Na Mwandishi wetu,
Waziri wa Maji Jumaa Aweso, amehitimisha ziara yake mkoani Arusha jana usiku huku akitoa mwafaka wa mradi wa maji katika vijiji vitatu wilayani humo.
Pamoja na mambo mengine, akiwa mkoani Arusha, Waziri Aweso amekagua ujenzi wa miundombinu ya mradi wa maji katika Kijiji cha Ligamba, wilayani Arumeru.
Katika ziara hiyo, Aweso amefanya kikao na madiwani wa eneo hilo jana usiku ambapo alifanya maamuzi ya kukamilisha mradi huo ambao kwa sasa umefika asilimia 80 ya utekelezaji wake.
Aweso alitumia nafasi hiyo kuzungumza moja kwa moja na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga kwa njia ya simu na kufikia muafaka kuwa sehemu iliyobaki ya ujenzi imalizike ili wananchi waanze kupata huduma ya maji.
Mradi huu unasimamiwa na Wakala wa Usambazaji Maji Vijijini (RUWASA) na utanufaisha zaidi ya wakazi 6,244 wa vjiji vitatu ambavyo ni Ligamba, Oleitushura na Nengungu.