29.2 C
Dar es Salaam
Sunday, January 5, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

ASKOFU SHOO: KANISA HALITAZIBWA MDOMO

*Awanya viongozi wa kisiasa, Serikali watakaojaribu kufanya hivyo

*Aeleza jinsi maaskofu KKKT walivyofunga kabla ya kutoa waraka

 

Na WAANDISHI WETU-KILIMANJARO/DAR


ASKOFU Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk. Fredrick Shoo, amewaonya watu wanaotaka kuwazuia au kuwaziba midomo viongozi wa dini wanapokemea  maovu yanayotokea nchini.

Amesema asitokee mtu yeyote nchini, awe kiongozi wa kisiasa au wa Serikali ambaye atajaribu kuwazuia au kuwaziba midomo viongozi wa dini wasikemee na kuonya juu ya maovu yanayotokea nchini.

Askofu Dk. Shoo alitoa onyyo hilo jana wilayani Hai, Mkoa wa Kilimanjaro alipokuwa akizungumza kwenye ibada maalumu ya kustaafu kwa aliyekuwa Mchungaji wa Usharika wa Masama Kati, Dayosisi ya Kaskazini, John Mshau.

Askofu Dk. Shoo ambaye pia ni Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini, amewataka wanasiasa wasitumie nafasi zao kuligawa taifa kwa sababu halitakaa kimya dhidi ya maovu.

“Wajibu wa viongozi wa dini ni kuonya na kukemea juu ya mabaya yanayoendelea nchini.

“Kwa hiyo, asitokee mtu yeyote wa kuwazuia viongozi wa dini kufanya wajibu huo kwani ni sawa na kupingana na Mungu.

“Wajibu wetu ni kuonya, kushauri, kukema na tunatenda hivyo tukitaka asijaribu mtu yeyote kutuzuia kufanya hivyo  kwani neno la Mungu linasema Bwana hutegemea wenye upole na huangusha chini wenye hila.

“Kwa hiyo sisi viongozi wa dini, hatutakubali kunyamaza, tutasema na kukemea maovu.

“Wanasiasa msije mkaigawa nchi katika vipande vipande kwa sababu Tanzania ni yetu sote, mkitaka kuipeleka mahali pabaya, sisi viongozi wa dini hatutanyamaza na kuwaacha mfanye mtakavyo, tutawakemea tu,” alisema Askofu Dk. Shoo.

Akitolea ufafanuzi waraka uliotolewa juzi na Baraza la Maaskofu wa KKKT, Askofu Dk. Shoo alisema uliandaliwa Machi 15, mwaka huu na maaskofu 27 wa baraza hilo.

Kwa mujibu wa Askofu Dk. Shoo, kabla ya kutoa tamko hilo maaskofu hao walifunga na kuomba Mungu ili wapate ujumbe sahihi watakaoutoa kwa waumini wao na Taifa kwa ujumla.

“Waraka huu ni matokeo ya kufunga na kuomba kwa muda mrefu tu na ni matokeo ya kukaa na kutafakari  kwa  utulivu na kwa unyenyekevu.

“Tuliomba sana na kumsihi Mungu ili atupe ujumbe tutakaoutoa siyo tu kwa waumini wa kanisa bali kwa Taifa zima. Baada ya kuupata ujumbe huo, tukaona hatuwezi kukaa kimya, bali tuutoe hata kama ni mzito na unatisha.

“Kwa hiyo, pasitokee kikundi cha watu wakafikiri wanaweza  kupinga sauti ya unabii ya kanisa.

“Hatuwezi kunyamaza na ninaomba wajue kutofautisha sauti ya unabii ya Mungu na propaganda za  kisiasa zinazopigwa huko.

“Tutofautishe ushabiki na kauli mbiu za kisiasa na matamko ambayo misingi yake ni uzalendo na upendo wa dhati kwa nchi kwani waraka tulioutoa ni neno la kinabii,” alisema.

Askofu Dk. Shoo aliwataka Watanzania kuupokea  na kuutafakari ujumbe huo kwa umakini na kwa hekima kubwa ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wanatumia muda mwingi kuliombea taifa.

“Niwasihi Watanzania wote tupokee ujumbe huu  na tuutafakari kwa umakini na tuombe Mungu atupe macho ya rohoni ya kupata ufahamu wa kuelewa  Mungu anataka kutwambia nini kwa ajili ya nchi yetu na siyo kwa kukurupuka.

