TIMU ya soka ya Azam FC jana ilikiona cha moto kwenye michuano ya Ligi Kuu Tanzania Bara, baada ya kushindwa kufurukuta mbele ya Coastal Union na kupata kipigo cha bao 1-0 ugenini katika pambano lililopigwa Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
Kipigo hicho ni cha kwanza kwa Azam tangu kuanza kwa Ligi Kuu msimu huu, ambapo Coastal Union wameweza kutibua rekodi yao ya kutofungwa baada ya awali kuiharibia Yanga na kuichapa mabao 2-0.
Matokeo ya jana yameifanya Azam iendelee kubaki nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi ikiwa imejikusanyia pointi 42 nyuma ya vinara Simba wenye pointi 45 wakifuatiwa na Yanga waliopo nafasi ya pili kwa kufikisha pointi 43.
Katika mchezo wa jana ambao ulitawaliwa na upinzani mkubwa, Azam walikosa nafasi ya wazi dakika ya 14 baada ya shuti lililopigwa na mshambuliaji, John Bocco, kutoka nje ya lango.
Coastal ambao walipania kupata ushindi nyumbani, walijibu mapigo kwa kufanya shambulizi kali dakika ya 29 lakini Juma Mahadhi, akiwa katika nafasi nzuri alipiga shuti hafifu lililodakwa kirahisi na kipa Aishi Manula wa Azam.
Timu zote zilikwenda mapumziko zikiwa hazijafungana, lakini Coastal walianza kipindi cha pili kwa kasi na kufanikiwa kufunga bao pekee la ushindi dakika ya 67 kupitia kwa Miraji Adam aliyepiga shuti kali la mpira wa faulo na kujaa wavuni.
Baada ya bao hilo Azam walimtoa mshambuliaji Allan Wanga na nafasi yake kuchukuliwa na Kipre Tchetche na Coastal kumtoa Ally Shibol na kumwingiza Ayoub Yahya, lakini mabadiliko hayo hayakuzaa matunda kwa pande zote mbili.
Coastal imekuwa timu pekee msimu huu ambayo imetibua rekodi za kutofungwa kwa vigogo Yanga na Azam Ligi Kuu katika mzunguko wa kwanza, kwa kuutumia vyema uwanja wake wa nyumbani.
Kikosi cha Coastal ambacho kinanolewa na kocha Ally Jangalu baada ya Mganda, Jackson Mayanja kutimkia Simba, kimeanza kuonyesha mafanikio makubwa mzunguko wa pili na kufufua matumaini ya kubaki Ligi Kuu.