32.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 5, 2024

Contact us: [email protected]

BAADA YA MBWA, KANGI AMPA IGP SIRRO SIKU 10 AMPELEKE LUGUMI

MKUTANO: Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana kuhusu mambo mbalimbali likiwamo swala la Lugumi. PICHA: IMANI NATHANIEL

Na AGATHA CHARLES – Dar es Salaam         |      


WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, amempa Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Simon Sirro siku 10 hadi Julai 31, kumfikisha ofisini kwake mmiliki wa Kampuni ya Lugumi Enterprises Ltd, Said Lugumi au ajisalimishe mwenyewe saa mbili asubuhi.

Agizo hili la Lugola kwa IGP Sirro ni la tatu ndani ya wiki hii baada ya Jumatano kumtaka amweleze mahali aliko mbwa Hobby ambaye aliondolewa pasipo kufuata utaratibu katika Bandari ya Dar es Salaam. Kabla ya hapo alimtaka amweleze kwanini mabasi hayasafiri usiku.

Kuhusu Lugumi ambaye aliingia mkataba na jeshi hilo wa uwekaji mashine za utambuzi wa alama za vidole katika vituo 108 vya polisi wenye thamani ya Sh bilioni 37, alisema si lazima kusubiri kufuatwa na polisi bali anaweza kufika na kugonga ofisi yake kujisalimisha.

Lugola alitoa kauli hiyo jana, Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu aliyoyabaini kwenye ziara yake aliyoianza Julai 11, mwaka huu ya kutembelea vyombo vyote vya ulinzi na usalama pamoja na idara za wizara anayoiongoza.

Alisema uamuzi huo wa kutaka Lugumi akamatwe ama ajisalimishe, aliuchukua baada ya kumpa maagizo IGP Sirro kupeleka taarifa ya kampuni hiyo kufunga vifaa, kazi ambayo ilionyesha haijakamilika.

“Taarifa nilizoletewa kazi hiyo haijakamilika. Nimemwelekeza IGP, Julai 31 saa mbili amtafute  Lugumi na kumleta ofisini mbele yangu,” alisema.

Alipoulizwa na mmoja wa waandishi iwapo Lugumi hatopatikana hatua ambazo angechukua ikizingatiwa suala hilo limeonekana kuwashinda mawaziri wawili waliotangulia, Lugola alisema mfanyabiashara huyo ni Mtanzania, hivyo isifikie hatua hiyo ya kutopatikana bali itapendeza iwapo akifika mwenyewe.

“Tusifikie huko, ni Mtanzania, asisubiri polisi. Itapendeza akija mwenyewe. Kumbuka waliopita hawakuwa maninja, sasa akija tutajua nini kitatokea. Tusubiri muda akifika yatakayojiri tutawaambia Watanzania,” alisema Lugola.

Anachokifanya sasa Lugola anatekeleza agizo la Rais Dk. John Magufuli ambaye wakati alipomwapisha, Ikulu, Dar es Salaam pamoja na mambo mengine, alimtaka kuhakikisha anashughulikia suala la Lugumi.

Siku mbili baada ya kuapishwa, Lugola alimtaka IGP Sirro kumwandalia taarifa muhimu itakayotoa mwongozo wa suala hilo.

SAKATA LA LUGUMI

Sakata la Lugumi liliibuka mwaka juzi baada ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) chini ya Makamu Mwenyekiti wake, Aeshi Hilaly kubaini utata mkubwa wa utekelezaji wa mkataba huo na kuagiza upelekwe mbele ya kamati hiyo ili wajumbe waweze kujadili.

Baada ya kukolea kwa sakata hilo bungeni, Spika wa Bunge, Job Ndugai, aliunda kamati ya uchunguzi iliyoongozwa na Aeshi.

Kamati iliyoundwa na Bunge ilikabidhi ripoti Ofisi ya Spika ambayo ilisema ingeishauri Serikali cha kufanya.