“Pia, Watanzania wekeni pembeni itikadi za vyama vya  kisiasa  na tutumie muda mwingi  kutafakari ni kitu gani Mungu anataka kutufunulia  katika nchi yetu kwa sababu kuna baadhi ya maovu yakiwamo ukatili  unaoendelea nchini ambao haumpendezi Mungu.

“Kuna mambo tumeyataja katika waraka wetu na mimi nasema mkayatafakari na pia yale ya kuunga mkono na kuendelea kuyatenda kwa ajili ya taifa letu, tuyaunge mkono lakini yale ambayo ni ya kuyakataa na kuyakemea,  tuyakemee na kuyaacha kabisa,” alisema Askofu Dk. Shoo.

Kwa mujibu wa Askofu Dk. Shoo, anaamini Watanzania wakimsikiliza Mungu juu ya anayoyataka ikiwa ni pamoja na kuvumiliana licha ya tofauti zao, Tanzania itakuwa na amani na utulivu zaidi.

“Naogopa sana kukaa kwenye nchi ambayo watu wana hofu juu ya maisha yao na uhai wao, hiyo ni hatari kubwa. Kwa hiyo, ndugu zangu kupitia waraka huu, tukae na tutafakari na kuona ni wapi Mungu anataka tubadilike.

“Nafahamu kuna watu wameupokea kwa namna tofauti,  lakini tuangalie nia njema iliyopo katika waraka ule na si vinginevyo  na naomba huu uwe mchango wetu kwa ajili ya nchi yetu.

“Sisi kama viongozi wa dini, tumefanya hivyo kwa kumheshimu Mungu kwa kutambua  nafasi yetu na utume tuliopewa. Najua kunaweza kujengeka dhana, kwamba ujumbe huu ni wa chama fulani au wa itikadi fulani.

“Jibu la hilo ni hapana, tumefanya hivyo kama wajibu wetu na kamwe hatutatoa ujumbe wa Mungu  kwa sababu ya kuwa upande fulani wa kisiasa, haiwezekani,” alisisitiza Askofu Dk Shoo.

Awali, akizungumza baada ya Mchungaji Kiongozi wa Usharika huo, Pray Usiri kuusoma waraka huo kanisani hapo, Askofu Mstaafu wa Dayosisis ya Kaskazini, Martine Shao alisema kitendo kilichofanywa na baraza la maaskofu ni cha kuungwa mkono.

“Nawapongeza maaskofu wote wa Baraza la Maaskofu wa KKKT kwani kitendo cha kuandika waraka huo kimeiamsha jamii na kujua kuna viongozi wa dini na wanaona yanayoendelea nchini.

“Kwa hiyo, napenda kuwafahamisha maaskofu wetu kwamba sisi tupo nyuma yenu na tunawaunga mkono.

“Pia, viongozi wote wa dini hakikisheni mnasimama imara ili kuhakikisha mnapigania maslahi mapana ya taifa kwa kuonya na kukemea yale yote ambayo kwa namna moja au nyingine yameonekana kuharibu taswira ya nchi.

“Viongozi wa dini, kumbukeni ninyi ndiyo mmebeba dhamana ya wananchi wote hivyo tunawatia moyo msikate tamaa kwani vita iliyopo mbele yenu ni kubwa.

“Tunawaomba msiyumbishwe, simamieni haki na kuwatetea wananchi,” alisema Askofu Mstaafu Shao.

 

Kwa habari zaidi jipatie nakala ya gazeti la MTANZANIA.

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

  1. Kama ni kweli juu ya waraka huu na hauna mwelekeo wa mikakati ya kisiasa tunashukuru ,lakini vinginevyo tujihadhari. Viongozi wa kidini pia wana misimamo yao ya kisiasa na walishindwa kuificha wakati wa uchaguzi uliopita.Hii ndiyo inatuchanganya waumini. Sisi hatupendi kuchanganya siasa na dini kwani siasa ni vitu vya nyakati na dini ni ya kudumu. Kuna mambo yanayofaa kwa wakati kisiasa na lisituvuruge katika imani zetu. Hatujazuiwa kuchangia kisiasa kama binafsi lakini misimamo ya kijumuia inabidi tuitafakari sana .

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles