*Yaichapa Mbeya City 2-1, African Sports yazinduka
ABDUCADO EMMANUEL DAR NA OSCAR ASSENGA, TANGA
TIMU ya soka ya Azam FC jana iliendeleza wimbi la ushindi kwenye michuano ya Ligi Kuu Tanzania Bara na kuzidi kuifukuzia Yanga kileleni baada ya kufanikiwa kuichapa Mbeya City mabao 2-1 katika mchezo uliochezwa Uwanja wa Azam Complex.
Ushindi wa Azam kwa Mbeya City umekuwa ni kwanza kwenye uwanja huo kutokana na historia ya timu hizo kila zinapokutana kuishia kupata matokeo ya sare.
Kwa matokeo hayo Azam imepanda hadi nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi hiyo ikiipumulia Yanga na kuishusha Mtibwa Sugar nafasi ya tatu zote zikiwa zimejikusanyia pointi 12 baada ya kushuka dimbani mara nne zikitofautiana kwa mabao ya kufunga.
Vinara, Yanga ambao ni mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, wamepachika wavuni mabao 11 na kuruhusu kufungwa bao moja, Azam wamefunga mara saba na kufungwa mawili huku Mtibwa wakiwa na mabao sita na kuruhusu nyavu zao kutikiswa mara mbili.
Katika mchezo huo, Azam waliandika bao la kuongoza dakika ya 10 kupitia kwa Mudathir Yahaya aliyepiga shuti kali lililomshinda kipa wa Mbeya City, Hanington Kalyesubula, baada ya pasi aliyompigia John Bocco kuokolewa na mabeki kabla ya kumkuta mfungaji.
Dakika ya 30 beki, Shomari Kapombe aliikosesha timu yake bao la wazi baada ya kushindwa kumalizia krosi iliyochongwa na Farid Maliki aliyepiga shuti ambalo lilitoka nje baada ya Kipre Tchetche kuukosa mpira huo.
Mbeya City waliendeleza kasi ya mashambulizi langoni kwa Azam ambapo dakika ya 32, Joseph Mahundi alipiga shuti kali lililopanguliwa na kipa Aishi Manula na kuwa kona ambayo haikuzaa matunda.
Kipindi cha kwanza mwamuzi, Martin Saanya, aliwaonya kwa kadi za njano kiungo wa Azam, Salum Abubakar ‘Sure Boy’ kwa kumchezea rafu Mahundi na Manula kwa kuchelewesha muda.
Dakika ya 45, George Mlawa wa Mbeya City alijaribu kufanya shambulizi kwa Azam lakini shuti alilopiga akiwa nje ya eneo la hatari liligonga mwamba na kudakwa na kipa kabla ya John Kabanda kukosa bao dakika ya 50 baada ya shuti lake kutoka nje ya lango kwa sentimita chache.
Tchetche aliipatia Azam bao la pili dakika ya 53 baada ya kufanya maarifa ya kumtoa golini kipa wa Mbeya City na kupiga shuti la kiufundi lililowapita mabeki na kutinga wavuni.
Bao hilo liliwazindua wachezaji wa Mbeya City ambapo dakika ya 56, Raphael Alpha, aliiandikia timu yake bao baada ya kugongeana pasi vizuri na wenzake na kuachia shuti kali akiwa ndani ya eneo la 18 lililomshinda kipa wa Azam.
Timu zote zilishambuliana kwa zamu kipindi cha pili na kuongeza kasi ya mchezo tofauti na awali ambapo Mbeya City walikuwa wakipoteza mipira mara kwa mara.
Kocha Mwingireza Stewart Hall wa Azam alifanya mabadiliko ya kuwatoa Mudathir na Tchetche kipindi cha pili na nafasi zao kuchukuliwa na Himid Mao na Allan Wanga huku Mbeya City wakimtoa Mlawa na kumwingiza David Kambole.
Katika hali isiyo ya kawaida, shabiki mmoja wa Mbeya City alikatiza uwanjani wakati mchezo unaendelea akitokea jukwaani na kuelekea kwenye benchi la ufundi la timu hiyo kabla ya polisi kumdaka na kumweka chini ya ulinzi na kumtoa nje ya uwanja.
Katika tukio lingine nahodha wa Mbeya City, Juma Nyosso, alifanya kwa mara nyingine kitendo cha udhalilishaji kwa Bocco wakati wachezaji wakiwa wamemzonga mwamuzi baada ya Mahundi kuangushwa chini.
Tukio hilo ni la pili kwa beki huyo ambapo mara ya kwanza alimdhalilisha aliyekuwa mshambuliaji wa Simba, Elius Maguli, wakati timu hizo zilipokutana msimu uliopita na Mbeya City kushinda mabao 2-1.
Kutokana na kosa hilo la msimu uliopita, Nyosso alifungiwa kucheza mechi nane za Ligi Kuu na Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Azam: Aishi Manula, Shomari Kapombe, David Mantika, Racine Diof, Serge Pascal Wawa, Jean Baptist Muguraneza, Salum Abubakar, Mudathir Yahya/Himid Mao, John Bocco, Kipre Tchetche/Allan Wanga na Farid Mussa
Mbeya City: Hanington Kalyesubula, John Kabanda, Hassan Mwasapili, Juma Nyosso, Christian Sembuli, Steven Mazanda, Richard Peter, Raphael Alpha, George Mlawa/David Kambole, Themi Felix na Joseph Mahundi.
Katika mchezo mwingine wa ligi hiyo, African Sports imezinduka na kuichapa Ndanda FC bao 1-0 katika mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
Bao pekee na la ushindi kwa African Sports lilipachikwa wavuni dakika ya 57 kupitia kwa Hassan Materema aliyeunganisha vema pasi ya Ally Hassan.