema na kukielewa kitabu cha Rene Dumont, False Start in Africa mara baada tu ya kuapa. Lengo kuu la kufanya vile lilikuwa ni kuhakikisha kila Waziri au Naibu Waziri anajua vyema mizizi ya umaskini Afrika na vihunzi mbele katika kufikia maendeleo ya kweli.
Sina shaka na vigezo ambavyo Rais Magufuli alivyovitumia katika kuunda Baraza jipya, lakini shaka yangu ni kwamba, Je, mawaziri hawa wanajua kweli kwa nini Watanzania ni maskini? Je, wanajua vikwazo katika kuwafikisha salama wananchi sehemu panapotakiwa? Lakini Je, wanayo dira na dhamira halisi ya Awamu ya Tano?
Wapembuzi wa mambo wamekuwa wakijaribu kujiuliza, hivi nini hasa dira ya nchi kwa sasa?
Tumeshuhudia Wizara ya Nishati na Madini kwa mfano, Wizara ambayo kwa sasa imezaa wizara mpya na kufanya wizara mbili tofauti baada ya kukaa muda mrefu bila Waziri. Tuna kesi ya ulinzi wa rasilimali za Taifa na kwa nia njema kabisa Rais kashikilia mchanga wa madini ya dhahabu (makinikia ya dhahabu) na amehakikisha almasi haisafiri kiholela kadhalika na sasa Tanzanite. Lakini Je, Waziri mpya kapewa mamlaka halisi ya kuhakikisha anashughulika na hilo? Anajua kuwa chanzo cha matatizo hayo ni mikataba? Amejipanga vipi kuhakikisha mikataba inasahihishwa kwa manufaa ya umma wa Watanzania? Ni baadhi ya mambo ambayo endapo hayajaangaliwa kwa undani, Baraza hili litabaki kuwa Moto wa Wimbombo na Ulindi wa karne ya 21.
Wizara yenye dhamana ya masuala ya Katiba na Sheria kwa mfano, Je inayo meno ya kuhakikisha Katiba inafuatwa? Nitolee mfano. Sakata la uteuzi wa Waziri Mkuu Aprili 1984, kufuatia kifo cha aliyekuwa Waziri Mkuu kipindi hicho, Edward Moringe Sokoine, lilikuwa gumu na washukuriwe kwa kweli waliokuwa washauri wa Rais Bi. Juan Wickens na baadae, Joseph Butiku. Kabla ya Baraza jipya kutangazwa, fununu zilienea kila kona kuwa, pengine kwa hadhi ya Mzee John Samweli Malecela angeweza kuteuliwa nafasi hiyo ya Waziri Mkuu.
Ilidaiwa na wachambuzi wa siasa kwamba kilichomponza Malecela ni kauli tu. Ni kauli peke yake ilimuondolea sifa ya si Waziri Mkuu, bali hata kuwa kiongozi. Malecela akiwa Waziri wa Mawasiliano, Ujenzi na Uchukuzi aliwahi kutoka kauli kuwa, wale wanaolalamikia ufanisi duni wa reli ‘waende kuzimu’. Si tu kwamba kauli hii iliwaudhi wananchi pekee, bali hata Mzee Mwinyi na Mwalimu Nyerere waliichukia na hawakutaka kabisa kumpa nafasi hiyo. Mwalimu Nyerere alinukuliwa akisema kuwa, “…kiongozi anatakiwa kuwaeleza wananchi juu ya jambo tena na tena ili waelewe badala lya kutoa majibu ya mkato na dharau…” Hicho ndicho kilimponza Malecela na pengine kumkosesha nafasi ya Uwaziri Mkuu na badala yake Mwalimu akamteua aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje, Dk. Salim Ahmed Salim kushika nafasi hiyo.
Sasa, kwa Baraza jipya bila Katiba kufuatwa kuanzia na uongozi wa juu hadi wa chini ni sawa kabisa na kuchemsha sufuria tupu na kukaa pembeni kungojea supu. Endapo kiongozi aliye juu ya Waziri hafuati sheria, basi ni dhahiri shahiri kuwa Baraza jipya ni Moto wa Wimbombo na Ulindi wa karne ya 21 ambao kwa sasa kazi yake kubwa ni kuhadaa wananchi wenye shida waendao kwa mganga.
Watanzania tunahitaji maendeleo. Ikiwa maendeleo haya yalikwamishwa na mawaziri waliohamishwa ama kuondolewa kabisa kwenye wizara, basi ipo haja ya kuona ni namna gani baraza jipya linaweza kuwa chachu ya maendeleo hasa ya ‘Tanzania ya viwanda’ kama chama kinavyojipambanua. Ni lazima kila wizara sasa ipewe dira na dhamira ya nchi sambamba kabisa na malengo ya jumla na malengo mahususi juu ya namna sahihi ya kuifikisha Tanzania na Watanzania wanapopataka.
Vilevile ipo haja kubwa sana kuhakikisha Waziri au Naibu Waziri si tu anafuata Katiba, bali pia anakuwa na uwezo wa kuilinda na kuitetea Katiba bila kujali ni dhidi ya nani kama kiapo chao kinavyosema. Kwa kufanya hivyo, Tanzania na Watanzania hawataishia kuangalia hadaa ya moto wa Wimbombo na Ulindi, bali watajua kuwa kwa sasa moto huo hauna tena jipya, ila moto wa kiberiti.
+255 759 947 397