SENETA Larissa Waters kutoka Jimbo la Queensland nchini Australia alifanya kitendo katika sakafu za Bunge la taifa hilo Jumanne wiki hii ambacho ijapokuwa si kigeni lakini pia kilichokuwa cha kimapinduzi.
Ni kwa kumnyonyesha mwanawe mwenye umri wa miezi miwili, Alia Joy katika ukumbi wa Bunge hilo huku likiendelea na mjadala.
Ni kwa sababu mbali ya taratibu za mabunge mengi duniani kutoruhusu kitendo kama hicho, kwa baadhi unyonyeshaji mtoto huku ukiendelea na shughuli zako mahali pa kazi ni kama vile ni mwiko.
Ni kitu ambacho kinaweza kukufanya ukumbane na mvua ya matusi kutoka kwa wale wanaojifanya wajuaji au wasiofurahishwa kweli na unyonyeshaji wa hadharani.
Lakini Larissa Waters kama mwanaharakati wa haki za wanawake ni miongoni mwa wanaotaka kubadili fikra kama hizo.
Hivyo, ametengeneza historia nchini Australia kwa kuwa mwanamama wa kwanza kumnyonyesha mtoto wake mwenye umri wa miezi miwili ndani ya ukumbi wa Bunge.
Bintiye Alia Joy Waters pia akaweka rekodi ya kuwa mtoto wa kwanza kunyonyeshwa bungeni.
Katika kile kinachoonekana kuwa alidhamiria ili kuunga mkono harakati za utetezi wa haki za wanawake, seneta huyo ambaye ndiyo amerudi kutoka likizo yake ya uzazi aliingia katika mitandao ya jamii kumpongeza mwanawe kwa kuwa wa kwanza kunyonyeshwa katika Bunge la Australia.
Aliongeza kwamba wanawake zaidi wanahitajika bungeni.
“Ninajisikia fahari mno kuwa mtoto wangu Alia ni wa kwanza kunyonya katika Bunge la shirikisho! Tunahitaji wanawake zaidi na wazazi bungeni,” alisema.
Kitendo hiki kitakuwa kichocheo zaidi si tu nchini Australia bali kote duniani katika utoaji wa haki za wasichana, wanawake na wazazi.
“Na tunahitaji mazingira bora katika maeneo ya kazi kwa uangalizi mzuri wa watoto kwa kila mtu,” alisema Naibu kiongozi huyo mwenza wa Chama cha Kijani cha Australia katika ukurasa wake wa facebook.
Bunge la Australia lilibadili sheria zake mwaka jana kuwaruhusu wanawake kunyonyesha watoto wakiwa bungeni kwa vile awali hawakuruhusiwa ukiondoa kufanya hivyo katika vyumba maalumu.
Seneta mwingine wa Chama cha Labour, Katy Gallagher alisema kuwa wakati huo unapaswa kutambuliwa.
“Wanawake wamekuwa wakinyonyesha katika mabunge tofauti duniani,” alikiambia chombo cha habari cha Skynews Australia.
Alisema; “Wanawake wataendelea kuwa na watoto na iwapo wanataka kufanya kazi zao na wawe kazini na kuangalia watoto wao…basi bila shaka ukweli ni kwamba tutalazimika kuwapatia haki yao.”
Hadi kufikia mwaka uliopita, wabunge katika Bunge dogo walikuwa wanaweza kuwabeba watoto wao na kuingia katika ofisi za bunge pekee ama maeneo ya umma.
Hata hivyo, suala la unyonyeshaji watoto bungeni licha ya kupitishwa katika baadhi ya nchi ni suala tata katika mabunge mengi duniani.
Mnamo mwaka 2016, katika Bunge la Hispania, mbunge Carolina Bescansa kutoka chama cha Podemos alikosolewa na kupongezwa pia kwa kumpeleka mwanawe bungeni na kumnyonyesha.
Mwaka 2009, Seneta Sarah Hanson na mwanawe mwenye umri wa miaka miwili Kora walitimuliwa kutoka bungeni nchini Australia kwa katika hali ya kufedhehesha.