27.1 C
Dar es Salaam
Thursday, January 2, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Azam kukabiliana na hujuma za Merreikh

azamNA ABDUCADO EMMANUEL, DAR ES SALAAM

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Azam FC wamejipanga kukabiliana na hujuma zozote kutoka kwa El Merreikh katika mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika.

Azam juzi iliwafunga miamba hiyo ya Sudan mabao 2-0 katika mchezo wa kwanza uliofanyika Uwanja wa Azam Complex, mchezo wa marudiano utafanyika jijini Khartoum, Sudan.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Katibu Mkuu wa Azam, Nassor Idrissa, alisema wanajua mbinu chafu za nje ya uwanja zinazotumiwa na El Merreikh, lakini wameandaa kikosi kazi kwaajili ya kukabiliana na hayo.

“El Merreikh imekuwa na historia hiyo ya kuwafanyia vurugu timu pinzani na hujuma nyingine nje ya uwanja, ili kuwaathiri kisaikolojia timu inayocheza nayo.

“Kwa kukabiliana na hilo,tumeandaa timu ya watu kadhaa ambayo itatangulia kuandaa ujio wa timu yetu. Lakini kabla ya hayo tayari kuna watu tulishawatuma Sudan kuandaa mazingira ya kufikia timu na wamesharudi baada ya kumaliza kazi hiyo,” alisema.

Idrissa alisema hata wachezaji wao watawaandaa kisaikolojia kupambana na hujuma kama hizo, ili kutimiza lengo la kulinda ushindi wao na kufuzukwa hatua 32 bora.

Akizungumzia kama watasafiri na maji na vyakula vyao, Idrissa alisema: “Tulitamani kufanya hivyo ili kujihakikishia chakula safi tukiwa kule, lakini kuna baadhi ya Watanzania wanaoishi kule watatuandalia kila kitu tutakachotumia Sudan.”
Wakati huo huo, Kocha wa Azam, Joseph Omog, ameeleza kuwa watajipanga zaidi kwaajili ya mchezo wa marudiano, huku akikiri ugumu kwenye mchezo huo.

“Mchezo wa ugenini utakuwa mgumu kuliko huu wa nyumbani, hivyo nitatumia michezo miwili ijayo ya ligi (Ruvu Shooting na Tanzania Prisons), kuweza kujiandaa na mchezo huo ila kikubwa inahitaji umakini wa hali ya juu,” alisema.

Naye Kocha wa Merreikh, Diego Garzitto, alisema timu yake inahitaji kufunga mabao matatu hadi manne bila kufungwa bao lolote, akidai wataanza kwanza kwa kufunga mabao mawili ya haraka kwenye mchezo huo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles