27.1 C
Dar es Salaam
Thursday, January 2, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Baada ya Arusha rungu kutua wapi?

Na ANDREW MSECHU

JIJI la Arusha ni miongoni mwa majiji yenye pilikapilika nyingi za kiuchumi huku likitawaliwa na hamasa kubwa kisiasa, lakini pia ndiyo kitovu cha utalii nchini.

Wiki hii wakazi wa jiji hilo wameshuhudia hali ambayo haijapata kutokea. Kimsingi Jiji la Arusha limekuwa na matukio kadhaa yakiwamo ya uvunjifu wa amani.

Kuibuka kwa Askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na kuzingira baadhi ya maduka ya kubadilishia fedha, si tu kulishtua watu bali iliibuka ile dhana ya mwendelezo wa matukio ya jiji hilo.

Maswali kadhaa pia yaliibuka huku wengine wakidhani kuwa nchi imeingia kwenye machafuko kwa kuwa si jambo la kawaida JWTZ kuonekana katika mazingira ya namna ile.

 Licha ya majibu kutolewa siku ya pili baada ya tukio hilo, kutoka kwa Gavana wa Benki Kuu, Profesa Florens Luoga, hata hivyo liliibuka swali jingine kuwa ni kwanini Arusha ndiyo imetiliwa hofu kwenye maduka hayo ilhali  mikoa na majiji mengi yanatoa huduma kama hizo?

Hayo yote yanatokana na kile kinachoelezwa kuwa ni nguvu kubwa imetumika hasa kwa kulihusisha jeshi hilo.

Kama inavyofahamika wajibu mkuu wa vikosi vya JWTZ ni kulinda mipaka ya nchi dhidi ya wavamizi kutoka nje.

Jukumu linalofuata ni kushiriki katika oparesheni maalumu pale inapoonekana inafaa, katika uokozi wakati wa maafa, kuokoa maisha na mali wakati wa maafa na kusaidia kukarabati miundombinu yanapotokea maafa.

Wakati mwingine, majukumu ya JWTZ yanaweza kuwa kushughulikia matatizo makubwa ya kiusalama ambayo yamevishinda vyombo vinavyohusika na ulinzi wa watu na mali zao, hasa jeshi la polisi, kama ilivyotokea jeshi kuingilia kati baada ya taarifa za kuwepo kwa vikosi vya magaidi katika mapango ya Amboni Tanga mwaka 2015.

Wajibu mwingine inaweza kuwa kushiriki katika vikosi vya kimataifa vya ulinzi wa amani katika mataifa ambayo amani imetoweka, pale inapoonekana inafaa.

Kwa askari wa JWTZ kuonekana katika maduka ya kubadilishia fedha kuanzia Jumatatu asubuhi Novemba 19, mwaka huu lilikuwa jambo la kushtusha, ambalo halikuwahi kufikiriwa.

Hata hivyo katika ufafanuzi wake, Gavana Luoga, amesema ukaguzi huo uliofanyika katika baadhi ya maduka ya kubadilishia fedha uliendeshwa na taasisi yake kwa kushirikisha vyombo vya dola ili kubaini watuhumiwa wa uhalifu wa kutakatisha fedha.

Aidha, ameeleza kuwa ililazimika kufanya hivyo kwa kuwa askari polisi wengi walikuwa kwenye usimamizi wa mitihani ya kidato cha pili. Hata hivyo amesema taasisi yake ilihusisha JWTZ wasio na silaha ili kuongeza nguvu katika kufanikisha mpango huo.

Profesa Luoga anasema ukaguzi huo wa kushtukiza uliyalenga baadhi ya maduka bubu Arusha na ulifanyika kutokana na maofisa wa Serikali kubaini kwamba wafanyabiashara hutumia njia mbalimbali kukwepa mkono wa sheria.

Anasema msako huo ulipangwa na Kitengo cha Ukaguzi cha Benki Kuu BoT na ulifanywa baada ya misako mingine miwili kufanyika awali, ambayo haileta mafanikio makubwa.

Anaeleza kuwa uchunguzi wa kina katika miezi sita iliyopita ulibaini kuongezeka kwa biashara za kubadilisha fedha kinyume cha sheria, na kukua kwa biashara haramu ya fedha za kigeni na utakatishaji fedha, hususan kupitia maduka ya kubadilisha fedha na kwa kuwa juhudi za kitengo cha ukaguzi kuwapata wahusika hazikuzaa matunda katika oparesheni mbili zilizopita, hivyo iliandaliwa oparesheni nyingine wiki hii.

Pamoja na mambo mengine amesema  uchunguzi uliofanyika umebaini waendeshaji wengi wa maduka ya kubadilisha fedha hawakukidhi vigezo vyote japokuwa leseni zilitolewa kwao baada ya taarifa kupotoshwa.

Gavana Luoga amesisitiza kuwa mtu yeyote anayejua kuwa upatikanaji wa leseni yake una dosari anapaswa kurejesha leseni hiyo kwa hiyari.

Anaeleza kuwa wote wanaoendesha maduka ya kubadilisha fedha bila leseni au kwa kutumia leseni zisizo zao wanatakiwa kufunga maduka hayo mara moja kabla hawajafikiwa na mkono wa sheria.

Anasisitiza iligundulika kuwa kuna mtandao mpana na madhubuti wa shughuli hizo na ambao ulilenga kuhakikisha kuwa shughuli za udhibiti hazifanikiwi hivyo baada ya mashauriano na wataalamu na kushirikisha vyombo vya upelelezi na usimamizi ilionekana kuwa ili kufanikisha zoezi lililokusudiwa ni muhimu wahusika wote wadhibitiwe kwa wakati mmoja na kufanyiwa ukaguzi.

Gavana huyo anasema ilihitaji ushiriki wa maofisa wengi sana kutoka vyombo mbalimbali na kuhakikisha kila mahali ambapo ukaguzi uliendeshwa kuna usalama wa kutosha na Wananchi wanaarifiwa kutoingia sehemu husika kwa wakati huo.

Pamoja na ufafanuzi huo bado kuna maswali mengi licha ya kutotumia silaha, maelezo kuwa askari polisi walikuwa kwenye usimamizi wa mitihani ya kidato cha pili mkoani humo hayajaondoa kiu ya uzito wa tukio hilo ulivyofanyika.

Ufafanuzi wa Profesa Luoga ulihitaji kueleza sababu za kina za kwanini  JWTZ limetumika katika oparesheni hiyo, au BoT imepoteza imani na watendaji wa mkoa huo?

Ni muhimu Gavana Luoga aeleze kama oparesheni hiyo itaendelea katika mikoa mingine au la, ili kuondoa sintofahamu iliyoibuka baada ya kusambaa kwa askari wa JWTZ katika maduka hayo jijini humo.

Tunahitaji kujua matokeo ya oparesheni hiyo, iwapo wafanyabiashara waliokutwa wakiendesha biashara hiyo wamechukuliwa hatua gani? Wamefilisiwa? Wamepelekwa mahakamani? Je; itahusisha na mikoa mingine?

Kwa namna oparesheni hiyo ya ukaguzi ilivyoendeshwa, inaonekana hatua ya kutumia askari wa JWTZ ilikuwa na nia pana zaidi.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles