Mshambuliaji wa timu ya Yanga, Said Bahanuzi, ameendeleza kuonesha cheche zake za kurejea kwenye moto wake wa mwaka juzi, kwani jana alimuonesha cha moto kipa wa timu hiyo, Deogratius Munishi ‘Dida’.
Bahanuzi alimpigia mashuti makali Dida, ambayo alishindwa kuyadaka, huku mawili kati ya hayo yakigonga mwamba wa juu na kujaa wavuni, jambo ambalo liliamsha hisia za mashabiki wa Yanga na kumsifia.
Mashabiki hao waliokuwa wakichungulia mazoezi ya Yanga kwa nje sambamba na MTANZANIA walisema: “Huyu jamaa amerejea kwenye kiwango chake cha mwaka juzi kilichomfanya aibuke mfungaji bora wa Kombe la Kagame, kwa namna ile tutalifuta jina la ‘mshambuliaji wa Kagame’ msimu ujao.”
Bahanuzi alitungiwa jina hilo kufuatia kushindwa kuonesha cheche kwenye ligi kama alizoonesha kwenye michuano ya Kombe la Kagame, kwa kuibuka mfungaji bora mwaka juzi kiasi cha kuwekwa benchi na makocha wa zamani wa timu hiyo, Waholanzi Ernest Brandts na Hans van Pluijm.