Mwishoni mwa Juni, mwaka juzi, Naibu Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson, aliiagiza Serikali kuhakikisha mfumo huo wa vifaa vya utambuzi wa vidole katika Jeshi la Polisi unafanya kazi ndani ya miezi mitatu kuanzia siku hiyo.

Dk. Tulia ambaye aliikabidhi Serikali matokeo ya uhakiki uliofanywa na kamati ndogo iliyoundwa, alisema ripoti ilikuwa na maoni, ushauri, mapendekezo ya namna na kutatua changamoto zilizoainishwa na taarifa ya PAC na alizuia wabunge kulijadili.

Hata hivyo, Aprili mwaka jana, sakata la Lugumi lilibuliwa tena na ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ambayo ilieleza kampuni hiyo ilifunga mashine vituo 36 tu kati ya 152.

 MBWA HOBBY

Kuhusu sakata la mbwa maalumu wa polisi wa kikosi cha Bandari anayefahamika kwa jina la Hobby, Lugola alikwepa kuweka wazi iwapo amepatikana ama la!

Hata alipobanwa na waandishi wa habari kuhusu mbwa huyo, alibakia kusisitiza tu kwamba suala la Kikosi cha Mbwa na Farasi, ameliacha lishughulikiwe na IGP Sirro.

Juzi baada ya kutoa saa kadhaa kwa IGP Sirro akimtaka ahakikishe mbwa huyo amepatikana, gazeti dada la hili, MTANZANIA Jumamosi, lilidokezwa na mmoja wa maofisa wa Kikosi cha Mbwa na Farasi kwamba mbwa huyo alikuwa hajapotea bali alipelekwa katika kikosi hicho kilichoko Kurasini, Dar es Salaam baada ya kukosekana chumba cha kulala bandarini.

Ofisa huyo ambaye alizungumza kwa sharti la kutotajwa jina gazetini kwa kuwa si msemaji, alisema kilichofanyika ni makosa ya kutoweka kumbukumbu katika vitabu.

Katika hilo la mbwa, Lugola alisema wakati akifanya ziara yake hiyo na kubaini changamoto hizo, alikutana na kukubalina na IGP Sirro kuzifanyia kazi pamoja na kuweka kumbukumbu vyema za mbwa hao hasa kuhusu idadi na matumizi.

“Nilibaini mapungufu ya idadi ya kukabidhiana ambayo ilikuwa ya leo tofauti na jana (siku ya ziara hiyo, Alhamisi). Kulitakiwa kuwe na mbwa sita, huyo hakuwepo. Nikaenda kikosini nikakuta changamoto. Nimekubaliana na IGP waingie kwa undani kuchunguza nini kimetokea kwenye kikosi hicho na wanipe taarifa. Tuachie chombo hicho kichunguze tuone nini cha kufanya,” alisema Lugola. 

AJALI

Kuhusu utatuzi wa ajali za barabarani, alisema Baraza la Taifa la Usalama Barabarani na kamati zake za mikoa na wilaya alilolivunja, ataliunda upya na ifikapo Julai 31 litakuwa tayari.

Alisema moja ya hatua zitakazochukuliwa sasa kudhibiti ajali barabarani, si tu kumkamata dereva, bali pia mmiliki iwapo itabainika alikabidhi gari likiwa bovu na watatakiwa kulala mahabusu kabla ya kufikishwa mahakamani.

Pia aliagiza dereva aliyeonywa zaidi ya mara tatu anyang’anywe leseni na arudi darasani na wamfanyie mazoezi upya.

Lugola pia aliliagiza Jeshi la Polisi kuongeza juhudi katika usimamizi wa Sheria ya Usalama Barabarani na ukaguzi wa magari ili kudhibiti ajali nchini.

 NIDA

Mbali na suala hilo, Lugola pia amemtaka Mkurugenzi wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) kufika ofisini kwake Dodoma Julai 25 akiwa na ama kampuni iliyoshindwa kuleta mtambo wa kutengeneza kadi ghafi za vitambulisho au fedha kiasi cha Dola za Marekani milioni 14 sawa na shilingi bilioni 32 walizopatiwa kwa ajili hiyo.

