28.2 C
Dar es Salaam
Thursday, January 2, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Bandari bubu kuingiza Sh bilioni 35 kwa mwezi

Na NORA DAMIAN, BAGAMOYO

MAMLAKA ya Usimamizi wa Bandari (TPA), imesema kurasimishwa kwa bandari bubu zaidi ya 250 kutaiwezesha Serikali kukusanya Sh bilioni 35 kwa mwezi.

Bandari hizo zipo katika mikoa ya Pwani, Tanga, Lindi, Mtwara, Mbeya na zile za maziwa katika mikoa ya Mwanza, Kigoma na Kagera.

Akizungumza jana kuhusu utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika kipindi cha miaka mitatu, Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Deusdedit Kakoko, alisema bandari hizo zinaweza kufika 300 mara baada ya tathmini kukamilika.

“Tumeanza utaratibu wa kuzirasimisha bandari bubu zote ili kuwezesha kukusanya mapato mengi zaidi ya yale tunayokusanya Bandari ya Dar es Salaam kwa mwezi,” alisema Kakoko.

Kwa mujibu wa Kakoko, asilimia 90 hadi 95 ya biashara ya bandari inategemea Bandari ya Dar es Salaam ambayo mapato yake ni Sh bilioni 70 kwa mwezi.

Alisema bandari hizo ambazo pia zinapitisha bidhaa magendo kama dawa, vyakula na kemikali

zipo kwenye mipaka ya nchi hivyo, ni rahisi silaha na uhalifu mwingine kufanyika na kuhatarisha amani.

“Tumeanza kwanza kufanya tathimini ya kuzitambua kazi ambayo ipo mwishoni. Tumebaini bandari nyingi bubu ambazo hazitambuliki na shughuli zinazofanyika na hivyo kuikosesha mapato mamlaka,” alisema.

Mkurugenzi huyo alisema kurasimishwa kwa bandari bubu mbali ya kuongeza mapato kutaimarisha ulinzi na usalama hasa katika maeneo ya mipakani.

“Mnakumbuka walivyofanya mkoani Mwanza na Tanga ambako wahalifu walijificha kwenye mahandaki, unaweza kuona namna wanavyoweza kusababisha kutokuwa na usalama,” alisema Kakoko.

Alisema katika kazi hiyo ya kuzitafuta bandari hizo wamewashirikisha viongozi wote wa vijiji, mitaa, kata, wilaya na mikoa na kwamba itakamilika mwisho wa mwezi huu.

“Isingekuwa busara TPA twende na vyombo vya usalama kuwakurupusha watu ndio maana tumewashirikisha kwa kuwaeleza mikakati yetu kwa sababu nyingine zipo chini ya serikali ya vijiji,” alisema.

Alisema baada ya kumaliza kufanya tathimini hiyo watafanya uchambuzi na kuandaa mapendekezo kisha kuyawasilisha kwa waziri mwenye dhamana.

Alisema hadi mwishoni mwa mwaka 2019 watakuwa wamekamilisha kazi hiyo na endapo haitawezekana kumilikiwa na Serikali bandari hizo zitapangishwa kwa kijiji au kampuni ili waziendeshe.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles