Ramadhan Hassan -Dodoma
OFIS ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) imeomba bajeti ya Sh trilioni saba kwa mwaka 2020/21 huku ikijikita kuboresha mfumo wa elimu na afya.
Akiwasilisha bajeti hiyo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo, alisema Serikali imepanga hospitali mpya 27 za halmashauri katika mwaka wa fedha 2020/21.
Alisema hospitali 67 za halmashauri zinaendelea kujenga na zimetengewa Sh bilioni 32.50 kwa kazi hiyo na zitakapokamilika zitawezesha hospitali hizo kutoa huduma kwa wagonjwa.
Alieleza pia utafanyika ujenzi wa hospitali mpya 27 za halmashauri ambapo zimetengwa jumla ya Sh bilioni 27.00.
Jafo alisema zitajengwa katika halmashauri za wilaya za Karatu, Chalinze, Kondoa, Kongwa, Mbogwe, Biharamulo, Nsimbo, Kigoma, Kakonko, Liwale, Serengeti, Sengerema, Mbeya, Kilombero, Kaliua, Babati, Mvomero, Newala, Madaba, Kwimba, Msalala, Ikungi, Handeni, Mkinga, Halmashauri ya Mji wa Tunduma na Halmashauri za Manispaa za Sumbawanga na Tabora.
Alisema mpango wa uimarishaji huduma za afya ya msingi umetengewa Sh bilioni 128.91 kwa ukamilishaji wa ujenzi wa vituo vya afya, ununuzi wa vifaa tiba, ajira za watumishi wa afya kwa mkataba, kujenga uwezo wa watumishi wa sekta ya afya na usimamizi wa mradi.
ELIMU
Jafo alisema katika elimu imepanga kutekeleza kazi ya ugharamiaji wa elimu msingi bila ada na zimetengwa jumla ya Sh bilioni 298.13 kwa shule za msingi na sekondari.
Alisema kati ya fedha hizo, Sh bilioni 137.63 zitatumika kwa shule za msingi na Sh bilioni 160.49 zitatumika kwa shule za sekondari na bajeti hiyo ni sawa na ongezeko la Sh bilioni 9.6 ikilinganishwa na bajeti ya Sh bilioni 288.48 iliyoidhinishwa katika mwaka wa fedha 2019/20.