MAGEREZA

Kuhusu suala la wafungwa kujilisha ambalo limezungumzwa mara kadhaa na Rais Magufuli, alisema ameliagiza Jeshi la Magereza kupeleka mkakati madhubuti unaotekelezeka wa kujitosheleza kwa chakula ili kuipunguzia Serikali mzigo.

Alisema iwapo itabainika katika mkakati huo kuna vipengele vinazuia wafungwa kulima ili kujilisha na kulisha mahabusu pamoja na chakula kingine kuuzwa, basi kipengele hicho kitapelekwa Bunge lijalo kufanyiwa marekebisho.

Kuhusu suala la simu magerezani, alimwagiza Kamishna Jenerali wa Magereza, Phaustine Kasike, kusimamia kikamilifu nidhamu ya askari.

“Katika kikao changu na maofisa wa Magereza, nimemwagiza CGP kuwa gereza lolote ambalo litapatikana na matukio hayo, mkuu wa gereza atawajibika. Atapoteza sifa za kuwa Mkuu wa Jeshi la Magereza,” alisema.

MISHAHARA

Lugola pia amewaagiza wakuu wote ndani ya wizara yake ifikapo mwishoni mwa mwezi Agosti, kutatua kero ya muda mrefu ya askari na watumishi raia wa wizara hiyo kutobadilishiwa mishahara baada ya kupandishwa cheo.

 WAKIMBIZI, WAHAMIAJI HARAMU

Kuhusu suala la wakimbizi nchini, alisema alimwagiza Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Wakimbizi kuongeza kasi ya kuwarejesha wale wa Burundii kwa kuwa hivi sasa kuna amani.

Pia alimtaka kushirikiana na Idara ya Uhamiaji na Polisi kuwafuatilia wakimbizi waliotoroka kambini na kuwarejesha.

Pamoja na hilo, alimwelekeza Kamishna wa Uhamiaji kuongeza doria mipakani ili kudhibiti wahamiaji haramu pasipo visingizio vya vitendea kazi. 

RUSHWA

Alisema baada ya kubaini wapo baadhi ya askari wanajihusisha na vitendo vya rushwa na kuwabambikia kesi wananchi, wamekubaliana na IGP kuendelea kuchukua hatua kwa watakaobainika, huku akiwataka wanaokumbwa na kadhia hiyo kutoa taarifa. 

KUFANYA KAZI SAA 24

Alisema ili Watanzania waweze kukuza uchumi kwa kufanya kazi saa 24, alimwelekeza IGP Sirro kuwasilisha mikakati ya kuimarisha usalama.

Pia alisema Julai 31, atakutana na wadau wa usafirishaji ili kujua namna gani wanaweza kufanikisha kwa usalama magari kusafiri usiku.

ZIMAMOTO

Kuhusu  changamoto za magari ya Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji, Lugola alisema pamoja na hayo Kamishna Jenerali wa jeshi hilo anatakiwa kuhakikisha askari wake wanafika eneo la tukio mara baada ya kutokea janga ili kushirikiana na wananchi badala ya kukaka ofisini.

KUPAMBANA NA WANAOMKOSOA

Pia alisema atapambana na watu aliodai wanauaminisha umma kuwa hana mamlaka na baadhi ya maamuzi yake.

Pasipo kuwataja majina, alisema wamefika wawili, na kusisitiza anatekeleza wajibu wake vyema.

Ingawa Lugola hakutaja jina, lakini miongoni mwa watu waliopinga baadhi ya maamuzi yake ni Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), Fatma Karume, ambaye alisema waziri huyo hana mamlaka ya kumwamrisha Mkuu wa Jeshi la Polisi.

Mbali na hilo, Lugola pia alisema ametoa taarifa Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA) kushughulikia akaunti feki zinazomchafua na kusisitiza kuwa yeye binafsi hana akaunti kwenye mitandao ya kijamii.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles