Na Wifrida Mtoi, Dar es Salaam
Timu ya Azam FC imetamba kuwa katika mchezo wa kesho wa Ligi Kuu Tanzania Bara, hawatamuacha salama Biashara United kwa sababu lengo ni kuchukua pointi tatu.
Kocha Msaidizi wa kikosi hicho, Vivier Bahati, amesema hawawezi kumuachia nafasi Biashara United japo wanafahamu ni timu ngumu lakini watapambana ndani ya dakika zote 90 ili kutafuta kile wanachokihitaji.
Amesema wachezaji wote wako vizuri kulingana na kiwango walichokionesha mazoezini, kila mmoja atapewa jukumu lake la kufanya uwanjani.
“Tunaelewa ubora wa Biashara, kila timu inayoshiriki ligi ina ubaya wake na uzuri wake, lakini sisi tutaangalia udhaifu wao uko wapi na kutumia nafasi tunazozipata,” amesema Bahati.
Kwa upande wake, nahodha wa Azam FC, Aggrey Morris, amesema wapo katika morali ya juu wanasubiri tu siku ifike waingie uwanjani.