DORTMUND, UJERUMANI
UONGOZI wa klabu ya Borussia Dortmund, jana uliamua kuachana na mshambuliaji wake, Pierre-Emerick Aubameyang, katika mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Stuttgart kutokana na kuchukuliwa hatua ya kinidhamu.
Hatua hiyo ilichukuliwa kutokana na mchezaji huyo kutumia siku mbili za mapumziko yake kwenda Barcelona kuungana na mchezaji mwenzake wa timu hiyo, Ousmane Dembele na baadaye akaonekana akiwa kwenye kumbi za starehe za klabu ya Barcelona.
Inadiwa kuwa mchezaji huyo alikwenda nchini Hispania bila taarifa kwa uongozi wa klabu hiyo, hivyo Dortmund wakaamua kumchukulia hatua kwa kumsimamisha kwenye mchezo huo wa jana.
Hata hivyo, klabu hiyo imedai kuwa kamati ya nidhamu ipo kwenye mipango ya kumchukulia hatua kutokana na kitendo hicho alichokifanya.
Si mara ya kwanza kwa mchezaji huyo kufanya kosa kama hilo, msimu uliopita aliwahi kuondoka kwenye klabu hiyo bila taarifa na kuelekea nchini Italia kwenye sherehe ya siku ya kuzaliwa kwa rafiki yake huku klabu yake ikijiandaa na mchezo wa Ligi ya Mabingwa, hivyo Dortmund waliamua kumsimamisha kucheza mchezo mmoja dhidi ya Sporting Lisbon.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 28, amekuwa akitupiwa lawama kipindi cha hivi karibuni kutokana na kushindwa kuonesha uwezo wake, ikiwa amecheza jumla ya michezo saba katika michuano mbalimbali na kupachika bao moja.
Mara ya mwisho mchezaji huyo kufunga mabao mawili ilikuwa kwenye mchezo wa Ligi Kuu nchini Ujerumani dhidi ya RB Leipzig, ambapo Dortmund ilifanikiwa kushinda mabao 3-2, Oktoba 14.
Safari ya mchezaji huyo katika klabu ya Barcelona inahusishwa na tetesi za kutaka kujiunga na wababe hao wa nchini Hispania ili kuungana na rafiki yake ambaye alikuwa anashirikiana vizuri ndani ya Dortmund, Dembele.