Na Mwandishi wetu, Tabora
MKUU wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri, amekabidhi vitambulisho 12,000 vya wajasiriamali wadogo wadogo ili waweze kuvitumia wanapotekeleza majukumu yao.
Hii ni awamu ya pili ya ugawaji wa vitambulisho hivyo kwa wajasiriamali wadogo tangu Rais John Magufuli, azindue zoezi hilo kwa kutoa vitambulisho ambavyo viuzwa Sh 20,000 kwa kila mfanyabiashara mdogo.
Vitambulisho hivyo vimekabidhiwa jana kwa wakuu wa wilaya zote za Mkoa wa Tabora kwa ajili ya kuwagawia wajasiriamali ambao sifa zao zinakizi kupewa vitambulisho hivyo.
Alisema halmashauri ya Wilaya ya Igunga imepata vitambulisho 1,500, Nzega Mji 2,000, Uyui 2,000 na Manispaa ya Tabora 2,000.
Mwanri alisema Halmashauri ya Wilaya ya Nzega imepata vitambulisho 2,000, Sikonge 500, Urambo 1,000 na Kaliua 1,000.
Aliwataka wakuu wa wilaya kushirikiana na watendaji katika kuhakikisha vitambulisho vyote vilivyotolewa kwenye awamu ya kwanza vinamalizika mapema na kwa walengwa sahihi.
Awali Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoani Tabora, Thomas Masese, alisema mkoa huo umepewa lengo la kugawa vitambulisho 71,500 ndani ya mwaka huu.
Alisema katika awamu ya kwanza wamepata vitambulisho 12,000 na vimebaki 59,500.
Masese alisema ugawaji wa viambulisho hivyo unaokana na mabadiliko ya Sheria ya Usimamizi wa Kodi ya mwaka 2015.
Alisema wakati wa ugawaji wa vitambulisho kwa walengwa ni lazima kumbukumbu muhimu kama vile sehemu ziwekwe ili kuepuka udanganyifu.